Kuongeza au kupunguza makali ya maisha ndicho kitu kinachosubiriwa na
wananchi leo wakati Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango
atakapowasilisha bajeti ya pili ya Serikali ya Awamu ya Tano bungeni
mjini hapa.
Bajeti ya kwanza ya Sh29.5 trilioni ilionekana kubana sehemu tofauti na
kusababisha wananchi wa kila nyanja kulalamika, wengi wakisema mzunguko
wa fedha umedhoofika huku biashara zikifungwa.
Bajeti hiyo ndiyo iliyowafanya wachambuzi wa masuala ya uchumi, makundi
ya biashara na wabunge kumtaka waziri huyo atangaze hatua mahususi za
kuiokoa sekta binafsi na zitakazoharakisha ukuaji uchumi.
Wadau wanatarajia kuwa Dk Mpango, ambaye aliwahi kuwa mchumi mwandamizi
katika Benki ya Dunia na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), ataangalia kwa kina hali ya sasa ya uchumi na kutangaza hatua za
kikodi zitakazozuia kupanda kwa gharama za maisha na wakati huo huo
kuipa mkono sekta binafsi ili Serikali ifikie lengo lake kuifanya
Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
Mfumuko wa bei, ambao unahusishwa na kupanda kwa bei za vyakula, tayari
umefika asilimia 6.4 kwa mwezi Aprili kutoka asilimia 5.1 mwezi kama huo
mwaka jana.
“Kwa wengine, hili linaweza kuonekana kama ongezeko dogo lakini kiuchumi
ni kubwa mno na tunatarajia serikali inakuja na namna nzuri ya
kukabiliana nao katika bajeti hii,” alisema David Silinde, waziri
kivuli wa Fedha na Mipango na mbunge wa Momba (Chadema).
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.