ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, May 11, 2017

NA ANNASTAZIA MAGINGA,Mwanza

KUFUATIA
uwepo wa baadhi za shule zisizokuwa na sifa, Mthibiti Mkuu wa Ubora wa Shule Kanda ya Ziwa, Michael Cheyo, ameifunga moja kwa moja Shule ya Elite English Medium iliyopo wilayani Nyamagana jijini Mwanza kutokana na kujiendesha bila kibali kutoka serikalini.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Cheyo amesema kwamba amechukua hatua hiyo baada ya kukagua na kuthibitisha kuwa shule hiyo haina vigezo vya kuihalalisha kutoa huduma ya elimu kwa
watoto.

Kwa mujibu wa amri hiyo iliyotolewa kwa maandishi Aprili 6, mwaka huu, uongozi wa shule hiyo yenye wanafunzi 139 wa chekechea hadi darasa la pili, umetakiwa kuwahamishia wanafunzi hao kwenye shule zenye usajili kutoka mamlaka husika serikalini.

Licha ya shule hiyo kutokuwa na kibali cha kutoa huduma hiyo kutoka kwa Kamishina wa Elimu nchini, ukaguzi ulibaini kutokuwepo na walimu wenye sifa na kwamba  wanafunzi waliokuwepo wamekuwa wakitumia choo ambacho hakijaezekwa.

Cheyo ameeleza kwamba baada ya kufanya ucunguzi wamebaini shule hiyo ilianza kutoa huduma ya elimu mwaka 2012 bila kufuata taratibu za kiserikali huku mmiliki wake Dismas Mandela, amepata kuonywa na mamlaka husika mara kadhaa akitakiwa kuisajili lakini aliendelea kukaidi.

Aidha kwa upande wake Naibu Mthibiti wa Ubora wa Shule katika Wilaya ya Nyamagana, Mwalimu Winfrida Mwombeki, amesema mmiliki huyo amekuwa akikaidi maagizo ya kumzuia kuendesha shule hiyo kinyemela.

“Baada ya kugundua kwamba ameanzisha na kuendesha shule hiyo bila vibali vinavyotakiwa, mwaka 2013 tulimwita tukamuamuru aifunge na tukamuelekeza utaratibu anaopaswa kuufuata ikiwa ni pamoja na kuomba kibali serikalini, lakini hakufanya hivyo.

“Machi 20, 2016 tulifuatilia na kubaini kwamba Shule ya Elite English Medium bado ilikuwa inaendelea kutoa huduma ya elimu bila kurekebisha kasoro zilizopo, hivyo tulichukua hatua ya kumwandikia mmiliki wake barua ya maelekezo lakini alipuuza.

Mwombeki amesema Kabla ya hapo, walimuandikia barua  kwa nyakati tofauti tofauti, yaani Januari 2, 2013 na Oktoba 22, 2013 kumzuia kutoendelelea kutoa huduma ya elimu bila kibali lakini aliendelea kukaidi.

Akifafanua zaidi kuhusu uamuzi wa kuifunga shule hiyo, Mthibiti Mkuu wa Ubora wa Shule Kanda ya Ziwa, Cheyo, amesema ukaguzi ulibaini kwamba hata walimu watano waliokuwa wakifundisha shuleni hapo; kati yao, watatu hawana vyeti vya taaluma hiyo.

“Tumemuamuru mmiliki husika aifunge shule hiyo na tumemwagiza asambaze wanafunzi kwenye shule mbalimbali zinazojiendesha kisheria. Tumechukua hatua hiyo kwa kuwa huyo mmiliki inaonekana ni mjeuri,” amesisitiza Cheyo.

Kutokana na hali hiyo, Mthibiti Mkuu wa Ubora wa Shule Kanda ya Ziwa, Cheyo, ametoa wito kwa wazazi na walezi kujenga dhana ya kuhakiki uhalali wa shule kabla ya kuwapeleka watoto wao ili kuepuka matatizo yasiyo ya lazima.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.