ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, March 10, 2017

VIGOGO 11 CCM KUENGULIWA MABADILIKO YA CCM

Dar es Salaam/Dodoma. Wakati mabadiliko ya katiba yatawaengua vigogo 11 katika uongozi wa CCM walio na kofia zaidi ya moja, hatima ya idadi kama hiyo ya wanachama wanaodaiwa kukisaliti chama hicho wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, itajulikana kesho.

CCM inatarajia kupitisha mabadiliko makubwa ya katiba, ambayo yatapunguza idadi ya wajumbe katika vikao vya juu na pia kupunguza kofia za uongozi mwanachama mwenye cheo ndani ya chama, ubunge au serikalini.

Mabadiliko hayo yalipendekezwa na Halmashauri Kuu ya CCM, iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam Desemba 13 mwaka jana.

Mabadiliko hayo yalitangazwa kwenye vyombo vya habari na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM aliyemaliza muda wake, Nape Nnauye kwamba muundo wa chama umebadilika na mwanachama anatakiwa kuwa na nafasi moja tu ya uongozi wa kazi za muda wote kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni za Uchaguzi wa CCM, Toleo la 2012, Kifungu cha 22 na 23.

Nape alizitaja nafasi hizo kuwa ni mwenyekiti wa tawi, kijiji au mtaa, kata/wadi, jimbo, wilaya na mkoa. Wengine ni makatibu wa halmashauri kuu wa ngazi zote, mbunge, mwakilishi na diwani.

Mabadiliko hayo pia yamepunguza ukubwa wa Kamati Kuu kutoka wajumbe 34 hadi 24, hali inayofanya wanaoingia kwa kupigiwa kura kupungua hadi wanne kutoka kumi.

Pia nafasi za ujumbe wa Halmashauri Kuu zimepungua kutoka 388 hadi 158, huku wengi wakiingia kwa nafasi zao na wajumbe kutoka wilayani kuondolewa.

Kutokana na mabadiliko hayo, baadhi ya viongozi wenye kofia zaidi ya moja wameshaanza kutangaza kutotetea nafasi zao katika uchaguzi ujao wa viongozi wa CCM na jumuiya zake.

Wa kwanza alikuwa Sophia Simba ambaye ni mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) Sophia Simba. Simba pia mbunge na mjumbe wa Kamati Kuu.

Mwingine ni Abdallah Bulembo aliyetangaza kuwa hatagombea uenyekiti wa Umoja wa Wazazi wa CCM. Bulembo ameteuliwa na Rais Rais John Magufuli kuwa mbunge, jambo linalomfanya awe na kofia mbili.

Mbali na hao waliotangaza hadharani, wapo vigogo wengine ambao wana nafasi zaidi ya moja za uongozi, akiwamo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi ambaye mbali na uwaziri ni mbunge, mjumbe wa NEC na mjumbe wa Kamati Kuu.

Pia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ni mbunge na mjumbe wa Kamati Kuu, kama ilivyo kwa Profesa Makame Mbarawa (Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano) ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu wakati Shamsi Vuai Nahodha ni mbunge na mjumbe wa Kamati Kuu.

Mabadiliko hayo pia, yatawakumba wenyeviti wa CCM wa mikoa ambao kwa nafasi zao ni wajumbe wa NEC. Mmojawapo ni Kimbisa, ambaye ni mwenyekiti wa Mkoa wa Dodoma na mjumbe wa Kamati Kuu.

Wenyeviti wa mikoa ambao pia ni wabunge ni Joseph Msukuma (Geita), Martha Mlata (Singida) na Deo Simba (Njombe). Mwenyekiti wa CCM wa Mbeya, Godfrey Zambi pia ni mjumbe wa NEC na mkuu wa Mkoa wa Lindi.

Mwingine anaonekana kuguswa na mabadiliko hayo ni Salma Kikwete ambaye ni mjumbe wa NEC anayewakilisha Wilaya ya Lindi Mjini na ambaye hivi karibuni aliteuliwa na Rais kuwa mbunge.

Bulembo ajiuzulu

Katika hatua nyingine, jana katika kikao cha Baraza Kuu Maalum la Jumuiya ya Wazazi, Bulembo alitangaza kutotetea nafasi yake ya unyekiti.

“Kila mmoja ni shahidi, wakati naingia, jumuiya hii ilikuwa inakwenda kufa, jambo lililosababisha aliyekuwa mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete kutaka kuifuta. Lakini nikamuhakikishia ataona mapinduzi akiniachia,” alisema Bulembo.

“Sasa natoka kifua mbele, yale yote niliyoyaahidi nimetimiza kwa asilimia 75. Tangu nimeingia hatujawahi kuomba hata shilingi moja kwa ajili ya uendeshaji,” alisema.

Hata hivyo, Bulembo alisema ataendelea na vikao vyote mpaka Oktoba atakapomkabidhi rasmi mwenyekiti mpya.

Alisema kwa sasa asiulizwe kwa nini amechukua uamuzi huo na kwamba hoja siyo kuteuliwa kwake kuwa mbunge bali ni utaratibu aliojiwekea katika maisha yake.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.