ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, February 1, 2017

KWANINI KIDETE IMESHIKA MKIA?

CHANZO/GAZETI LA MWANANCHI:
Dar es Salaam. Shule ya sekondari Kidete ya Dar es Salaam, ndiyo iliyoshika mkia kitaifa katika matokeo ya mtihani kidato cha nne 2016.

Shule hiyo iliyopo umbali wa kilometa 10 kutoka daraja la Mwalimu Julius Nyerere katika Wilaya ya Kigamboni, matokeo yake yamewashangaza baadhi ya wanafunzi na walimu.

Mwandishi wetu alifika katika shule hiyo saa 9:34 alasiri, muda wa masomo ukiwa umekwisha na wanafunzi wengi walikuwa wameondoka, lakini walikuwapo wachache waliokuwa wakijisomea.

Miongoni mwa wanafunzi hao, Salma Said ambaye anasoma kidato cha nne mchepuo wa Sayansi, alisema taarifa za shule yao kuwa ya mwisho kitaifa zimewafikia, lakini bado hajaziamini.

“Hapa kuna walimu takribani 25 na wanajitahidi sana kufundisha mpaka muda wa ziada, huenda matokeo hayo yametokana na wanafunzi wenyewe, lakini si walimu. Hata mazingira ya shule ni rafiki kwa kujifunza,” alisema Salma.

Mwanafunzi mwingine, Iddy Omary wa kidato cha nne mchepuo wa Sanaa alisema Kidete haikuwahi kuwa miongoni mwa shule za mwisho, hata kama ilikuwa haifanyi vizuri si kwa kiwango hicho kilichowashtua.

“Miundombinu ya shule ni mizuri na waalimu wanajitahidi kufundisha hata wanafunzi walikuwa wanaonyesha jitihada katika masomo, licha ya kwamba baadhi yao hawakuwa na nidhamu sana,” alisema Omary.

Mwalimu mmoja ambaye alikutwa shuleni muda huo, kwa sharti la kutotajwa jina gazetini kwa kuwa si msemaji, alisema amejisikia vibaya kuona shule hiyo inakuwa ya mwisho kitaifa.

Alisema hadi muda huo alikuwa amepokea pole nyingi kutoka kwa marafiki na walimu wenzake.

“Sikuwahi ‘kufelisha’ wanafunzi, nimehamia hapa miaka ya karibuni, hata huko nilikotoka sikuwahi kupata rekodi mbovu kama hii,” alisema mwalimu huyo.

Alisema changamoto kubwa katika shule hiyo ni ufaulu mdogo wa wanafunzi wanaojiunga kidato cha kwanza na umbali wa shule kwa wanafunzi walio wengi ambao husababisha kufika kwa kuchelewa na kuwa na muda mfupi wa masomo.

“Wanafunzi wengi hapa wanatoka Yombo Buza na maeneo mengine ya Wilaya ya Temeke wakati mwingine wanafika hapa saa tatu asubuhi wakiwa wametoka nyumbani saa 10 au 11 alfajiri na inabidi waondoke saa 8:30 mchana ili wawahi kufika nyumbani,” alisema mwalimu huyo.

Alisema suala la umbali wa wanafunzi hupunguza uwezo wao wa kujisomea kwani huchoka hivyo kuishauri Serikali izingatie umbali wa wanafunzi wakati wa kuwapangia shule.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.