ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, January 10, 2017

WASTAAFU WA SERIKALI, JWTZ NA USALAMA WA TAIFA WADAI HALI NGUMU, WAITAKA SERIKALI YA MAGUFULI IBORESHE PESHENI ZAO.

Mmoja wa wastaafu akipata usaidizi kupanda chombo cha usafiri kurejea nyumbani mara baada ya kuhakiki taarifa zake katika zoezi la uhakiki wa watumshi wa Serikali wanaolipwa mishahara yao na Hazina.

Na Peter Fabian.MWANZA.

WASTAAFU wa serikali ikiwemo Taasisi na Idara za serikali wamelia hali ngumu ya maisha na kuitaka serikali ya awamu ya tano ya Rais Dk John Magufuli kuboresha na kuongeza viwango vya fedha za malipo ya pesheni zao (mafao) ikiwa ni pamoja na kuwalipa kila mwisho wa mwezi kulingana wengi wao kukabiliwa na hali ngumu ya maisha na gharama za kila siku kuwa juu ya uwezo wao.

Wakizungumza hii jana wakati wa zoezi la uhakiki wa watumishi wa serikali wanaolipwa mishahara yao na Wizara ya Fedha na Mipango (Hazina) kwenye viwanja vya Ghand jijini Mwanza wamewawataka watendaji wa Wizara hiyo kuliangalia upya suala la malipo ya pesheni zao walizokuwa wakilipwa baada ya kustaafu utumishi wa umma tangu mwaka 2000 kurudi nyuma kwa kuwa viwango vyao havikidhi hali ya sasa ambapo baadhi hula mlo mmoja wakishindwa kumudu gharama za kila siku.

Katibu wa Umoja wa Wanajeshi wastaafu Mkoa wa Mwanza (MWAWATA), Kapteni mstaafu Ndibaiyukao Mchunguzi akizungumza na GSENGO.
Katibu wa Umoja wa Wanajeshi wastaafu Mkoa wa Mwanza (MWAWATA), Kapteni mstaafu Ndibaiyukao Mchunguzi, amesema kuwa wastaafu wengi hali yao ya kimaisha inazidi kuwa mbaya kutokana na viwango vya pesheni wanazolipwa kutokidhi mahitaji ya sasa iliyopo ya maisha kuwa magumu hivyo kupelekea wastaafu hao waliolitumikia taifa kwa uaminifu kuwa ombaomba mitaani huku wengine wakishindwa hata kugharamia matibatu kutokana na kuwa wagonjwa baada ya kustaafu utumishi wa umma. BOFYA PLAY KUSIKILIZA 

“Wastaafu wanaolipwa vizuri pesheni zao ni wale waliostaafu kuanzia mwaka 2000 hadi 2016 lakini waliostaafu mwaka chini ya mwaka 2000 wana hali ngumu sana ikizingatiwa kulipwa chini ya Sh laki moja kwa mwezi hivyo lazima serikali ya awamu ya tano ya Rais Dk John Magufuli iliangalie hili kwa huruma kwani wastaafu wengi wanakabilia na ukata huku hali ya maisha inazidi kuwa ngumu ukizingatia wanasomesha watoto na baadhi ni wagonjwa wasioewza kujishughulisha tena kutokana na kukosa nguvu,”alisema.

Naye Afisa Usalama wa Taifa mstaafu, Chacha Mahende alieleza kuwa kilio kikubwa cha wastaafu ni serikali sikivu inapaswa kuliangalia suala hili la wastaafu kulipwa malipo ya pesheni yasiyo na tija kwa sasa hivyo inasababisha baadhi kushindwa kumudu gharama za maisha ikiwemo kupata matibabu ya uhakika kulingana na wagonjwa ambao wameanza kuugua baada ya kustaafu utumishi wa umma.

Ishmash Kusekwa mbele ya kamera za wandishi wa habari.
Kwa upande wake Mhasibu Mkuu wa Serikali Msaidizi, Ishmash Kusekwa, kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, alieleza kuwa zoezi hilo linahusu waliokuwa watumishi wa serikali waliostaafu kuanzia mwezi Juni 2004 tu pamoja na wastaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na maafisa wa Usalama wa Taifa na wastaafu wa serikali kuanzia mwezi Julai 2004 hao wanalipwa pesheni zao kupitia Mfuko wa Hifadhi wa PSPF.

“Tunahakiki wastaafu waliokuwa wakilipwa mishahara yao na Hazina (Wizara ya Fedha) waliostaafu Juni 2004 hatuta husika na wale waliostaafu Julai 2004 kwa kuwa hao waliishaingizwa katika utaratibu wa Mfuko wa Hifadhi wa PSPF, lakini pia tunawahakiki waliokuwa watumishi ambao ni wastaafu wa Taasisi na Idara ya Usalama wa Taifa pamoja na Wanajeshi wa JWTZ kwa kuwa hawakuwa wachangiaji wa Mifuko ya Hifadhi kwa mjibu wa taratibu za ajira zao hivyo wanahakikiwa kwa kuwa wanalipwa na Hazina,”alisema.

Aidha Mkaguzi Mkuu Msaidizi wa Ndani wa Serikali wa Bajeti na Malipo, Stanslaus Mpembe alieleza kuwa zoezi hilo litahusisha Mikoa sita ya Kanda ya Ziwa ya Geita, Simiyu, Mara, Shinyanga, Mwanza, Kagera ambapo litafanywa na watendaji wa serikali katika Ofisi za Halmashauri zote za mikoa hiyo ambapo tayari wastaafu wa Mikoa 13 ya Kanda za Mashariki, Kaskazini na Kati imeisha hakikiwa.
Mpembe amewataka wastaafu na ndugu wa wastaafu hao waliopata vibali ya Mahakama kusimamia mirathi wajitokeze wakiwa na nyaraka zao na picha tatu za paspoti na wasiokuwa na nyaraka wataelekezwa sehemu ya kuzipata na kuwahakikishia kuingia kwenye utaratibu wa malipo ya peshani zao kulingana na watakavyokuwa wamejaza fomu za uhakiki ambazo zina maelekezo na watasaidiwa na wahakiki kufanikisha zoezi hilo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.