ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, January 2, 2017

RAIS MAGUFULI AKAMILISHA ZIARA KAGERA AWATEMBELEA WAATHIRIKA WA TETEMEKO.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Charles Masinde mmoja wa wananchi walio athiriwa na tetemeko, ambapo Magufuli amemuahidi mabati 30 mwananchi huyu.
HATIMAYE Rais Dkt. John Pombe Magufuli amemaliza ziara yake ya siku mbili Mkoani Kagera kwa kuwatembelea baadhi ya wananchi walioathiriwa na tetemeko la ardhi pamoja na kukagua miundombinu iliyoathiriwa na tetemeko hilo na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa majengo ya shule ya sekondari ya Ihungo Omumwani iliyobomolewa na tetemeko la ardhi la Septemba 10, 2016.
Mara baada ya ukaguzi huo Rais Dkt Magufuli akazungumza na wananchi wa Mkoa huo wa Kagera katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Ihungo na kuagiza kuvunjwa kwa kamati ya maafa ya Mkoa huo iliyokuwa ikiratibu utoaji wa misaada na kufanya tathmini ya athari ya tetemeko hilo.

Aidha, Dkt Magufuli amewataka wote walioahidi kuchangia katika kamati ya tetemeko la ardhi ya mkoa wa Kagera ambao bado hawajatekeleza ahadi zao ambazo ni jumla ya shilingi bilioni nne nukta tano wakamilishe ahadi hizo ili ziweze kumalizia miundombinu ya Serikali iliyoathiriwa na tetemeko hilo.

Ameongeza kuwa wale wote wanaoendelea kuguswa kusaidia wapeleke michango yao moja kwa moja kwa wananchi badala ya kuipeleka serikalini kwa kuwa hakuna mchango mwingine utakaopokelewa katika Ofisi ya Waziri Mkuu.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Mbunge wa Bukoba mjini (CHADEMA) Wilfred Rwakatare mara baada ya kuwasili katika shule ya Sekondari Ihungo mkoani Kagera.

Pia Rais Dkt Magufuli ameagiza shule ya Sekondari ya Omumwani iliyokuwa inamilikiwa na Jumuia ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi CCM imilikiwe na Serikali na kutaka wanafunzi wote wanaosoma katika shule hiyo kutolipa ada kama zilivyo shule nyingine za serikali.


Dkt Magufuli ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Kagera kupunguza utitiri wa kodi katika zao la kahawa ili bei ya zao hilo ipande na kuwanufaisha wakulima.

Balozi wa Uingereza hapa Nchini Bi Sarah Cooke ambaye nchi yake imechangia kiasi cha shilingi bilioni sita kwa ajili ya ujenzi wa shule ya Sekondari ya Ihungo, amempongeza Rais Dkt Magufuli na serikali yake kwa jitihada za kupambana na rushwa suala ambalo nchi yake ya Uingereza inalipa kipaumbele sambamba na kutoa elimu bila malipo jambo linalowawezesha watoto wengi wa kitanzania kupata elimu bure

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.