ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, January 11, 2017

KAMBI YA LIPUMBA YACHUKUA RUZUKU CUF.

Kambi inayoongozwa na Profesa Ibrahim Lipumba kwenye mgogoro unaoendelea ndani ya CUF imechukua Sh369.4 milioni kutoka serikalini ikiwa ni mgawo wa ruzuku ya chama hicho.

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimedai kuibiwa fedha za ruzuku zaidi ya Sh milioni 369 huku chama hicho kikiwahusisha waliokuwa viongozi wa chama hicho, akiwemo Mwenyekiti wao, Profesa Ibrahim Lipumba na Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya.

Aidha chama hicho kimemuomba Rais John Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Ofisi ya Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na vyombo vingine vinavyohusika, kuchukua hatua za dharura za kuokoa fedha hizo.

Hata hivyo, Sakaya ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF upande wa Bara, alisema fedha hizo hazijaibiwa kama ambavyo inadaiwa, isipokuwa kwa nafasi aliyonayo ndani ya chama alimuandikia Msajili kuomba fedha hizo kwa ajili ya chama kuingia katika uchaguzi, ndipo zikaingizwa katika akaunti hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Saalam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi, Julius Mtatiro alisema CUF imeibiwa Sh 369,378,502.64 za ruzuku.

“Fedha hizo zilitoroshwa kutoka Hazina ya Serikali Januari 5 mwaka huu na kuingizwa kwenye Akaunti ya NMB tawi la Temeke yenye jina la The Civic United Front ikiwa na akaunti namba 2072300456,” alisema Mtatiro.

Alisema katika tukio hilo la wizi, Hazina imetorosha ruzuku hiyo kwa kumuamini Lipumba, Sakaya, aliyekuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF, Thomas Malima na genge lao ambao walishavuliwa uongozi na pia uanachama.

Hata hivyo, Mtatiro alisema kuwa baada ya kugundua utoroshwaji huo, CUF imejiridhisha kuwa akaunti ambayo Hazina wameshiriki kuitumia kutorosha fedha za umma na mali ya CUF ni akaunti ya CUF, ambayo hutumiwa na Wilaya ya Temeke kwa ajili ya kupokea mgawo wa ruzuku kutoka kwa Chama Taifa.

Aidha, Mtatiro alisema vikao vya kitaifa vya CUF, yaani Kamati ya Utendaji ya Taifa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, havikuwahi kupitisha maamuzi yoyote kwamba fedha za CUF ziwekwe katika akaunti hiyo ya wilaya iliyoko NMB Temeke.

Mtatiro alisema siku mbili kabla ya utoroshaji wa fedha hizo, ulisukwa mpango wa kuwaondoa baadhi ya viongozi wa CUF wa Wilaya ya Temeke kwenye utiaji saini unaoihusu akaunti tajwa; na kuwafanya watu wa Profesa Lipumba kuwa watia saini, ambao ni Sakaya na Malima.

Alisema watia saini hao wapya, waliulizia kiasi cha fedha kilichomo kwenye akaunti hiyo na walifanya hivyo katika tawi la NMB Mandela Road.

Alisema kesho yake, wakiongozwa na Malima walikwenda katika Benki ya NMB tawi la Temeke na wakatoa Sh milioni 69 na kuhamisha Sh milioni 300 kwenda kwenye akaunti ya mtu binafsi kwenye akaunti ya NMB 41401600207 ikimilikiwa na Diwani wa CUF wa Handeni mkoani Tanga.

“Mtu huyu ni wa karibu na Lipumba na ni mmoja kati ya wanachama wanane waliosimamishwa uanachama na Baraza Kuu, jana (juzi) akaunti hii ilikuwa kwenye mchakato wa kuondoa fedha hizo kutoka kwenye akaunti hiyo, na kubaki na Sh 207,907 tu,” alisema Mtatiro.

Alisema mtu huyo alitoa Sh milioni 100 kutokea Benki ya NMB tawi la Magomeni, kisha akiwa hapo Magomeni akatoa Sh milioni 50, tawi la Kariakoo alitoa Sh milioni 100 na mwisho akatoa tena Sh milioni 49.5 huku wakiwa na ulinzi wa polisi na gari ya chama hicho akiwa na Sakaya na wengine.

“Hadi tuongeavyo sasa miezi mitano CUF inadai ruzuku ya Shilingi milioni 635 na kwa kuwa fedha zilizotoroshwa Hazina zimepelekwa kwenye akaunti isiyotambuliwa Bodi ya Wadhamini ya chama inatamka kuwa hadi sasa ruzuku yake ni Shilingi 635,000,000,” alisema Mtatiro.

Ntatiro alisema Bodi ya Wadhamini ya CUF inakutana na pia Kamati ya Utendaji ya Taifa ya CUF pia kwa ajili ya kutafakari tukio hilo kubwa la chama na kuelekeza hatua za kiutawala na kisheria za kuchukua haraka.

Akizungumza na gazeti hili jana, Sakaya alisema chama kimepata nafasi ya kushiriki uchaguzi mdogo katika kata 14 kati ya 20 za Tanzania Bara, hivyo fedha zinahitajika kwaajili ya maandalizi hayo hivyo aliamua kumuandikia Msajili kuomba fedha.

“Hizo fedha hazijaibwa wala nini, hao wanaoongea hawajui wanaongea nini, mimi niliandika barua kwa nafasi yangu kulingana na uchaguzi tulionao mbele yetu nikaomba hizo fedha na zimetolewa kwaajili ya kusambazwa zinakohitajika,” alisema Sakaya ambaye alisema yuko jimboni kwake.

Sakaya alisema taarifa zilizotolewa na Mtatiro, hazina ukweli na kwamba Mtatiro hana nafasi yoyote ndani ya chama. Alisema ukweli ni kwamba Msajili kuweka fedha kwenye akaunti hiyo ya tawi la Temeke ni sahihi, kwani ana maamuzi ya kuweka popote ili mradi zinaingia katika akaunti zinazomilikiwa na chama.

Aidha alisema pia kuwa ni kweli fedha hizo zimetolewa na ni kwa ajili ya kusambazwa katika halmashauri ambazo zinahitajika kuendelea na kampeni za uchaguzi. Uchaguzi huo mdogo wa viti vya udiwani utafanyika Januari 22 mwaka huu.

Lipumba pamoja na viongozi na wanachama wengine 10 Agosti mwaka jana walisimamishwa uanachama na Baraza kuu la Uongozi la Taifa lililokutana katika kikao cha dharura huko visiwani Zanzibar hata hivyo maamuzi hayo yalitenguliwa na Msajili wa vyama vya Siasa.

Kikao hicho pia kilimteua Mtatiro kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi itakayokuwa na wajumbe wawili ambao ni Katani Ahmed Katani na Severina Mwijage, ambayo itafanya kazi za Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti hadi hapo utakapoitishwa Uchaguzi mwingine wa kujaza nafasi hizo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.