ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, December 13, 2016

SERIKALI YACHARUKA SUALA LA MAITI SABA MTO RUVU .

Dar es Salaam. 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imepokea kwa huzuni taarifa za kupatikana kwa maiti za watu saba kwenye Mto Ruvu wilayani Bagamoyo na kuahidi kufanya uchunguzi usiku na mchana kuwabaini wahusika.

Akihutubia kwenye sherehe za Maulidi zilizofanyika kitaifa Kijiji cha Shelui wilayani Iramba, Singida jana, Majaliwa alisema mauaji ya watu hao waliookotwa Desemba 8 hayakubaliki na Serikali kwa kutumia vyombo vyake vya ulinzi na usalama vinafanya upelelezi kuwatafuta waliohusika.

“Tukio hilo limetuhuzunisha sana na niwapeni taarifa kuwa upelelezi unafanywa usiku na mchana kuwatafuta waliohusika na mauaji hayo,” alisema.

Maiti hizo ziliokotwa kwenye ukingo wa mto huo zikiwa zimefungwa kwenye mifuko ya sandarusi na mawe makubwa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Bonaventure Mushongi alisema miili ya watu hao wanaokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25 na 35 iliharibika vibaya kutokana na kukaa muda mrefu kwenye maji.

Habari zaidi zinasema watu hao wanasadikiwa kuwa wahamiaji haramu.

Akizungumza kwenye kipindi cha Tuongee Asubuhi kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Star Tv, mapema jana asubuhi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchembe alisema uchunguzi wa awali unaonyesha watu hao ni wahamiaji haramu.

Waziri Mkuu pia alizungumzia suala la ugaidi ambalo dalili zake zimekuwa zikionekana kwenye matukio kadhaa katika siku za hivi karibuni nchini.

Majaliwa alisema Serikali ipo makini katika suala hilo na haitawabambikia kesi za ugaidi watu wasiokuwa na hatia.

“Ili kuimarisha nidhamu na maadili katika utumishi wa umma, mahakama zitatenda haki katika kushughulikia makosa yanayohusiana na ugaidi,” alisema na kusisitiza:

“Ni heri mahabusu 10 watoroke kuliko mtu mmoja kuingia mahabusu kwa kuonewa.”
Majaliwa aliwataka Waislamu nchini kufanya kazi ili kujiongezea kipato, akisema hata mafundisho ya dini yanasema “asiyefanya kazi na asile”.

Alisema Serikali itaendelea kulinda uhuru wa kuabudu kwa kuwaachia wananchi waamini dini wanazozipenda.

Aliwataka viongozi wa dini kuwafundisha waumini wao kuacha vitendo vya kukashifu dini za wengine kwa kuwa vinaweza kusababisha mgawanyiko katika Taifa.

“Tanzania tunakaribisha wakimbizi. Je, sisi tukifarakana kwa sababu ya tofauti ya dini zetu tutakimbilia wapi?” Alihoji.

Waziri Majaliwa alikemea uwapo wa migogoro kwenye misikiti na kutaka imalizwe kwa kufanya vikao vya ndani badala ya kufanyika hadharani.

Sheikh Mkuu wa Tanzania, Aboubakar Zuberi alisema wakati wa kumkaribisha Waziri Mkuu kuwa Waislamu wanatakiwa kujiimarisha kiuchumi kwa kuanzisha shughuli za kujiingizia kipato.

“Haiwezekani ukawa umeshika dini lakini huna biashara wala hulimi. Sasa utapataje fedha za kuendesha maisha, utakula nini kama hufanyi kazi,” alisema na kuongeza kuwa: “Waislamu tusikae ovyoovyo bila kutafuta riziki, tusile vya watu bila kufanya kazi.”

Alishauri viongozi wa misikiti kuwa wabunifu wa kutafuta vyanzo vya mapato ili kujiimarisha kiuchumi huku akisema migogoro mingi husababishwa na watu kukaa bila kufanya kazi halali.
“Waislamu tujitambue na tubadilike. Tusali lakini tukumbuke kufanya kazi za kutupatia riziki,” alisema.

Kuhusu amani, Sheikh Mkuu aliwataka Waislamu kushirikiana na watu wengine bila kujali dini zao, rangi, makabila na maeneo wanayotoka kuilinda na kuidumisha ili isitoweke nchini.

Kushika dini si udini
Kwenye sherehe hizo mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba alisema jamii inatakiwa kutofautisha kati ya dini na kumcha Mungu.

“Mtu anaposhika sana dini yake, si mdini bali ni mcha Mungu. Mdini ni mbaguzi anayedharau dini za watu wengine,” alisema Mwigulu, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani.

Alisema jamii imekuwa ikiwachukulia watu wanaoshika dini sana kama wenye siasa kali na masuala ya ugaidi, jambo ambalo alisema si la kweli.

Mwigulu alisema watu wanapokamatwa, makosa yao yasihusishwe na dini zao.
“Ukikamatwa na kosa lolote, hata kama mtuhumiwa utakuwa muumini wa dini ya Kiislamu au Kikristo, makosa yako yasihusishwe na dini yako bali mzigo huo abebeshwe mhusika mwenyewe,” alisema.

Kesi za ugaidi ziharakishwe
Katika hotuba yake kwenye sherehe hizo, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Suleiman Lolila pia alizungumzia suala la ugaidi, akitaka mahakama iharakishe kusikiliza kesi za tuhuma za makosa hayo.

Alisema kufanya hivyo kutasaidia raia wema wasio na makosa kuachiwa huru na kuendelea na shughuli zao.
CHANZO: MWANANCHI.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.