Lipumba anatarajia kuanza ziara mkoani Tanga kesho huku uongozi wa chama hicho ukisisitiza kutambua uamuzi wa Mkutano Mkuu uliomwondoa madarakani na wa Baraza Kuu kumvua uanachama.
Mwenyekiti wa CUF wa Wilaya ya Tanga, Rashid Jumbe alitoa tamko hilo jana akieleza kuwa hawatakuwa tayari kukaidi Katiba ya Chama chao na kwamba hawatampokea na hakuna maandalizi yatakayofanyika kumpokea.
"Tumeambiwa Lipumba ana dhamira ya kufanya ziara mkoani hapa. Sisi kwa uamuzi wa Baraza hatumtambui, wala hatujaandaa maandalizi ya kumpokea.
“Wilaya za Korogwe na Muheza ndizo zimesema atazitembelea, lakini sisi hatuko pamoja nao na watakaompokea wataingia kwenye mgogoro mwingine kwa sababu hatambuliki," alisema Jumbe.
Mwenyekiti huyo pia alizungumzia mgogoro baina yao na CCM kutokana na sakata la umeya ambapo alisema hatima ya mgogoro huo itajulikana baada ya mkutano mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29.
Alisema kutokana na sakata hilo walitoa malalamiko kwa viongozi mbalimbali lakini hakuna hatua zozote zinazoendelea, hivyo Kamati ya Utendaji iliwataka madiwani wa chama hicho kutohudhuria kikao chochote cha Halmashauri hadi itakapotoa uamuzi.
"Tumetoa malalamiko yetu kwa viongozi wa CCMna lengo letu ilikuwa tuonane na Rais lakini tulimpata Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa aliyetwambia kuwa atalifanyia kazi, lakini sasa tumeamua kupeleka malalamiko yetu kwa wenye chama na wao ndio watakaotoa uamuzi juu ya mgogoro huo.
“Hivyo tumeitisha mkutano ambao utakuwa na wajumbe 440 ambapo tuna imani kuwa tatizo letu litakwisha Oktoba 29,” alisema Jumbe.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.