Suleiman Matola (kulia) ameachia ngazi Simba SC baada ya kutofautiana na bosi wake, Dylan Kerr (kushoto) |
KOCHA Msaidizi wa Simba SC, Suleiman Abdallah Matola amejiuzulu nafasi hiyo kutokana na kile alichodai kutolelewana na Kocha Mkuu, Muingereza, Dylan Kerr.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE usiku huu, Matola amesema kwamba amefikia uamuzi huo baada ya kuona maelewano na bosi wake huyo yanazidi kuwa magumu kila kukicha.
“Ni jambo la muda mrefu, huyu kocha hasikilizi ushauri wangu, imefikia sasa ananichukia na kazi haziendi tena. Sasa nimeona ili kuepusha matatizo zaidi, nimuachie yeye timu,”amesema Matola.
Matola amesema kwamba haoni mwelekeo wowote mzuri kwa Simba SC chini ya kocha huyu Muingereza ambaye hasikilizi ushauri, ndiyo maana ameamua kujitoa.
“Nimekutana na uongozi, nimewaambia juu ya uamuzi wangu, wakanisihi sana nisifanye hivyo, lakini nikashikilia msimamo wangu. Wakaniambia hata nirudi kufanya kazi timu za vijana, lakini nikawaambia nitajifikiria kwanza,”amesema Matola.
Juhudi za kumpata Kerr kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa na hakuna kiongozi wa Simba SC aliyepatikana mapema jioni hii kuelezea sakata hilo.
Historia ya Matola ndani ya Simba SC inaanzia mwaka 2000 alipojiunga nayo kama mchezaji akitokea Kagera Stars (sasa Kagera Sugar) na aliichezea timu hiyo hadi mwaka 2005 alipohamia Super Sport United ya Afrika Kusini.
Matola alirejea Simba SC mwaka 2007 na kucheza kwa msimu mmoja kabla ya kustaafu moja kwa moja.
Kuanzia mwaka 2010 amekuwa kocha wa timu za vijana za Simba SC ambako baada ya kufanya vizuri akapandishwa kuwa Kocha Msaidizi, akianza kufanya kazi na Mcroatia Zdravko Logarusic, baadaye Mzambia, Patrick Phiri, Mserbia, Goran Koponovic na huyu wa sasa Kerr.
Haijawahi kutokea Matola akatofautiana na kocha yeyote kati aliyofanya nao kazi awali – na Muingereza huyu anakuwa wa kwanza kutofautiana na Nahodha wa zamani wa Simba SC.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.