Baadhi ya wanafunzi walioshiriki kwenye mdahalo |
Frank Timothy Malata, mgombea Ubunge Jimbo la Mufindi Kusini. Kwa tikeki ya Chadema akitoa maelezo.
|
Mwanafunzi Mangula akiuliza swali juu ya huduma bora ya Umeme |
Zikiwa zimebaki siku 23 kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, hapo jana wakazi wa Jimbo la Mufindi kusini wamewataka wagombea Ubunge na Madiwani watakaopata nafasi ya kuwaongoza katika kipindi kinachofuata kutafuta suluhisho la ukatili dhidi ya watoto ikiwa ni pamoja na adhabu kupita kiasi kutoka kwa walimu na wazazi, Mimba za utotoni na kukatishwa masomo kwa watoto kwa ajili ya ndoa ama ajira.
Hayo yalisemwa katika mdahalo uliofanyika katika Shule ya Msingi Igowole wilayani Mufindi, ambao ulishirikisha wanafunzi kutoka Shule za Msingi Igowole, Ibatu na Kisalasi, pamoja na walimu, wazazi na walezi ambao waliwahoji wagombea wa Ubunge Frank Timothy Malata (CHADEMA) pamoja na wagombea udiwani Castory Boniface Masangula (CCM) na Israel Mpina Msalilwa (CCM).
Aidha walisisitiza suala la upatikanaji wa viwanja vya michezo kwa watoto na kudai kuwa michezo ni njia mojawapo ya kumbadili mtoto kimwili na kiakili.
Akijibu hoja kutoka kwa wananchi, Mgombea Ubunge katika Jimbo hilo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Frank Timothy Malata ameahidi kupatikana suluhisho la adha hizo na kukomesha ukatili dhidi ya watoto. Mgombea huyo pia ameahidi kuinua michezo kwa kuanza na upatikanaji wa viwanja bora vya michezo mbalimbali zaidi ya mpira wa miguu.
Kwa upande wake Mgombea Udiwani Kata ya Igowole kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM Castory Boniface Masangula ameahidi kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa kamati za ulinzi za watoto na sekta nyingine zinazojihusisha na ulinzi wa mtoto ili kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya ukatili wowote.
Naye Israel Mpina Msalilwa ambae ni mgombea Udiwani wa kata hiyo kupitia CHADEMA aliahidi kushirikiana na serikali pamoja na wadau mbalimbali kuondoa tatizo la mrundikano wa wanafunzi madarasani pamoja na kupiga vita ukatili dhidi ya watoto zikiwemo adhabu kupita kiasi zinazotolewa na wazazi, walezi ama walimu.
Katika hatua nyingine, watoto ambao ndio walengwa wakuu wa Midahalo hii walitoa maoni yao kuwa nini kifanyike baada ya viongozi hao kushika nyadhifa wanazogombea ambapo walitaja kuwa wanakerwa na uhaba wa vitabu, vyoo, huduma bora za afya, umeme na usafiri na kupambana na mimba za utotoni hasa hasa kwa wanafunzi.
Wakati huo huo, Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Mufindi Navoneiwa Mfinanga amewataka wagombea hao kuwa karibu na kamati za watoto ili kuhakikisha wagombea wanatimiza ahadi zao
Midahalo hii ni muendelezo wa midahalo ya kipindi cha redio cha Walinde Watoto kinachoandaliwa na Kampuni ya TRUE VISION Production chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ikishirikiana na UNICEF yenye lengo la kuibua ajenda ya watoto kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015.
Unaweza kusikiliza kipindi cha Walinde Watoto mahali popote kupitia redio shiriki 19 ikiwemo TBC inayorusha matangazo hayo siku ya Jumamosi kuanzia saa tisa mchana na pia kupitia tovuti ya www.walindewatoto.org nawww.facebook.com/WalindeWatoto
“Tuwape nafasi viongozi wanaojali watoto kwa kutetea haki zao” – Baraza la Watoto
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.