Na Emmanuel Mlelekwa
KAHAMA
Baraza la hifadhi ya mazingira la Taifa NEMC limethibitisha kuwa mgodi wa uchimbaji madini wa ACACIA Bulyanhulu ulioko wilayani Kahama Mkoani Shinyanga umebainika kuwa na kosa la kushindwa kuzuia Sumu inayotumika kusafishia Dhahabu na kupelekea athari katika jamii inayozunguka mgodi pamoja na viumbe hai.
Akitoa ripoti ya uchunguzi wa kimaabara ya NEMC kwa vyombo vya habari mkuu wa wilaya ya Kahama Benson Mpesya amesema kuwa mgodi wa Bulyanhulu ACACIA haukuwa makini katika kuhifadhi sumu hiyo hali ambayo ilipelekea wakazi 130 kupata madhara ya kiafya pamoja na viumbe hai wanaoishi majini.
Amesema kuwa mnamo January 8 Mwaka huu sumu hiyo aina ya Cynide ilisambaa kwenye mashamba ya wakulima kufuatia mvua kubwa iliyonyesha siku hiyo iliyobomoa ukingo wa ukuta unaohifadhi maji yenye sumu hiyo na kuepelekea kiwango kikubwa cha sumu kusambaa kwenye maeneo ya mashamba ya wakulima.
Ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo serikali kupitia ripoti ya NEMC imeutaka mgodi huo kuwalipa fidia wananchi wa kijiji cha Kakola namba 9 ambao waliathiriwa na sumu hiyo ambao baada ya tukio hilo kutokea walitakiwa kutotumia maeneo yao ikiwemo kilimo kwa kwa kipindi cha mwaka mzima na kupelekea kukabiliwa na tatizo la njaa.
Hata hivyo mkuu wa wilaya amesema kuwa ni lazima wakazi wa eneo hilo walipwe fidia ili waweze kununua chakula kwani serikali ilikuwa bado inasubiria ripoti ya NEMC ambayo imetolewa na kwa mujibu wa sheria ya uhifadhi na udhibiti wa mazingira mgodi inatakiwa ufanye hivyo.
Kauli hiyo imekuja kufuatia wakazi wa kijiji cha Kakola Namba 9 kulalamika mbele ya waandishi wahabari kuwa mgodi wa Bulyanhulu wameshindwa kuwalipa fidia kutokana na uharibifu uliotokana na sumu hiyo jambo ambalo limechangia wakazi wa eneo hilo kukabiliwa na uhaba wa chakula na madhara mbalimbali kiafya.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.