WATENDAJI wa kata na mitaa wilayani Kahama mkoani Shinyanga wametakiwa kusimamia vyema majukumu katika nafasi za uongozi wanazozitumikia ikiwa ni pamoja na kutetea haki za watoto ili kutokomeza matukio ya unyanyasaji kwa watoto yanayosababisha kukosa haki zao.
Wito huo umetolewa leo na mwezeshaji wa mafunzo kwa jamii juu ya kupunguza ajira mbaya kwa watoto Fanuel Ruben ambayo yametolewa kwa watendaji wa kata za Mhongolo, Mwendakulima na Zongomela.
Ruben amesema matukio ya unyanyasaji kwa watoto yaliyopo katika jamii viongozi hao wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kuyafuatilia na kushiriki kuyatokomeza ikiwa ni pamoja na kutoa elimu mara kwa mara kwa wananchi watambue umuhimu wa haki ya mtoto.
Aidha amewataka watendaji hao kutopindisha sheria katika kusimamia upatikanaji wa haki ya mtoto ikiwemo rushwa bali wafikishe kesi zinazohusu unyanyasaji wa watoto katika ngazi za juu ikiwemo ofisi za maendeleo ya jamii ili haki ya mtoto ipatikane.
Naye mwenyekiti wa asasi ya kiraia ya KACODA ambao wameratibu mafunzo hayo Clement Masonga amesema mafunzo hayo watendaji wayachukulie kuwa chachu ya kukomesha utumikishwaji wa watoto katika jamii ikiwemo majumbani,migodini na viwandani na maeneo mengine.
Nao watendaji hao wamesema wataenda kufikisha kile walichojifunza juu ya haki za mtoto licha ya changamoto iliyopo katika jamii kutokutoa ushirikiano pale wanapoona vitendo vya unyanyasaji kwa watoto.
Mafunzo hayo ni ya siku mbili ambayo yalianza Julai 2 na kumalizika leo katika ukumbi wa DVTC yakiratibiwa na asasi ya kiraia ya Kahama Community Development Association.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.