ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, July 15, 2015

MUDA WA PEPSI KOMBE LA MEYA 2015 JIJI LA MWANZA UMEWADIA.

75
Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza Stanslaus Mabula (kushoto ndani ya bajaji) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa SBC Mwanza Nicolaus Coetz ambao ni watengenezaji wa vinywaji jamii ya PEPSI wakiwa wameshika kadi na funguo za zawadi ya bingwa wa PEPSI KOMBE LA MEYA 2015 ambayo ni Bajaji ya abilia, Kombe, Fedha taslim shilingi milioni 2 na Medali ya dhahabu. Wengine katika picha ni Mkurugenzi wa My Way Entertainment Paul Mganga (kushoto) na Meneja masoko wa SBC Promod Nair. (aliyeketi kwenye pikipiki) 
Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza Stanslaus Mabula (katikati) akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa SBC Mwanza Nicolaus Coetz (kulia) wakikabidhi vifaa kwa kiongozi wa timu Mabingwa wa 2014 - 2015 Mkolani Fc ambao watakwenda kufungua mashindano mnamo tarehe 19 wakipepetana na Mirongo Fc.
Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza Stanslaus Mabula akizungumza na wadau wa michezo (wanaonekana katika picha za chini kabisa)  BOFYA PLAY KUSIKILIZA TAARIFA YA SPORTS RIPOTI YA JEMBE FM.

Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza Stanslaus Mabula akizungumza na wadau wa michezo, mbele yake ni baadhi ya vifaa vya michezo kwa michuano hiyo ambapo huboreshwa kila mwaka.
Kutoka kushoto ni Kombe kwa bingwa, likifuatiwa na kombe kwa nafasi ya pili, nafasi ya tatu, timu yenye nidhamu na kiatu kwa mfungaji bora wa michuano ya PEPSI KOMBE LA MEYA 2015
Kwa kutambua mchango na juhudi binafsi za mwasisi wa PEPSI KOMBE LA MEYA katika kuhimiza jamii kutunza mazingira ya bonde la ziwa Victoria wadau wa mazingira kutoka LAVLAC walimkabidhi Mstahiki Meya wa jiji la Mwanza Stanslaus Mabula cheti cha utambuzi.
Hiki ndicho kiatu cha dhahabu kwa mfungaji bora wa Michuano.
Kila timu itakabidhiwa full jezi na mipira miwili.
Zawadi kwa pamoja.
Full set kwa wahusika wote dimbani.
Afisa mauzo wa SBC Hussein Mkwawa akizungumzia **Kwanini PEPSI wanadhamini mashindano hayo**
Viongozi mbalimbali wa timu shiriki PEPSI KOMBE LA MEYA 2015.
Baadhi ya waandishi wa habari waliojitokeza kwenye kusanyiko hilo la utambulisho wa ratiba na vihusishi vya PEPSI KOMBE LA MEYA 2015.
Viongozi mbalimbali wa timu shiriki PEPSI KOMBE LA MEYA 2015.

75PEPSI KOMBE LA MEYA 2015
KANUNI ZA MASHINDANO
1.   Mashindano yatajulikana kama mashindano ya KOMBE LA MEYA 2015.
2.   Lengo la mashindano ni kuwezesha vikundi vya ujasiriamali, kuleta umoja, hamasa, mshikamano na burudani.
3.   Mashindano yatafanyika kuanzia tarehe 19/07/2015 hadi tarehe 12/09/2015.
4.   Mashindano yatahusisha jumla ya timu 24. Timu 18 kutoka katika kata za Wilaya ya Nyamagana ambazo ni kata za Nyegezi, Lwanhima, Luchelele, Mabatini, Mhandu, Kishiri, Mkolani, Buhongwa, Mkuyuni, Igogo, Nyamagana, Isamilo, Mirongo, Mahina, Igoma, Mbugani, Pamba, Butimba pamoja  na timu maalum za wadau kama Bodaboda, Nyegezi Stand, Mafundi Viatu, Magazeti, Machinga, Sokoni, Mwanza Jiji, Mafundi Gereji, Wanahabari, Daladala, Mnadani na Polisi Jamii kwa mchezo wa Soka.
5.   Mashindano yataendeshwa kwa awamu mbili:
(a)  Awamu ya kwanza itazikutanisha timu 14 zitakazocheza kwa mtindo wa mtoano. Timu hizo ni:-
Timu saba zilizoshika nafasi za mwisho katika msimu uliopita, timu ya  Mafundi Viatu pamoja na timu sita za Kata Mpya.
(b)  Awamu ya pili itakuwa ligi katika makundi na baadae mtoano kuanzia hatua ya robo fainali.
6.   Timu zitapangwa katika makundi manne na kila kundi litatoa washindi wawili watakaoingia robo fainali.
7.   Timu itaruhusiwa kusajili wachezaji wasiozidi 25 kwa fomu iliyotolewa. Wachezaji wa Ligi Kuu ya Vodacom na Ligi Daraja la Kwanza hawaruhusiwi katika mashindano haya.
8.   Timu itakayomchezesha mchezaji ambaye hayupo kwenye orodha ya wachezaji waliosajiliwa itapoteza michezo yote ambayo mchezaji huyo aliichezea.
9.   Wachezaji waliocheza mechi za awali za mchujo watakuwa huru kusajili katika timu yoyote mara baada ya mechi hizo kumalizika.
10.  Iwapo mchezaji atagundulika kuwa amesajiliwa katika timu zaidi ya moja, ataondolewa kwenye mashindano na timu hiyo haitaruhusiwa kuweka mchezaji mwingine mbadala. Kama ikibainika hivyo mchezoni timu hiyo itanyang’anywa ushindi kwa mechi hiyo na nyingine zote alizokwishacheza.
11.  Sheria zote 17 za soka zitafuatwa.
12.  Kubadili wachezaji (substitution) mwisho ni wachezaji watano.
13.  Mchezaji akipewa kadi nyekundu hatoruhusiwa kucheza mechi moja inayofuata. Pia mchezaji akipata kadi mbili za njano katika mechi tofauti hatoruhusiwa kucheza mechi moja inayofuata.
14.  Mashindano yanasimamiwa na Kamati ya Mashindano.
15.  Kamati ya mashindano inayo mamlaka ya kuifuta katika mashindano timu yoyote ambayo wachezaji na washabiki wake watakua ni chanzo cha vurugu katika mashindano.
16.  Kila timu ina wajibu wa kulinda na kutunza nidhamu ya wachezaji na washabiki wake ndani na nje ya mchezo.
17.  Maamuzi ya refa yatakuwa ya mwisho katika mchezo.
18.  Ni kapteni wa timu pekee ndiye anaruhusiwa kupeleka malalamiko kwa muamuzi wakati wa  mchezo.
19.  Timu itakayogomea mchezo itakuwa imepoteza mchezo husika na Kamati ya mashindano itakaa kuijadili timu hiyo kwa adhabu nyingine kama itaona inafaa.
20.  Mchezo utaanza saa 10:00 jioni. Kila timu inatakiwa kufika uwanjani saa moja kabla ya muda wa kuanza mchezo.
21.  Viongozi wa timu watatakiwa kusaini kwenye nakala ya kanuni itakayobaki kwa muandaaji wa mashindano ikiwa ni ishara ya kuwa wamezielewa na wataziwasilisha vyema kwenye timu zao ili kuboresha mchezo.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.