ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, July 29, 2015

USHINDI WATAWALA UFUNGUZI WA AIRTEL RISING STARS

Wachezaji wa Shein Rangers na Mchanganyiko Fc wakichuana vikali katika mchezo wa ufunguzi wa Airtel Rising Stars kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam juzi (Jumatatu Julai 27). MCHANGANYIKO FC ilishinda kwa 1-0. Ushindi watawala ufunguzi wa Airtel Rising Stars 
TIMU ya mkoa wa kisoka wa Ilala ya Bombom juzi (Jumatatu, Julai 27) imeanza vema mashindano ya soka kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising stars baada ya kuiadhibu bila huruma Ilala Academy 4-1 katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Kumbumumbu ya Karume jijini Dar es Salaam. 

Mchezo huo wa ufunguzi uliokuwa na hamasa ya aina yake ulikuwa ni moja ya michezo mitatu iliyochezwa kwenye uwanja huo wa kihistoria. Bombom ilionesha mchezo safi huku wachezaji wake wakiwa wanacheza kwa kujiamini na kuonesha vipaji vyao mbele ya mashabiki wengi wao wakiwa ni vijana. 

Mchezo wa pili ambao pia ulivuta hisia za watazamaji wengi ulizikutanisha timu za Wakati Ujao na Makangalawe ambapo timu ya Wakati Ujao ilifanikiwa kuibuka na ushindi mwembamba wa 1-0. 

Wakati Ujao walianza mchezo huo kwa kasi na kuleta kizaazaa langoni mwa wapinzani wao na juhudi zao ziliza matunda katika dakika ya saba wakati mshambuliaji hatari Yahaya Bunga alipowatoka mabeki wa timu ya Makangalawe na kuachia shuti kali liliotinga wavuni huku mlinda mlango akichupa bila mafanikio. 

Mchezo wa tatu ulizikutanisha timu Shein Rangers na Mchanganyiko Fc ambapo Mchanganyiko walifanikiwa kuchomoza na ushindi wa 1-0. Machanganyiko FC walimudu kutawala mchezo huku wakikosa mabao kadhaa katika kipindi cha kwanza. 

Baada ya timu hizo kurejea katika kipindi cha pili, Mchanganyiko waliendeleza mashambulizi ya kasi na hatimaye kuweza kupata goli la ushindi mnamo dakika ya 56 kupitia kwa mchezaji wao Mwaki Salum. Mchezaji huyo mwenye umbo dogo alipata mpira akiwa nje kidogo ya 18 ambapo alichia shuti kali na kuiandikia bao la ushindi kwa timu yake.

Mashindano ya Airtel Rising Stars mwaka huu yanajumuisha mikoa ya Ilala, Temeke, Kinondoni, Morogoro, Mbeya, Mwanza na Arusha ambapo fainali za taifa za michezo hiyo zimepagwa kupigwa jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 11 hadi 21.

Huu ni mwaka wa tano kwa kampuni ya simu za mkononi ya Airtel kuanzisha na kudhamini michuano hiyo ya Airtel Rising Stars yenye lengo la kutafuta na kuendeleza vipaji.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.