Mwandishi wa habari mkongwe nchini marehemu, Betty Luzuka. |
Na,Mwandishi wetu,Arusha
Mahakama ya mwanzo ya Maromboso imetupilia mbali kesi ya pingamizi iliyofunguliwa na mke wa aliyekuwa ofisa mwandamizi wa jumuiya ya Afrika Mashariki,Phil Kleruu aitwaye Hilda Kleruu kwa madai kwamba siyo mwaminifu na hivyo amekosa sifa ya kuwa msimamizi wa mirathi ya mwandishi wa habari mkongwe nchini marehemu ,Betty Luzuka.
Kesi hiyo ya mirathi iliyovuta hisia za watu mbalimbali jijini Arusha ilifunguliwa katika mahakama ya mwanzo ya Maromboso yenye nambari 222 ya mwaka 2013 iliitaka mahakama hiyo ipitie hukumu yake iliyotolewa Septemba 27 mwaka 2013 na hakimu Prince Gideon iliyompa ushindi kaka wa marehemu,Ssarongo Luzuka.
Hilda, alifunguliwa kesi na kaka wa marehemu, Ssarongo Luzuka akimtuhumu kujimilikisha mali za marehemu bila kufuata utaratibu wa kifamilia na kimahakama mara baada ya marehemu kuaga dunia Agosti mwaka 2013 katika hospitali ya Shreee Hindu ya jijini Arusha baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Akitoa hukumu ya pingamizi mbele ya mahakama juzi hakimu aliyekuwa akisiliza pingamizi hiyo,Moka Mashaga alisema kuwa kitendo cha mdaiwa kuchukua fedha kwenye akiba ya marehemu kabla na baada ya kifo chake kimethibitisha kwamba hakuwa mwaminifu kuwa msimamizi wa mirathi.
Katika hukumu ya kesi hiyo iliyosomwa kwa muda wa saa 1;30 mahakama hapo hakimu huyo alisema kwamba mpingaji (Hilda) amepoteza sifa ya kuwa msimamizi wa mirathi kwa kuwa alitaka kuuza mali za marehemu kabla hata shauri lililo wasilishwa mahakamani hapo kusikilizwa.
“Ushahidi wa mdaiwa ni hafifu na umetupwa ,mahakama inakubaliana na ushahidi wa wadai kwani umeonyesha walikuwa karibu na marehemu na alipougua waliweza kutuma fedha za matibabu na hata kumhudumia”alisema Hakimu Moka
Hatahivyo,Hakimu huyo alienda mbali zaidi na kusema kuwa wosia uliowasilishwa na upande wa mdaiwa una dosari kwa kuwa haukuwa na mhuri na kuongeza kwamba kitendo cha wakili wa upande wa mdaiwa,Wilferd Mirambo kutofika mahakamani hapo kuthibitisha wosia huo kimethibitisha wosia huo una dosari na wakili huyo hakutaka kujiingiza katika makosa.
“Mahakama inaheshimu wosia lakini uwe umefuata sheria wakili Mirambo pamoja na kuitwa mahakamani lakini hakuweza kufika kuthibitisha wosia huo,mahakama inathibitisha kwamba kitendo cha kutofika mahakamani kinathibitisha kwamba hakutaka kujiingiza kwenye makosa”alisisitiza Hakimu huyo
Akimalizia kusoma hukumu hiyo hakimu Moka alisema kwamba kaka wa marehemu Sarongo Luzuka pamoja na dada wa marehemu Jullie Luzuka wataendelea kuwa wasimamizi wa mirathi ya marehemu kwa kufuata sheria za mirathi na baada ya siku 30 watapaswa kuleta orodha ya mali za marehemu mahakamani hapo ili ziweze kugawanywa kwa mujibu wa sheria.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.