NA PETER FABIAN, MWANZA.
KATIBU wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Mwanza , Miraji Mtaturu, amewataka wananchi wa Jimbo la Nyamagana kumuhoji Mbunge wao, Ezekiel Wenje, fedha za mfuko wa Jimbo hilo zaidi ya milioni 156 kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita zilifanya kazi gani?.
Maturu alisema hayo juzi kwa nyakati tofauti wakati akihutubia wakazi wa Bugarika Kata ya Pamba na wakati wa uzinduzi shina la vijana waendesha Pikipiki wakareketwa wa CCM (Reli), mtaa wa Nyamagana Magharibi jijini hapa.
Katibu huyo alidai kuwa, fedha hizo hutolewa na serikali ya CCM kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya jimbo hilo lakini Mwenyekiti wa mfuko ambaye ni Wenje, amekuwa akizitumia kwa kazi tofauti na malengo yake na kuzigawa kwa ubaguzi akipendelea madiwani wa Chama chake cha CHADEMA.
“Umefika wakati wananchi mumuhoji Wenje, na awape majibu ya kueleweka siyo anakuja na kuwapa vijana viroba vya pombe halafu anatukana viongozi wa serikali na CCM na kusepa baada ya mkutano.” Alisema Mtaturu na kudai kuwa toka mwaka 2011 hadi 2013 fedha hizo hazieleweki zimefanya shughuli gani.
Alifafanua kwamba, kazi ya mfuko huo ni kuchochea maendeleo kwenye jimbo hili lakini kwa kipindi hicho hazijafanya kazi iliyokusudiwa tofauti na mwaka 2014/2015 mfuko huo uliopeleka mifuko 80 saruji kwenye shule kadhaa za Msingi, baada ya Madiwani wa CCM kuingia kwenye Kamati hiyo.
Alisema, Wenje amekuwa akijinadi kwenye mikutano ya hadhara kuwa amefanya kazi na kuwaletea maendeleo wananchi wa Nyamagana lakini kazi hizo haziuonekani machoni mwao, hivyo wananchi wakati ukifika wa kutafuta mwakilishi mwingine, ni vyema wakamtosa na kuchagua mtu sahihi kutoka CCM badala ya kupeleka Mbunge na mtalii kama yeye.
Akizindua tawi la vijana hao, Mtaturu aliwataka vijana wengine waige mfano wa waendesha bodaboda hao kwa kujiunga kwenye vikundi ili Chama na serikali viwawezeshe, pia aliwataka wananchi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili wapate fursa ya kuchagua viongozi bora ambao anaamini watatoka CCM.
Akiwa Bugarika, Mtaturu alimuagiza Mtendaji wa Kata ya Pamba bw Charles Musso aondoe dampo la taka lililorundikana katika makazi ya wananchi wa Bugarika kwani linaweza kusababisha mripuko wa magonjwa kwa wananchi na kumtaka Diwani wa Kata hiyo Samuel Range aanze kuaga kwani ameshindwa kuwaletea maendeleo wana Bugarika badala yake amewarundikia rundo la uchafu huo.
Alitoa siku nnne taka hizo ziwe zimeisha ondolewa vinginevyo atamuagiza Meya wa jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula (CCM), Mtendaji huyo aondolewe na kupelekwa mwingine atakayeweza kuwatumikia wananchi ikiwemo kusimaia shughuli za maendeleo na usafi wa mazingira kikamilifu.
Mbunge Wenje alipotafutwa na MTANZANIA kwa njia ya simu jana, alidai kwamba CCM haiwezi kumsema vizuri bila kufafanua zaidi kwa madai kuwa ana shughuli za chama chake ikiwa pamoja na kuwa kwenye Kikao cha Kamati Kuu jijini Dar es salaam na hawezi kujibishana na wapinzani wake kwenye majukwaa kwa sasa.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.