NA PETER FABIAN, MWANZA.
KAIMU Mganga Mkuu (RMO) wa Mkoa wa Mwanza, James Kengia, amelitaka Shirika la ICAP Tanzania nchini linaloshughulikia makundi maalumu ya vijana kutekeleza kwa vitendo mkakati wake wa kudhibiti maambukizi mapya ya ugonjwa wa ukimwi ikiwemo vijana wanaojidunga na kutumia dawa za kulevya katika Wilaya za Ilemela na Nyamagana jijini Mwanza.
Akizungumza katika ufunguzi wa Warsha ya siku moja iliyoshirikisha wadau kutoka baadhi ya Taasisi za seikali na makudi ya vijana na kijamii ambayo hushughulikia makundi maalumu iliyofanyika katika ukumbi wa Gold Crest juzi jijini hapa, Kengia alisema ni vyema ICAP Tanzania wakajipanga vyema kudhibiti maambukizi mapya ya Ukimwi na vijana kutumia dawa za kulevya.
Kengia ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema kwamba endapo ICAP ikatumia fursa hiyo na kujikita kikamilifu kuokoa kundi maalum la vijana wanaojitumbukiza katika vikundi hatarishi vinavyoweza kuongeza kasi ya maambukizi ya Ukimwi na wanaojidunga na kutumia dawa za kulevya.
“Nilipongeze shirika hili kwa kuona umuhimu wa kuja na mkakati wa kuokoa kundi hili la vijana wa kiume na kike lililo katika mazingira hatarishi zaidi kwa jamii ambalo limekuwa likikumbwa na maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi na kasi ya utumiaji wa dawa za kulevya kutokana pia na kufanya mapenzi ya jinsia moja kinume na maumbile na wanaojiuza na kufanya ngono nzembe,”alisema.
Kwa upande wake Afisa wa Utafiti na Mtaalamu mshauri wa Afya wa ICAP Tanzania, Haruka Maruyama, alisema kwamba warsha hiyo, iliyohusisha wadau mbalimbali wa makundi ya kijamii, baadhi taasisi za umma zinazojihusisha kwa karibu katika utoaji huduma za kijamii na kuyahudumia makundi hayo ili kujaribu kushirikiana kuwaokoa na kudhibiti ongezeko la waathirika.
“Tumejikita katika mradi huu, kwanza Wilaya za Ilemela na Nyamagana katika Mkoa wa Mwanza, lakini pia tutaendelea kuzifikia wilaya zingine hasa zilizo na visiwa ndani ya Ziwa Victoria ambavyo kumekuwa na kasi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi kutokana na makundi ya vijana ikiwemo watumiaji wa dawa za kulevya,”alisema.
Naye Meneja Mradi wa ICAP Tanzania Mkoa wa Mwanza, Aziz Itaki aliwaeleza washiriki kuwa Shirika hilo limejikita kuokoa makundi maalumu ya vijana wanaojidunga na kutumia dawa za kulevya, wanawake wanaofanya biashara za ngono kwa kuuza miili yao na wanaofanya mapenzi ya jinsia moja (Kiume) katika Wilaya za Ilemela na Nyamagana jijini Mwanza.
Itaki alisema kuwa kutokana utafiti walioufanya na shirika hilo mwaka 2014 na kuonyesha kuwepo makundi ya vijana ya kijamii kwenye wilaya hizo yanayojihusisha moja kwa moja na kujidunga na utumiaji dawa za kulevya, kufanya mapenzi ya jinsia moja na wanawake wanaojiuza kwa kufanya ngono kwa ajili ya kujipatia kipato, pia kuanza kufanya utafiti wa ugonjwa wa homa ya ini kwa makundi hayo.
Mratibu wa ICAP Mkoa wa Mwanza, Gerald Nyigu, akitoa takwimu za shirika hilo kwa kipindi cha kuanzia Januari 2014 hadi Marchi 2015 mwaka huu, alisema kuwa ICAP imefanikiwa kuwa kwafikia vijana 1093 kutoka katika makundi hayo matatu ikilinganishwa na vijana 273 (2013) wa awali, ambapo vijana wanaojidunga na kutumia dawa za kulevya ni 509 wanawake wakiwa 52.
Nyigu alisema kuwa vijana wa kike na wanawake wanaojiuza waliofikiwa ni 446 na wanaofanya mapenzi ya jinsia moja waliofikiwa ni 86 huku waliobainika na kukutwa na virusi vya Ukimwi (HIV) baada ya kuwafanyia vipimo ikiwa ni 1030 katika makundi yote matatu katika Wilaya zote mbili na kushauriwa kuanza utumiaji wa dawa za kufubaza katika vituo vya Afya na Hospitali ya Rufaa yaw a Mwanza ya Mkoa Sekou Toure na Rufaa ya Bugando (BMC) jijini hapa.
“Takwimu zinaonyesha kuwa baada ya upimaji huo waliokutwa wameathirika ni 191 katika makundi matatu, wameshauriwa na kuanzishiwa dawa, lakini shirika linaendelea kuwajengea uwezo wahudumu wa makundi hayo pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa waliokubali kufikiwa ili kusaidia kuwafikia wengine zaidi,”alisisitiza.
Mratibu huyo alitoa wito kwa Jeshi la Polisi katika Wilaya za Ilemela na Nyamagana kushirikiana na ICAP ili kuwafikia vijana walio katika makundi hayo badala ya kuwavizia na kuwakamata jambo ambalo limekuwa ni changamoto kubwa kwa shirika na wataalamu wake kutoa elimu, kuwafikia kirahisi na kuwafanyia vipimo na kutoa ushauri kwa lengo la kupunguza kasi ya maambukizi mapya ya Ukimwi kupitia makundi hayo.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.