HOSPITALI ya Mkoa wa Mwanza ambayo ni ya Rufaa ya Sekou Toure liyopo jijini hapa, inakabiliwa na upungufu wa dawa kutokana na ongezeko kubwa la wagonjwa wa rufaa na wakawaida wanaopata huduma moja kwa moja katika hospitali hiyo.
Hayo yamesemwa na Katibu Hoispitali hiyo, Daniel Temba wakati akitoa taarifa fupi kwa Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Miraji Mtaturu, alipotembelea ghafla Hospitalini hapo kujionea changamoto zilizopo na utolewaji huduma ya Afya kwa wananchi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kama inavyoelekeza.
Temba alisema kuwa kutokana na ongezeko hilo ni moja ya changamoto kubwa linaloikabili Hospitali hiyo licha ya kuwa na upungufu wa asilimia 39 ya watumishi na madaktari wakutoa huduma kwa wananchi katika vitengo mbalimbali.
Katibu huyo alisema kuwa “Serikali imefanya juhudi kubwa kuwekeza katika sekta ya afya na kuboresha miundombinu ya utoaji huduma ya Afya ikiwemo ya Hospitali hii lakini tunakabiliwa na upungufu wa upatikanaji wa dawa kutokana na ongezeko kubwa la wagonjwa,” Temba alifafanua kuwa, kila siku Hospitali hiyo hupokea wagonjwa wa rufaa na wanaotibiwa kawaida wapatao 447 wakiwemo akina mama 35 wanaojifungua kwa siku hivyo dawa wanazopata haziendani na ongezeko la idadi hiyo, wanaweza kuhudumia nusu ya wagonjwa hao kutoka katika Hospitali za wilaya mkoani humo.
Aidha, hivi karibuni Hospitali yake ilipokea dawa zenye thamani ya shilingi milioni 46 kupitia fedha na ruzuku ya serikali lakini hazitoshelezi mahitaji ikilinganishwa na idadi kubwa ya wagonjwa wanaohudumiwa.
Alisema wataendelea kukabiliana na changamoto hiyo kwa kukusanya mapato kutoka kwa wagonjwa wa kawaida, mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na kuwaomba wananchi wajiunge na mifuko hiyo ili wanufaike na matibabu.
Kwa upande wake Mtaturu, alitoa wito kwa uongozi wa Hospitali hiyo, kupambana na vitendo vya rushwa na wizi wa madawa ili kusaidia wananchi wengi wasiyoweza kumudu gharama kupata matibabu kwa kuchangia kiasi cha shilingi 5,000 dirishani.
“Madaktari na watumishi wa Hospitali hiyo nao watumie muda wao kuwahudumia wagonjwa badala ya kuwanyanyasa kwani serikali imekuwa ikithamini sekta ya Afya na kutenga bajeti ambayo kwa kiasi fulani haitoshelezi, hivyo ni vyema wakatumia vifaa, dawa na utalaamu wao kuwahudumia wanyonge,”alisisitiza.
Wito wangu pia kwa wananchi waendelee kujiunga kwenye mifuko ya Afya ili waweze kupata huduma bora kutokana na wengi wao kushindwa kulipia gharama za papo kwa papo, lakini pia itawezesha wananchi kupata huduma hiyo na kuondoa malalamiko ya kushindwa kumudu gaharama.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.