ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Friday, March 6, 2015

SADIFA VIPAJI VYA WASANII WA SARAKASI VIMULIKWE NA TAASISI ZA MAJESHI NA KUPEWA AJIRA IKIWEMO KUVIENDELEZA

Kijana Hamis Juma (20), mkazi wa kijiji cha Songiwe Kata ya Misasi wilayani Misungwi mkoani Mwanza ambaye ni msanii wa mchezo wa sarakasi, akionyesha umahili wake wa kipaji cha kutembea juu ya kamba huku akicheza muziki wa nyimbo za Injili za msanii Rose Mhando wakati alipotoa burudani kwenye sherehe za kuapishwa kwa Kamanda wa UVCCM Mkoa wa Mwanza, Charles Kitwanga, wilayani humo hivi karibuni. 
 
NA PETER FABIAN, MISUNGWI.

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Sadifa Juma Hamis, amezitaka taasisi za majeshi na Wizara ya Utamaduni Vijana na Michezo kuzipa kupaumbele vipaji vya sanaa zingine ili kuvipatia ajira na kuviendeleza badala ya kuegemea kwenye vipaji vya soka pekee.

Sadifa Hamis ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Donge Unguja Zanzibar, alitoa kauli hiyo hivi karibuni wilayani Misungwi wakati wa sherehe za kuapishwa Kamanda mpya wa UVCCM Mkoa wa Mwanza, Charles Kitwanga “Mawe matatu” ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Misungwi na Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati na Madini.

Mwenyekiti huyo alimtaja kijana Hamis Juma (20) mkazi wa kijiji cha Songiwe Kata Misasi wilayani humo ambaye ni msanii wa michezo ya sarakasi aliyekosa mtu wa kumsimamia na kumsaidia kuendelea kipaji chake katika vyuo vya sanaa ikiwemo elimu ili kunufaika na kuweza kujiajili au kuajiliwa na taasisi hizo badala ya kung’ania kumlika vipaji vya soka pekee.

“Msanii huyu wa fani ya sarakasi ni mahili kweli, nimedokezwa kuwa anatoka kijijini na amekuwa akitoa burudani ya hamasa sehemu mbalimbali anapoalikwa, lakini mchezo anaoucheza kuwaburudisha ni hatari kwa maisha yake kutokana na kutembea juu ya kamba kwa miguu yake huku akichezea chupa na akiruka na kujikunja kama jongoo,”alisema.

Sadifa, alisema kwamba kutokana na kijana Juma kuonyesha kipaji chake na umahili wa kutembea juu ya kamba , amekusudia kumualika jimboni kwake ili kuhakikisha wananchi wake wanamuona na kupata burudani ikizingatiwa fani hiyo ni miongoni mwa michezo aliyokuwa akiicheza na kuipenda kabla ya kuwa kiongozi.

“Ntapeleka taarifa za kijana huyu kwa viongozi wa taasisi za majeshi, Waziri wa Vijana Utamaduni na Michezo hata kumsemea Bungeni ili kuweza kumtafuta na kukiona kipaji chake na wakiendeleze zaidi na kuwa mwanamichezo wa kimataifa, huku vijijini nimegundua vipaji vipo ila havijulikani kutokana na kutojitangaza na kupata watu wa kuwachukua,”alisisitiza.

Kwa upande  kijana Juma alisema ujuzi na kipaji hicho ni cha kuzaliwa nacho na hakuwahi kujifunza katika Chuo chochote zaidi ya kucheza kwa ubunifu na tahadhari kubwa ikizingatiwa maeneo anayoishi na kutoka hayana huduma nzuri ya Hospitali endapo ataumia na kupata majeruhi, pia sanaa hiyo ndo ajira yake ya kujipatia mkate wa kila siku.

Naye Kamanda Kitwanga, alisema amekunwa na kijana huyo atajitahidi kumtafutia Chuo cha kupata ujuzi zaidi na kujiendeleza kama vile Chuo cha sanaa Bagamoyo ili kumuwezesha kuwa mkali zaidi wa sanaa hiyo na ikiwezekana aweze kumulikwa na kuchukuliwa na taasisi za majeshi kusaidia kulinda kipaji chake na kukiendeleza.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.