ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, March 4, 2015

KITWANGA ATAMBIA SERIKALI KUDHIBITI WATUMISHI "MCHWA" WALIOFIKISHWA MAHAKAMANI KWA UFISADI FEDHA ZA MIRADI MISUNGWI

Kamanda wa UVCCM Mkoa wa Mwanza, Charles Kitwanga "Mawe matatu" akihutubia wananchi na vijana wa UVCCM zaidi ya 400 baada ya kusimikwa kwenye sherehe  hivi karibuni Mjini Misungwi.

NA PETER FABIAN, MISUNGWI.

MBUNGE wa Jimbo la Misungwi, Charles Kitwanga “Mawe matatu” amejivunia utekelezwaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika miradi mbalimbali ya maendeleo kwa asilimia 90 ikiwemo ya mtandao wa barabara, maji, afya, elimu na umeme wilayani humo.

Pia  kukuza Pato la Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, yamepanda kwa zaidi ya asilimia 300.8 baada ya Serikali kudhibiti mianya ya ulaji (Ufisadi) ikiwemo kuwachukulia hatua za kisheria ‘mchwa’ waliokuwa wakitafuna fedha za umma na kusababisha kukwamisha utekelezwaji wa miradi ya maendeleo .

Kitwanga alitoa kauli hiyo hivi karibuni Wilayani Misungwi, alisema kuwa kutokana na hatua hiyo, Serikali itaendelea kuboresha huduma za jamii na kuimarisha miundombinu ikiwemo ya barabara na maji.
 
Mbunge huyo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Madini, alisema wakati akihutubia mamia ya wananchi na vijana wa UVCCM zaidi ya 400 baada ya kusimikwa na Mwenyekiti wa UVCCM taifa, Sadifa Juma Hamisi, kuwa Kamanda wa UVCCM wa mkoa wa Mwanza.
 
“Haya, Kamanda mteule wa vijana mkoa wa Mwanza na Mbunge mwenzangu hebu njoo ueleze wananchi ulivyotekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM jimboni mwako,” alisema Mwenyekiti huyo wa UVCCM taifa na kumuita Kitwanga jukwaani.
 
Kitwanga alianza kueleza kuwa, wilaya hiyo ilikuwa na watumishi wa Halmashauri ‘mchwa’ waliokuwa wakitafuna fedha za miradi ya maendeleo ya wananchi na vyanzo vya mapato ya wilaya hiyo, sasa wamedhibitiwa na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kuwafikisha mahakamani.
 
“Mheshimiwa Mwenyekiti wa UVCCM taifa, wilaya hii ilikuwa na mchwa waliokuwa wakitafuna fedha za miradi ya maendeleo ya wananchi na za vyanzo mbalimbali vya mapato. Toka mwaka 2010 tulikuwa tukikusanya sh M 260 (kwa mwaka) lakini sasa tunakusanya zaidi ya sh B 1 baada ya kudhibiti na kuwachukulia hatua mchwa hao,” alieleza.
 
Alifafaanua kuwa, wakati wanakusanya kiasi hicho kidogo, vyanzo vya mapato ya ndani vilikuwa lakini sasa licha ya vyanzo hivyo kupunguza, wanakusanya zaidi ya asilimi 300.8 hali ambayo inadhihirisha wazi kuwa, fedha nyingi zilikuwa zikiishia mifukoni mwa watu wachache waliokuwa wakijinufaisha binafsi badala ya kutumikia wananchi.
 
Alitamba “CCM Misungwi tumetekeleza ahadi zetu vizuri na tunaendelea kukamilisha miradi iliyobaki, pamoja na kuboresha huduma za afya, elimu, maji na kusambaza umme vijijini kutoka asilimia 15 hadi 80, tunaendelea na mipango ya kuboresha shule na kupata walimu wa kutosha,” alisema.
 
Huku akishangiliwa kwa kuchapa kazi, alivitaja baadhi ya vijiji vilivyong’ara kwa umeme kuwa ni pamoja na Bujingwa, Fela, Kanyerere A na B, Kolomije, Seke, Nyamayinza, Ibongoya A na B, Sumbugu, Ngaya, Isenengeja, Mwawile, Igenge, Kasololo na Mbalama.
 
Mwaka 2010 wakati Rais Dk Jakaya Kikwete akimnadi Kitwanga kwenye uwanja wa soko la zamani mjini Misungwi, aliwaeleza wananchi wa mji huo kuwa  wilaya hiyo ina ‘mchwa’ wanaotafuna fedha za maendeleo yao na kuwaomba wachague viongozi bora watakaopambana na walaji hao.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.