NA PETER FABIAN, MWANZA.
BARAZA la Halmashauri ya Jiji la Mwanza limelidhia Menejimenti ya Jiji hilo kukopa kiasi cha Sh bilioni 7 katika Benki ya CRDB tawi la Mwanza ili kuzitumia kwenye ulipaji fidia kwa wananchi wa maeneo ya Luchelele wilayani Nyamagana jijini hapa.
Awali akiwasilisha kwa kusoma mapendekezo hayo kwa niaba ya Menejimenti na Kamati ya Fedha ya Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, Kaimu Afisa Mipango Miji wa Jiji hilo, Deogratias Kalimenze, March 9 mwaka huu, alisema kuwa mkopo wa fedha hizo utatumika kwa ajili ya ulipaji fidia kwa wananchi wa maeneo ya Luchelele ili kupisha mradi wa uuzaji wa viwanja.
“Halmashauri ya Jiji ilitenga maeneo ya Luchelele Kati, Ziwani na Shadi yaliyo Kata ya Mkolani kwa ajili ya uanzishwaji Mji mpya wa kisasa utakaokuwa na Miundombinu muhimu ya utowaji huduma kwa jamii, maeneo ya Sekta za Afya, Elimu, Miundombinu ya Maji, Barabara, Viwanja vya Michezo, Makazi bora kwa Jamii, Biashara, Masoko na Uwekezaji wa Mahoteli,”alisema.
Kalimenze alisema kuwa Halmashauri hiyo ilianza utekelezaji wa mradi huo mwaka 2006 kwa kufanya upimaji wa viwanja na kulipa fidia maeneo ya Luchelele Ziwani na viwanja hivyo kumilikishwa kwa waombaji mbalimbali, eneo lililobaki la Luchelele kati, Nganza kati na Shadi kufanyiwa uthamini mapema mwaka 2012 kabla ya kuibuka mgogoro wa ardhi Januari 27 mwaka 2013.
“Hali ya mgogoro huo kuibuka ulisababisha kukwama kwa hatua zilizokuwa zimeanza kuchukuliwa na Halmashauri ya Jiji, kuingia makubaliano ya kuomba mkopo wa fedha kiasi cha zaidi ya Sh bilioni 20 kutoka Banki ya Maendeleo (TIB) na kukwamisha utekelezaji wa ulipaji fidia kutokana na kukamilika zoezi uthamini wa mali za wananchi na ukadiriaji wa gharama yaa miundombinu,”ilisema taarifa hiyo.
Aidha taarifa hiyo iliongeza kuwa kutokana na mgogoro huo kudumu kwa kipindi kirefu hadi mwezi Agosti 2014, Halmashauri kushindwa kufaniniwa kupata mkopo na kibali cha kukopo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu- TAMISEMI kutokana na changamoto hiyo na kushindwa kuendelea na ujenzi eneo la mradi.
“Halmashauri ilikaa na wananchi na kutoa mapendekezo yake ambayo yalilidhiwa na pande zote mbili za wananchi na Halmashauri ambapo ilianza upya utekelezaji wa mradi kwa kushirikiana na wananchi katika kikao cha pamoja Januari 27 mwaka 2013 na baada ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Wenyeviti wapya wamekuwa wakishawishi wananchi kutolipa fedha za viwanja vyao hadi ulipaji fidia utakapotekelezwa,”alisema Kalimenze.
Afisa huyo alisema kuwa kazi ya uhakiki upya maeneo ya viwanja ilianza rasmi Septemba 23 mwaka 2014 na jumla ya watu 1444 wamefanyiwa uhakiki maeneo yao, jumla ya viwanja 1690 vimehakikiwa na viwanja 1385 vimemilikishwa kwa wananchi kuwa mali yao na viwanja 305 vitachukuliwa na Halmashauri katika mradi wa uuzaji viwanja na viwanja 385 viliingiliana na maeneo ya umma wamiliki wake watalipwa fidia huku Jiji hilo kuingiza faida ya Sh bilioni 7.3 baada ya kutolewa gharama zote zikiwemo deni na liba ya mkopo.
Meya wa Halmashauri ya Jiji hilo, Stanslaus Mabula, ambaye ni Diwani wa Kata ya Mkolani (CCM) aliwahasa wajumbe wa kikao cha baraza kupitia taarifa kwa umakini na kujua faida zake ikiwemo sera ya uanzishwaji Miji mipya na uendelezaji makazi bora ili uamuzi wa azimio watakalotoa la kukubali Halmashauri yao kukopa Sh bilioni 7 usije ukazaa hoja za Ukaguzi badae, lakini pia kuwasaidia wananchi ili walipwe fidia kutokana na mgogoro huo uliosababisha kushindwa kuendeleza maeneo hayo.
Mabula alisema kuwa uamuzi wa hatua hiyo wa Baraza uliolidhiwa na wajumbe wake wote, baada ya kujadiliwa kwa kina na kujibiwa hoja za madiwani juu ya faida ya mkopo na utekelezwaji wa mradi huo kisha kupitishwa kwa kauli moja bila kuingiza masuala ya Itikadi za Vyama vyao vya Siasa ili kuwezesha wananchi wa maeneo hayo kulipwa fidia na kumaliza mgogoro huo uliodumu kwa miaka saba.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.