Mbunge wa Jimbo la Misungwi, Charles Kitwanga “Mawe Matatu” |
MBUNGE wa Jimbo la Misungwi, Charles Kitwanga “Mawe Matatu” ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kupeleka kwa wakati fedha iliyotengwa kiasi cha Sh milioni 45 kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Mwagimagi Kata ya Ilujamate.
Kitwanga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Madini alitoa kauli hiyo jana wakati alipofanya ziara ya kutembelea jimboni humo katika kijiji cha Mwagimagi Kata ya Ilujamate na kusomewa taarifa ya wananchi ambayo ilieleza wananchi kuchangia fedha na nguvu kazi na kujenga jengo la Zahanati ya kijiji hicho.
Mbunge alimwagiza Mukurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Nathan Mushana na Wakuu wa Idara alioambatana nao kuhakikisha wanapeleka fedha kiasi cha Sh milioni 45 ili kukamilisha jengo la Zahanati ya kijiji kutokana na wananchi kulijenga kwa nguvu kazi ambalo tayari limepauliwa na kupigwa ripu kwa gharama ya kiasi cha Sh.14,771,000/= milioni.
“Halmashauri kupitia bajeti yake ya mwaka wa fedha wa 2014/2015 tulitenga kiasi cha fedha Sh. milioni 45 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa Zahanati ya kijiji hiki lakini nimesikitishwa na taarifa kuwa hamjaletewa hata robo ya fedha hizo, hivyo Kaimu Mkurugenzi toeni fedha hizo na kuhakikisha zinakamilisha ujenzi na kuwekwa vifaa na Zahanati ianze kutoa huduma kwa wananchi,”alisisitia.
Kitwanga “Mawe Matatu” aliuagiza pia uongozi wa Kata (WDC) kupitia upya mhutasari wa mgawanyo wa vijiji vinavyounda Kata ya Ilujamate ili kuondoa malalamiko ya wananchi kuwa haukuzingatia asili ya ujirani wa vijiji hivyo ni vyema kuunganishwa kwa vijiji vya Mwagimagi, Buhunda na Gukwa ili kuwa Kata ya Buhunda.
“Taarifa yenu imeeleza kuwa mnalalamikia mgawanyo huu ulivyo sasa kwani wananchi utembea umbali mrefu kufika makao makuu ya Kata hivyo lazima WDC mkae na mtuletee Halmashauri ili kuangalia jinsi ya kulitafutia ufumbuzi suala hili ikiwemo mipaka ya Kata na suala la barabara ntahakikisha fedha ya ujenzi wake zilizo katika bajeti ya mwaka huu 2015/2016 zinatumika kulijenga,”alisisitiza.
Awali taarifa ya kijiji iliyosomwa na mjumbe wa serikali ya kijiji, Emmanuel Lubinza, ambapo ilieleza mbali na kutokamilika kwa ujenzi wa zahanati hiyo pia kijiji hicho kwa sasa hakina huduma ya Afya na hutembea umbali mrefu kupata huduma hiyo katika vijiji vya jirani vilivyopo katika Kata za jirani jambo ambalo ni adha kubwa kwa wananchi.
Aidha taarifa hiyo ilieleza kuwa kijiji hicho pia kinakabiliwa na changamoto za upungufu wa walimu sita katika shule ya Msingi Mwagimagi, upungufu wa madawati 280 na nyumba za walimu nane katika shule hiyo pamoja na kukoseka kwa miundombinu ya barabara ya kutokea kijiji cha Ishokela kupitia Mwagimagi hadi kijiji Mwamazengo.
“Tunaomba pia msaada wako Mheshimiwa Mbunge wa kufikishiwa miundombinu ya maji safi na umeme ambao umefika kijiji jirani cha Ishokela ili kusaidia kufika katika Zahanati yetu ya kijiji na shule ya msingi na ofisi ya kijiji,”ilisisitiza taarifa hiyo.
Mbunge Kitwanga, alitoa wito kwa wananchi kuanza kusoma nakala za vitabu 153 vya Katiba inayopendekezwa walivyogawiwa katika Kata ya Ilujamate na kusambazwa kwa wanainchi wa vijiji vya Kata hiyo ili kusaidia kupitia masuala muhimu yanayohusu Taifa ikiwemo ya wafugaji, wakulima kabla ya kupiga kura ya maoni ili kuwajengea upeo wa kuijua Katiba watakayoipigia kura.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.