ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, December 31, 2014

WAVUVI, WAFANYABIASHARA WA SAMAKI NA DAGAA WATAKIWA KUTUMIA VIPIMO SAHIHI VISIWA VYA UKEREWE NA SENGEREMA

 NA PETER FABIAN, MWANZA.
WAVUVI na Wafanyabiashara wa samaki na dagaa wa Visiwa vya Wilaya za Ukerewe na Sengerema mkoani Mwanza, wamepewa Elimu na kushauriwa kufanya biashara zao ya kuuza na kununua bidhaa hiyo kwa kutumia vipimo vinavyokubalika na kutamburika kisheria na Wakala wa Vipimo (WMA) nchini.

Akizungumza na MTANZANIA jana Jijini Mwanza, Mkuu wa Kitengo cha Vipimo kutoka Ofisi ya Wakala wa Vipimo Jijini Dar es salam, Zainabu Kafungo, alisema baada ya kufanya ziara katika visiwa vya Ghana, Kamasi, Burubi na Siya (Ukerewe) na visiwa vya Kanyara, Kijiweni na Mchangani (Sengerema) na kutoa elimu kwa wavuvi hao.

“Tumejionea wavuvi wanavyopunjika kwa kufanya biashara za dagaa kwa kutumia kisado na ndoo za prasitiki ambazo kimsingi si vipimo sahihi na kuwashauri kutumia kipimo cha muundo unaokubalika kisheria na kuthibitishwa na serikali kupitia wakala wa vipimo nchini,”alisema.

Kafungo alieleza kuwa kipimo kinachokubalika ni kile ambacho kimekaguliwa na kuhakikiwa na WMA kiwe na mhuri wa serikali na kutumia kisicho kipimo kwenye biashara ni kosa la jinai chini ya sheria ya vipimo sura ya 340 iliyofanyiwa mapitio mwaka 2002 na kanuni zake,”alisisitiza.

Mkuu huyo, alieleza kuwa wakiwa visiwa hivyo walivyotembelea wavuvi wengi walikubaliana na elimu waliyopewa na kuahidi kufanya biashara ya kutumia vipimo ili kuwasaidia kupata faida na kuwawezesha kupiga hatua za kimaendeleo badala ya kuwa watumwa wa wafanyabiashara na mawakala wanaokuja kununua samaki na dagaa kwa bei ya chini.

 Akizungumzia biashara ya dagaa na samaki inayofanyika katika soko kuu la kimataifa la Mwaloni Kirumba, alisema kuwa bado ni ukiukwaji wa sheria kwani wafanyabiashara wengi pale hawtumii vipimo vinavyotambulika na serikali na kusababisha soko hilo kukosa hadhi ya kuwa la kimataifa.

 “Hakuna biashara ya kimataifa isiyozingatia vipimo ambavyo vinakubalika na kuhakikiwa na kuwa na mhuri wa serikali ya nchi husika, wafanyabiashara wa dagaa kutumia magunia ya lumbesa na visado na ndoo hakuhalalishi vipimo hivyo kwakuwa havitamburiki kisheria na badala yake watumie minzani sahihi,” alisema.

Kafungo ametaka serikali kuharakisha kupitisha sheria mpya ya vipimo ili kusaidia kukomesha wizi na udanganyifu wanaofanyiwa wavuvi visiwani na walaji katika masoko kwa kutumiwa vipimo vinavyowapunja na kudumaza maendeleo ya sekta ya uvuvi endelevu na biashara halali vyenye tija na kuwanufaisha kwa kupiga hatua za maendeleo.

Mkuu huyo alisema bado sheria zinazotumiwa na wakala wa vipimo zinaonekana kudharaulika na pengine kubezwa na watuhumiwa wanaokamatwa katika ukaguzi wa vipimo kutokana na sheria inayotumika ni ile ya mwaka 1982 kuonekana kupitwa na wakati na kutokuwa na makali ya kuogopwa na watuhumiwa wanaokamatwa kuvunja sheria na kanuni zake.

 “Mtuhumiwa akikamatwa, kosa la kwanza hutozwa faini isiyozidi Sh.10,000/= au kifungo cha miaka mitatu jela au vyote kwa pamoja, akikutwa na kosa la pili hutozwa faini isiyozidi Sh.20,000/= au kifungo cha mika saba jela au vyote kwa pamoja, hivyo mkosefu huweza kutenda kwa kuona anao uwezo wa kulipa faini bila kuathiliwa mtaji wake,”alisema.

Ametowa wito kwa Wizara ya Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo kupitia Maafisa wake kushirikiana na WMA kuhakikisha wavuvi na wafanyabiashara wanatumia vipimo halisi (Minzani) ili kuwezesha kuwa na takwimu sahihi za kiasi cha samaki na dagaa zilizovuliwa na kuuzwa ndani na nje badala ya ilivyo sasa jambo ambalo hupelekea kutolewa takwimu zisizosahihi.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.