![]() |
| Mbali na tuzo lukuki zilizojaa ofisi ya Halmashauri ya jiji la Mwanza, basi hizi ni tuzo mbalimbali zilizotwaliwa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mwanza. |
MWANZA.
CHUO cha Maafisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Monduli Arusha, kimetoa tuzo kwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa utoaji bora wa huduma za jamii mkoani hapa.
Tuzo hiyo imekabidhiwa jana na Brigedia Jenerali A. F. Kapinga akiongozana na maafisa 27 wa majeshi ya ulinzi wa mipaka ya nchi za Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda ambazo zipo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki , pia Namibia, Zambia , Zimbabwe toka SADC na wenyeji Tanzania.
Akizungumza wakati akikabidhi tuzo hiyo, Brigedia Jenerali Kapinga kwa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Halfa Hida, alisema kunatokana na kutambua mchango wa Halmashauri hiyo katika kutoa huduma za kijamii na kuishirikisha jamii katika utekelezaji wa miradi yao ya maendeleo.
“ Jiji la Mwanza limekuwa ni mfano katika mapambano ya usafi na utunzaji mazingira na kusababisha kuwa mshindi kwa mara tisa mfululizo lakini pia limeweza kuishirikisha jamii katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye kata zote 12 za jimbo la Nyamagana,” alisema.
Brigedia Kapinga alisema kwa maofisa hao wa majeshi ya ulinzi kutoka katika nchi hizo kutembelea Jiji imelenga kuwajengea uwezo maofisa hao ili kushirikiana na jamii katika nchi zao na kujifunza jinsi taasisi za umma zinavyoweza kutoa huduma za jamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Hida alipongeza Chuo hicho kwa kutoa tuzo hiyo pia maafisa hao kutembelea Jiji lake na kujifunza jinsi halmashauri yake inavyoshirikiana na jamii katika utekelezaji wa sheria na miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
“ Halmashauri hii imekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha jamii kushirikiana katika utekelezaji wa mambo mbalimbali ya kijamii pia kuishirikisha jamii katika kuchangia maendeleo pamoja na kuboresha kipato pia uchumi wa taifa kutoka kwenye vyanzo vyake vya mapato,” alisema.
Mkurugenzi aliwataka maafisa hao kushirikiana na jamii katika mataifa yao katika kudumisha na kuendeleza mahusiano ya ushirikishwaji wa wananchi wakati wa utoaji huduma za afya, elimu, maji, miundombinu ya barabara, mawasiliano na kuwaelimisha kushiriki katika ulinzi wa mataifa yao.
Maafisa hao 27 walio kwenye mafunzo katika chuo cha Monduli mkoani Arusha walipata fursa ya kutembelea miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa jengo la kitega uchumi la Mwanza City Commecial Complex Company Ltd (MCCCCL), ujenzi wa uwanja wa michezo wa Nyamagana, barabara zilizojengwa kwa mawe eneo la Capl point.
Tupe maoni yako

0 comments:
Post a Comment