ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, October 8, 2014

HALMASHAURI YA JIJI YATOA KIASI CHA TSH BL 1.3 KUSAIDIA UJENZI WA MAABARA YATAKA WADAU WAWEKEZAJI KUCHANGIA

NA PETER FABIAN, MWANZA.                                                      

MKURUGENZI wa Halmashauri ya  Jiji la Mwanza, Halifa Hida, amesema  kimetolewa kiasi cha shilingi bilioni 1.3 kusaidia ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara kwa kila shule ya sekondari katika Kata 12 za Jimbo la Nyamagana mkoani Mwanza.

Hida alieleza kuwa hatua hiyo imelenga kusaidia ujenzi huo kwenda haraka ili kukamilisha utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Jakaya Kikwete, kuwa ifikapo Desemba kila sekondari moja iwe na maabara tatu za Baiologi, Kemia na Phizikia.

“Hii ni mara ya pili kusaidia ukamilishaji wa maabara za sekondari baada ya awamu ya kwanza ya ujenzi wa maabara 22 katika shule za sekondari 30 zilizopo kwenye Kata 12 ambazo tayari zimekamilika na kutumiwa na wanafunzi, na awamu hii tumejipanga kuhakikisha ujenzi wa maabara 68 zinakamilika kwa wakati kama ilivyoagizwa,”alisema.

Hida alieleza kuwa mbali na fedha hizo pia wamepeleka vifaa ikiwa ni saruji mifuko saba kwa kila chumba cha maabara ya sekondari iliyotolewa na mwekezaji na mfanyabiashara , Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwanza Huduma, Zuri Nanj, kiasi cha mifuko 500 ili kusaidia ujenzi huo.

Kwa upande wake Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Stansilaus Mabula, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mkulani (CCM), alisema hatua hiyo imelenga kukamilisha ujenzi huo kutokana na utaratibu wa ushirikishwaji wa wananchi, Halmashauri na Serikali Kuu kuchangia maendeleo.

“Halmashauri imeweza kupeleka kiasi  hicho kutokana na kuboresha na kuongeza uwezo wa ukusanyaji wa mapato kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani ili kusaidia ujenzi huo kukamilika kwa wakati na tunataraji ifikapo Novemba 20 mwaka huu kazi hiyo ya ujenzi itakuwa imekamilika,”alisisitiza.

Mabula alisema kwamba Taasisi hiyo ingeamua kufanya ujenzi huo kwa kufuata taratibu za manunuzi ya umma (BQ) gharama ingekuwa kubwa zaidi kwani chumba cha maabara kimoja kinagharimu kiasi cha shilingi milioni 80 hivyo uamuzi wa kupeleka fedha hizo kwa wananchi katika Kata utasaidia kuharakisha ujenzi huo.

“Sisi kama Halmashauri tunachangia asilimia 10, Serikali Kuu asilimia 70 na wananchi asilimia 20 ikiwa ikiwemo nguvu kazi kwa utaratibu wa ushirikishwaji ili kuhakikisha hili linafanikiwa tayari Halmashauri imeisha peleka fedha hizo kwenye Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) ili kusimamia ujenzi huo,”alisema.

Meya aliongeza kuwa mbali na fedha hizo pia Halmashauri tayari imeisha peleka pia fedha za maendeleo kwa kila Kata moja kiasi cha shilingi milioni 10 kusaidia kukamilisha miradi ya maendeleo iliyoibuliwa na wananchi kwenye Kata kwa dhana ya ushirikishwaji ambapo hadi sasa jumla ya shilingi milioni 120 zimetolewa kwa Kata zote 12 za Jimbo la Nyamagana.

Mabula ametoa wito kwa wadau wa maendeleo, wawekezaji na wafanyabiashara waliopo Jijini humo na waliopo nje wanaotoka Jiji hilo kujitokeza na kuunga mkono ujenzi wa maabara kwa kusaidia fedha na vifaa ili kuwapunguzia wananchi mzigo na kuiwezesha Halmashauri kukamilisha ujenzi haraka kama ilivyoagizwa na Rais Dkt. Kikwete.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.