MWANZA.
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) jana imezindua mwendelezo wa utekelezaji mpango wa kunusuru kaya maskini milioni moja zenye wakazi milioni 6.5 katika Halmashauri na Manispaa 161 nchini.
Kaimu Mkurugenzi wa TASAF, Godwin Mkisi ambaye ni meneja wa fedha makao makuu alisema wakati wa uzinduzi wa warsha ya mafunzo kwa wataalamu na madiwani na wadau wa jamii uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwamba awamu ya tatu inashirikisha halmashauri 33 ikiwemo Jiji katika mikoa ya Mwanza, Morogoro, Pwani, Tanga na Simiyu.
Mkisi alisema mpango huo unataraji kutekelezwa kwa awamu mbili ndani ya miaka kumi ambapo kila awamu moja itakuwa ya miaka mitano na unaolenga kaya maskini zaidi .
“ utekelezaji wa mpango huu umelenga kuwajengea uwezo kwenye mfumo wa kijamii , katika ngazi zote za utekelezaji ili kuwezesha uelewa mzuriwa kanuni na taratibu za utekelezaji wake.” Mkisi.
Aidha alieleza umakini wa wawezeshaji ambao ni munimili muhimu ili kuondokana na familia zinazoishi maisha duni kwenye lindi la umaskini uliokithiri hapa nchini utapungua endapo mpango huu utatekelezwa kikamilifu katika kaya zilizoingizwa mpango huo kabambe.
Mkisi alifafanua kuwa mpango huo utatekelezwa katika sehemu kuu nne, kwanza ni uhawilishaji wa fedha utakaotoa ruzuku kwenye kaya masikini zaidi, pili kuongeza kipato kwa uwekaji akiba.
Tatu, kutoa ajira za muda kwa wananchi wa kaya masikini zaidi wenye uwezo wa kufanya kazi hususani wakati wa hari na kujenga pia kuboresha miundombinu inayolenga sekta ya afya, elimu na maji.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Evarist Ndikilo ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema katika utekelezaji wa mpango huo uliozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete Februari 15 , 2012 mjini Dodoma.
“ Mpango huu ulizinduliwa kwa lengo la kunusuru kaya maskini ukilenga kuimarisha uwazi, uwajibikaji na kutoa fursa kwa makundi mbalimbali ya kijamii kushiriki kwa nia madhubuti,” alisema.
Pia Ndikilo alieleza usimamizi na utekelezaji wa awamu hii ya tatu uzingatie vyema changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa awamu ya pili katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mwanza katika wilaya za Sengerema , Nyamagana, Ilemela, Misungwi, Kwimba, Magu na Ukerewe pia mikoa ya kanda ya ziwa.
“ Katika Halmashauri za Wilaya, Jiji na Manispaa pia kata zote zifuatilie kwa ukaribu utendaji wa shughuli za mfuko wa maendeleo ya jamii zisiingie kwenye malengo yasiyokusudiwa ,” alieleza.
Mpango huu unaendele kutekelezwa kikamilifu katika halmashauri zote Tanzania Bara pia Zanzibar katika visiwa vya Pemba na Unguja kuhakikisha azma ya serikali ya kuwakomboa wananchi dhidi ya umaskini ili wapate maendeleo na huduma bora za kijamii huku mpango huu usipotoshwe na baadhi ya wanasiasa kwa manufaa yao ya kisiasa bali ulenge zaidi kuwaelimisha.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.