Kufuatia habari zilizozagaa kwenye duru mbalimbali za kisiasa, vyumba vya habari na mitandao ya kijamii, habari zinasema kuwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Nzega, Mkoani Tabora, Dkt. Hamisi Kigwangalla, ambaye katika nyakati tofauti tofauti amekuwa akitajwa kuwania Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka 2015.
Japokuwa amekuwa akikanusha habari hizi mara kadhaa kwenye vyombo vya habari alipohojiwa, uchunguzi umebaini kuwa ameonekana kwenye maeneo kadhaa akifanya mambo yanayoashiria uwepo wa mkakati uliojificha wa kutafuta namna ya kuungwa mkono kwenye safari ya kuelekea nyumba nyeupe, Magogoni.
Mwenyekiti huyo wa Kamati nyeti ya TAMISEMI amekuwa akitajwa kuwa chaguo la vijana wengi nchini kwa namna alivyokaa mstari wa mbele ndani na nje ya Bunge kutetea maslahi ya vijana hususan mikakati ya kukuza ajira kwa vijana, utetezi kwa wamachinga na mama ntilie, pia amekuwa akiungwa mkono na makundi mbali mbali kutokana na aina ya siasa zake kuwa kila mara amekuwa akitetea wanyonge na wanaokandamizwa kwa nguvu kiasi cha kufikia kuwekwa chini ya ulinzi mkali wa polisi ili kutuliza ghasia: mfano wa makundi hayo ni pamoja na kundi kubwa la wachimbaji wadogo wadogo na makundi makubwa ya kada za watumishi wa umma kwenye sekta za elimu na afya.
Makundi mengine nyeti kwenye jamii ambayo kwa nyakati tofauti tofauti yamekuwa yakitoa kauli zilizoashiria kumuunga mkono Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Bunge ya TAMISEMI ni pamoja na viongozi wa dini, Maaskofu kule Zanzibar na Masheikh kule Morogoro.
Mchunguzi yeyote yule wa masuala ya siasa hapa nchini hawezi kusema kauli zote hizi zilitoka bure tu! Panapofuka moshi kwa kiasi kikubwa pana moto chini yake.
Habari za kiuchunguzi zimebaini uwepo wa maandalizi mazito ya mkutano nyeti na waandishi wa habari katika hoteli maarufu ya kitalii jijini Dar es salaam katika siku za usoni.
Habari hizi tumezinyaka mtaani kutoka kwa waandaaji wa mkutano huo ambao ni wasaidizi na watu wa karibu na Mbunge huyo. Inasemekana wameonekana wakiandaa mkutano wa aina yake ambao utaunganisha mawasiliano ya ‘live media streaming’ kutokea jimboni kwake ambapo kutakuwa na wananchi wakirekodiwa ‘live’ wakishuhudia “namna Mbunge wao anavyotangaza nia kutokea Dar es salaam, na watu wa ukumbini wakishuhudia namna wananchi watakavyopokea tangazo la Mbunge huyo machachari wa Nzega”, kilisema chanzo chetu cha habari kwa masharti ya kutotajwa.
Aidha wasaidizi hao walionekana wakifanya mawasiliano na makampuni kadhaa mahiri ya kazi za mawasiliano ya mitandaoni kwa lengo la kurusha kwenye mitandao ya kijamii moja kwa moja (online streaming) kinachotokea kwenye ukumbi wa hotel ambapo mbunge huyo atakuwa akihutubia waandishi wa habari na wadau mbalimbali watakaokuwa wamealikwa.
Alipohojiwa na mwandishi wetu, Dkt. Kigwangalla, alianza kwa kuhoji kwa mwandishi wetu; “nani kakuambia kwamba ninaandaa mkutano kwa ajili ya kutangaza nia?”, kasha akendelea kusema: “…ni kweli ninapanga kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu jambo hilo lakini sijasema ni lini, wapi na kwa staili gani na kama nitaitika wito wa wapenzi na washabiki wangu kuwa nami niingie kwenye kinyang’anyiro cha kutafuta ridhaa ya Chama changu kwenye nafasi hiyo nyeti ama la, lakini nimekusudia sasa kusema neno moja kati ya hayo, ili kumaliza hizi tetesi na hisia zilizozagaa kila mahali.”
Aliendelea kusema kuwa: “nimechoka kujibu hili swali kila ninapokwenda, sasa nadhani nalazimika kusema neno. Muda wa tafakuri umeisha…lazima niseme kitu kuondoa mashaka ya watu.”
Mbunge huyo ambaye amejizolea umaarufu mkubwa nchini ndani ya kipindi kifupi sana cha kuutumikia umma kutokana na misimamo yake tata na staili ya usemaji na ufuatiliaji wa maslahi ya wananchi, pia uchungu kwa Taifa na raslimali za Taifa, anafanya idadi ya wanaotajwa ama waliokwisha weka wazi nia zao za kutafuta ridhaa ya kugombea Urais kutokea CCM na ambao wako katika umri wa miaka kati ya 40 na 50 kufikia wanne. Wengine ni pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na mbunge wa Bumbuli, January Makamba na Mbunge wa Songea Mjini, Emmanuel Nchimbi.
Kama Dkt. Kigwangalla atatangaza nia ya kuwania Urais mwaka 2015, atakuwa wa pili miongoni mwa kundi hili. Hivi karibuni, Mbunge wa Bumbuli na Naibu Waziri wa Mwasiliano, Sayansi na Teknolojia akihojiwa na mtangazaji Salim Kikeke wa BBC Swahili, alisema ana asilimia 90 kuwa atagombea Urais mwaka 2015; jambo lililozua mjadala mkali kuhusu ujana na Urais. Je, ni wakati wa vijana kushika nafasi hii kubwa na nyeti ya uongozi wa Taifa letu? Wakati utasema.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.