ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, July 28, 2014

BAADHI YA WATUMISHI KUSHINDWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO NI KUDHOROTESHA UCHUMI WA NCHI.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara Mwiguru Nchemba (wa tatu kutoka kushoto), Mwemyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza Anthony Dialo (wa pili kutoka kushoto), Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza Joyce Masunga (wa kwanza kushoto), Mjumbe wa NEC toka Zanzibar (wa kwanza kulia) na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Evarist Ndikilo (Nyuma) wakiwasili kufungua Shina la vijana eneo la  Furahisha juzi kabla ya kuhutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara viwanja vya Furahisha .

Naibu Katibu Mkuu CCM Bara Mwiguru Nchemba akisalimiana na vijana  wajasiliamali wa Shina la Waketeketwa wa CCM eneo la Furahisha jana kabla ya kulizindua na kuwachangia kiasi cha Sh. milioni 2 ili kuwaongezea mtaji wa kikundi chao. 
"Sasa nalifungua rasmi shina hili" Naibu Katibu Mkuu CCM Bara Mwiguru Nchemba.
Katibu wa Vijana wajasiliamali wa Shina la wakereketwa eneo la Furahisha akisoma lisala kwa  mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu CCM Taifa Mwiguru Lamaeck Nchemba jana jijini Mwanza.
"Hongereni kwa kutoa burudani nzuri kwa mamia ya wananchi waliofika kunisikiliza katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza " Ni Kundi la Msanii maarufu Mchele Mchele kutoka Kisesa Wilayani Magu.
"Hamjambo, mambo poa siyo"
Naibu Katibu Mkuu CCM Bara Mwiguru Nchemba akiwa ameongozana na viongozi wa Mkoa, Taifa na Wilaya kuwasili katika viwanja vya furahisha jana jijini Mwanza.
Tunafikisha ujumbe wetu kwa njia ya Mabango yetu.
"Huu ndiyo Ukweli wa ujumbe wetu kwa waliohudhulia mkutano wa hadhara Naibu Katibu Mkuu CCM Bara Mwiguru Nchemba viwanja vya Furahisha jana jijini Mwanza. 
"Mnasoma na kuuona ujumbe wetu"
Naibu Katibu Mkuu CCM Bara Mwiguru Lamerck Nchemba ambaye pia ni MNEC, Naibu Waziri wa Fedha na Mbunge wa Jimbo la Ilamba Magharibi mkoani Singida akihutubia wananchi katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza.
Sehemu ya umati wa wananchi wakiwemo wana CCM kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa na Jiji la Mwanza waliohudhulia mkutano wa hadhara wa Naibu Katibu Mkuu CCM Bara Mwiguru Lamerck Nchemba kwenye viwanja vya Furahisha jana jijini Mwanza.
"CCM oyeee!! " Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana Raphael Shiratu akisalimia mamia ya wananchi katika viwanja vya Furahisha kabla ya Naibu Katibu Mkuu wa CCm Bara Mwiguru Lamerck Nchemba jana.
"Hawavumi lakini wamo ni wasanii wakereketwa wa CCm wakifanya vitu vyao jukwaani jana katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza.
Msanii maarufu Mchele Mchele na Kundi lake akitoa burudani viwanja vya Furahisha jana.
NAIBU waziri wa Fedha Mwiguru Nchemba, amesema kitendo cha kushuka kwa uchumi nchini kinatokana na kuwepo na baadhi ya wafanyakazi wa sekta za umma pia wakitumia mwanya wa kufuja fedha za miradi ya maendeleo huku wakishindwa kusimamia majukumu yao ipasavyo.

Mwigulu ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Taifa na Mbunge wa Jimbo la Ilamba Magharibi mkoani Singida alisema hayo jana alipokuwa akihutubia umati wa wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza.

Kauli hiyo imekuja wakati Tanzania ikiwa inakabiliwa na deni kubwa linalopelekea serikali kushindwa kulipunguza kutokana na baadhi ya watendaji na watumishi wa serikali kushindwa kusimamia kanuni na taratibu za matumizi ya fedha hali inayopelekea wananchi kuona bado ni masikini na huduma zikiwa hazipatikani kwa wakati.

Nchemba ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha na Mbunge wa Jimbo la Ilamba Magharibi (CCM) alisema kuwa deni la taifa zaidi ya trioni 29.9 limetokana na kuwepo kwa watumishi wa umma kushindwa kutekeleza wajibu wao huku wakienda kinyume na kanuni na sheria za manunuzi na kusababisha kuwepo matumizi mabaya ya fedha za serikali na wananchi walipa kodi.

“Tutafuta misamaha yote na hatutakubali kama Wizara kuletewa mipango ya ulaji fedha ikiwa ni kuomba fedha kwa ajili ya vikao semina na sherehe mbalimbali wakati wananchi wanahitaji maji, umeme na dawa ,” alisema na kuongeza kuwa.

Tumeagiza kupunguza sherehe za maadhimisho ya Kifua Kikuu (TB), Mazingira, Unywaji wa maziwa, maji na mengine zaidi ya 60 yanayolenga kutafuna kwa fedha za walipa kodi ambao huangaika kupata huduma muhimu zikiwemo za Afya, Elimu, Umeme na Miundombinu ya Barabara.

Nchemba alisema kwamba watumishi wa umma wanaofuja fedha na kusahau kuwatumikia wananchi wajiandae kuwapisha vijana wasomi kwenye nafasi zao kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao na kupelekea taifa kuongeza mzingo wa madeni ya ndani na nje.

Aliongeza kuwa hawatashindwa kuwachukulia hatua kali za kimaadili na kuwaondoa kwenye nafasi hizo walizonazo na sasa dawa inachemka ya kuwawajibisha na wao wajiandae kufungasha virago.

Nchemba alisema watu waliokuwa wakiishi kwa  kukwepa kodi na kwa misamaha ya kodi isiyo na tija wakati wao umefikia mwisho, badala yake watafute utaratibu rasmi wa biashara watakayofanya huku "wanaoidai serikali tunaendelea kuhakiki madeni yote ya ndani na nje kabla ya kuanza kuwalipa" alisisitiza.

"Serikali imekuwa ikikosa mapato mengi kutokana na misamaha ya kodi inayotolewa kwa Watu wasiostahili. Kwa sababu misamaha hiyo haiwasaidii watanzania wa kawaida, jambo hilo halikubaliki na sasa lishafikia kikomo" alisema Mwigulu.

Alisema kupitia usimamizi mzuri wa kodi na matumizi ya fedha, serikali katika mwaka huu wa fedha 2014/2015 itahakikisha inalipa madeni ya watumishi hasa walimu ambao ni zaidi ya nusu ya watumishi wote wa umma.

Aidha alisisitiza kuhusu utaratibu mpya ulioanzishwa na serikali kupitia wizara yake, wa ununuzi wa magari kwa mfumo wa pamoja na Wizara itanunua moja kwa moja kutoka Kiwandani au kwa watengenezaji tofauti na mfumo wa awali wa kila Wizara na Taasisi kununua kwa wakati wake.

Mwigulu alisema kuwa mfumo huo wa awali wa ununuzi wa magari ulitoa kibali kwa kila ofisi kuagiza gari kwa utaratibu wa kujitegemea na kupitia mawakala kitendo ambacho kiliongeza gharama na urasimu kwa serikali.

"Serikali imekuwa ikipata hasara kwa kutokuwa na mfumo wa pamoja wa uagizaji magari kutoka kiwandani, badala yake walanguzi ndiyo wamekuwa wakishiriki biashara hiyo kwa kuongeza bei tofauti na ile ya kiwandani, hilo Ndugu zangu sasa ndiyo mwisho" alisisitiza.

Aliwapongeza pia wananchi wa Mkoa wa Mwanza kwa kukiiunga mkono Chama cha Mapinduzi kuwahakikishia kuwa yale yote yaliyoahidiwa watahakikisha yanatimia.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza Anthony Diallo alisema, kazi inayofanywa na uongozi wa juu wa CCM ni ya kutia moyo, na kwamba yeyote mwenye ndoto ya kushindana na CCM hivi sasa anapoteza muda wake.

"Wananchi wenzangu, Mimi ninaimani Kubwa sana na Naibu Katibu Mkuu Mwigulu, pia Nina Imani Kubwa sana na Sekretarieti nzima ya CCM chini ya Abdulrahman Kinana, kazi wanayofanya ya kupigania wanyonge inaonesha kiwango cha uzalendo walichonacho, cha muhimu tuwaunge mkono" alisema Diallo.

Alisisitiza kuwa hata yeye nguvu aliyonayo katika kuwatumikia wanaCCM na wananchi wa Mwanza  inatokana na Imani yake kwa Mwigulu  anayefanya kazi usiku na mchana kuhakikisha ahadi zinatekelezwa CCM inakuwa chaguo la watanzania ili kuwatumikia bila kuwabagua.

Aliongeza kuwa kasi ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa mwaka 2010/2015 na namna sekretarieti mpya ya CCM inavyosukuma na kusimamia shughuli za maendeleo nchini, ni dhahili kuwa umaskini utaondoshwa nchini kwa kasi kubwa.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.