Ili kuboresha suala la utoaji huduma na kutetea masilahi yao kwa waajiri wao na kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo udhibiti wa wizi kwa mali za wateja, Mameneja na Wafanyakazi wa Mahoteli Mkoani Mwanza wameanzisha ushirika wa umoja wao.
Mwenyekiti wa ushirika huo Shijan Mtunga amesema kuwa uamuzi huo utasaidia kubadilishana uzoefu katika utoaji huduma bora kwenye mahoteli ambapo tayari wanachama wapatao 50mkoani Mwanza tayari wamejiandikisha kuunda ushirika unaoitwa LZHA.
Ameongeza kuwa kutokana na kuwepo changamoto kubwa ya ushindani katika utoaji huduma kwenye mahoteli nchini hasa linapokuja suala la utalii, ambapo mabadiliko ya kiuchumi katika sekta ya utalii na biashara sanjari na kutoa huduma bora kwa wateja yanahitajika imewalazimu kuunda umoja huo utakaojulikana kama Lake Zone Hoteliers Associatian (LZHA) ili kudhibiti mahoteli yatakayo kuwa yakitoa huduma chini ya kiwango tofauti na hadhi ya leseni zao.
Pia umoja huo umeazimia kuweka mfumo wa kupeana taarifa na kuwabaini baadhi ya watumishi ambao si waaminifu na wenye tabia ya wizi kwa waajiri wao na wateja ambao huacha kazi na kukimbilia kwenye mahoteli mengine hata kuweka taswira mbaya kwa hoteli za Mwanza.
Umoja huo pia umelenga kukabiliana na ushindani wa kibiashara na soko kutoka nchi wanachama wa Jumuiya Afrika mashariki na kuitikia sera ya serikali ya kukuza utalii kwa kutoa huduma zenye viwango vya kimataifa ili kuwavutia watalii wanaofika Jijini Mwanza.
Suala la Miundo mbinu hasa ya barabara limekuwa hoja ya msingi ambalo watalii wamekuwa wakililalamikia.
Naye Gloria Munhambo Afisa Mwandamizi wa Bodi ya Utalii Tanzania Kanda ya Ziwa amelipongeza azimio la kuundwa kwa umoja huo na kutoa ushauri wa kutumia Ofisi za kituo cha utalii kilichopo Jijini Mwanza kwa ajili ya kupata taarifa za vivutio mbalimbali vya utalii kanda ya ziwa ili viwafae watalii wanaozuru Mwanza na pia akisisistiza suala la Menejimenti za mahoteli kutoa nafasi za mafunzo ya kujiendeleza kwa wahudumu wao.
Umoja huo utazinduliwa Aprli 14 mwaka huu katika uwanja wa Nyamagana na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyarandu.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.