Mwenyekiti wa EAISA na Kamishina wa Bima wa Uganda, Alhaj Ibrahim Lubega Kaddunabbi akifafanua jambo mbele ya waancdishi wa habari (hawapo pichani). |
Waratibu wa kikao hicho kikazi zaidi. |
WAKATI upatikanaji wa huduma ya Afya kupitia Mfuko
wa Bima unaonekana kusuasua hapa nchini na wananchi wengi kusita kujiunga na
mfuko huo kutokana na adha na usumbufu wanaoupata kwenye Idara a Afya pindi wanapohitaji
kupatiwa matibabu wakiwa na Kadi za Bima ya Afya, hali ni tofauti kwa nchi za
zingine zilizopo Jumuia ya Afrika Mashariki.
Akizungumza wakati wa kupitisha uamuzi huo Kamishina
wa Mamlaka ya Bima nchini Tanzania Israel Kamuzora alisema kuwa bado zipo
kasoro katika huduma inayotolewa kupitia Mfuko wa Bima ya Afya nchini kuonekana
kusuasua kutokana na wataalamu wa Idara za Afya za serikali na binafsi
kushindwa kutoa kipaumbele kwa wananchi walio na Kadi kupatiwa matibabu sawa na
watu wengine wanaolipia gharama.
“Mfuko huu hapa nchini umeonekana kama vile watu
waliojiunga kama vile ni msaada wakati katika mataifa mengine ya Ulaya, Amerika
na Asia na baadhi Barani Afrika bila kuwa na Kadi ya Bima hupatiwi matibabu na
Daktari au Mtaalamu lakini hapa kwetu wataalamu wanauliza kuwa analipia gharama
ukijibu ndiyo unaanza kutibiwa na kudai una kadi unaelezwa subiri kwanza hili
siyo sawa.”alisema.
Kamishna Kamuzora alisema kwamba bado serikali
inatakiwa kutoa elimu kwa wataalamu na viongozi wa Hospitali, Vituo vya Afya na
Zahanati kwamba wananchi wenye Kadi za Mfuko wa Bima ya Afya wapatiwe matibabu
bila kujali kuwa na fedha tasilimu huku
pia ikidaiwa kuwa wanachama wengi wa mfuko huo hulalamikia usumbufu kwa
kuelezwa na wataalamu wa Idara ya Afya baadhi ya vipimo havilipiwi na mfuko
huo.
“Nchi zilizoendelea ukienda kwa Daktari na pesa
anaweza kukukataa kukupatia matibabu kwa kuwa anatambua kuwa hutoweza kumlipa
lakini ukiwa na Kadi atachangamka kukupatia huduma ya matibabu mara moja (First Class) kwa kutambua kuwa Kampuni ya Bima wanao uwezo wa kumlipa
gharama za kutibu kutokujua kwetu isiwe ndiyo utaratibu, hivyo elimu iendelee
kutolewa kwani sasa imeanza kueleweka” alisisitiza.
Kamzora aliongeza kuwa kwa sasa hapa nchini wananchi
wameanza kuchangamkia zaidi wakiwemo walimu ambao awali waliweka mgomo na
kukataa kukatwa mishahara yao ili kuchangia mfuko huo lakini hali ni tofauti
kwa sasa wengi wao wanaisifia na kuwahamasisha wengine na wananchi kujiunga na
mfuko huo lakini leo ukijaribu kuigusa kuwaondolea Bima ya Afya wengi wao
watagoma kutokana na kuelewa faida zake.
“Japo itachukua muda kwani tumeelewa tuliko toka na
hata kwenye Hospitali zetu wameanza kulitambua hilo lakini kikubwa zaidi ni
kuhakikisha elimu inazidi kutolewa na kuwafikia walengwa ili kusaidia wengi
kujiunga na mfuko huo wa Bima ya afya ili kupatiwa matibabu bila kunyanyaswa na
itafikia wakati hata hao wa kulipia gharama kwa fedha tasilimu watapata
usumbufu kutokana na Teknolojia”alisema Kamishna Kamzora.
Naye Jonathan Gatera ambaye ni Mwakirishi wa Gavana
wa Benki Kuu ya Rwanda alisema kwamba kwa serikali ya nchi ya Rwanda katika utoaji wa huduma ya Afya
kwa wananchi wake inazingatia wale walio na Kadi za Bima ya Afya na serikali imekuwa
ikihamasisha kwa kutoa elimu na asilimia kubwa wamejiunga na hutumia kupatiwa
matibabu mpango ambao umekuwa na mafanikio makubwa.
Mjumbe kutoa Kenya, Agnes Ndirangu ambaye
alimwakirisha Kamishna wa Bima wa nchini hiyo alisema kwamba Taifa hilo lina
kitengo maalumu cha kukusanya na kusikiliza malalamiko na changamoto mbalimbali
za Bima kutoka kwa wananchi ikiwemo Bima ya Afya ili kuboresha meanzisha
upatikanaji wa huduma bora.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wakuu wa Mamlaka za
Bima kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki Alhaj Ibrahim Lubega Kaddunabbi
alisema kuwa kikao hicho kilichoketi kwa siku mbili kilikuwa kujadili na
kupitisha maamuzi ya kuifanya Bima itumike kwa nchi zote wanachama wa Jumuiya
hiyo badala ya kila nchi kuwa na utaratibu wake wa utohaji huduma za Bima na
Viwango tofauti.
Alhaji Kaddunabbi ambaye ni Kamishna wa Bima wa
nchini Uganda alisema kwamba lengo la kikao hicho ni kuhakikisha Makampuni ya
Bima kushirikiana kwa pamoja kutoa huduma za Bima kwa pamoja badala ya kuwa na
Bima ya kila nchi jambo ambalo limekuwa kero na adha kubwa kwa wananchi
wanapoamua kutembelea nchi nyingine na kupata usumbufu wa kukata Bima upya ili
kuruhusiwa kuingia nchi nyingine.
“Kwa sasa ukiwa na gari lako na BIMA ulilokata nchini
Uganda ukienda nchini za Kenya, Tanzania, Rwanda na Burundi haitambuliki, tunalazimika kukata Bima tofauti, huu ni usumbufu ni vyema tukawa na utaratibu wa Makampuni na Mashirika
ya Bima kutoa huduma hiyo na kukubalika na nchi zote wanachama, hata ukitokea umepata ajali basi upatiwe matibabu ukiwa nchi nyingine kwa Bima uliyokata nchi nyingine” alisema.
Katibu wa Wakuu wa Mamlaka za Bima (East Afrika
Insurance Superviors Assocciation) kwa kifupi inafahamika EAISA, Venant Kamana
kutoka nchini Burundi alisema kwamba Makampuni hayo ya utoaji wa Bima endapo
yatafikia uamuzi wa kutoa huduma za pamoja kwa kushirikiana haitoathiriwa na uthamani wa fedha kwani Mabenki yaliyopo kila nchi yatatumika viwango vinavyojulikana kimataifa katika
ubadilishaji wa fedha toka nchi moja hadi nchi nyingine za Jumuiya.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.