NA PETER FABIAN.
MWANZA.
VIONGOZI na wananchama wa CCM wenye uwezo wa
kifedha, wametakiwa kuacha uchoyo na ubinafsi kwa kujitokeza kukichangia chama na jumuiya zake katika kukuza mitaji na kuwajengea uwezo wananchi ili kukisaidia chama kuvuka malengo ya ilani ya uchaguzi 2010-2015.
Kauli hiyo ilitolewa na Mjumbe mstaafu wa Baraza Kuu
la UVCCM taifa wa mkoa wa Mwanza, Barnabas Mathayo, mwishoni mwa wiki wakati akizindua
mashina matano ya UVCCM Katani Kirumba, wilayani Ilemela na kusaidia vikundi
vya wajasiriamali na Umoja wa Vijana (UVCCM) wilaya ya Ilemela, msaada wenye
thamani ya sh milioni 15.9
Msaada huo ni pamoja na pikipiki sita zenye thamani
ya sh Milioni 12 (kwa UVCCM) Wilaya ya Ilemela na fedha taslimu sh milioni 3.9 aliyakabidhi
viongozi wa mashina matano ya UVCCM pamoja na vikundi vitatu vya akina mama na
vijana wajasiriamali wa Kata ya Kirumba wilayani humo.
“ Msaada huu siyo kwa nia ya mimi kugombea nafasi ya
Ubunge au Udiwani na si kwamba ninavyo vingi bali ni moyo wa kujitolea
kukisaidia Chama chetu ninacho kipenda, tatizo la wana CCM wengi wetu wenye
uwezo ni wachoyo na wagumu wa kukisaidia Chama.” Alieleza Mathayo.
Mjumbe huyo mstaafu akiwaomba wana CCM wengine wenye
uwezo wajitolee kukisaidia Chama na jumuia zake na hasa katika kipindi hiki cha
kuelekea katika chaguzi za Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ili
CCM iweze kurejeshe majimbo na Kata ilizopoteza , alidai kuwa wana CCM wafanye
kazi kwa pamoja na kuacha porojo kama za wabunge wa Chadema wa Ilemela na
Nyamagana.
“ Wazee mkisikia vijana tunajitolea kukisaidia Chama
msinune na kulalama kuwa fulani anataka kugombea Ubunge au Udiwani, ukitoka CCM
hujafanya kitu cha kukumbukwa utachekwa, acheni ubinafsi, uchoyo na kubeza watu
wanaojitolea kukisaidia na kukiimarisha Chama, tuungeni mkono ili tukomboe
majimbo ya Ilemela na Nyamagana.” Alieleza na kushangiliwa na umati mkubwa
wawatu.
Mathayo alianza mwaka 2010 kabla ya kustaafu wadhifa
huo alipomwaga pikipiki 25 zenye thamani ya sh milioni 37.5 kwa UVCCM wilaya za
Ukerewe, Misungwi, Kwimba, Magu na Sengerema (kila wilaya tano tano) na Januari
mwaka huu alichangisha zaidi ya sh milioni 10.7 kusaidia UVCCM kata ya Mahina
wilayani Nyamagana.
Akipokea msaada huo Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mwanza Sixbert Ruben na kumpongeza Mathayo, alisema siasa ni uchumi na maisha, alichokifanya kisiwe chokochoko na maneno kutoka kwa baadhi ya wana CCM wanaodhani uongozi wa Chama ni kwa ajili ya maslahi yao binafsi, yanakatisha tamaa ya watu kujitolea kukisaidia Chama.
Mwenyekiti Reuben aliwataka vijana wasikubali kutumiwa na baadhi ya wana siasa wenye uchu wa madaraka ambao wanawatumia kama makalai ya kubeba zege ambao wakipata uongozi hawarudi kuwasaidia na kukumbuka kuwasaidia kama Matahayo anavyofanya toka alipokuwa kiongozi na sasa mwana chama wa kawaida.
Naye Mwenyekiti wa UVCCM wilayani Ilemela Hery James, akipokea msaada wa Pikipiki za vijana wake alisema kwamba nyenzo hizo ambazo ni mkombozi wa vijana kwa tatizo la ajira, zitatumika ipasavyo kujiletea maendeleo na kuimarisha Jumuia hiyo ikiwa pamoja na kuwahamasisha vijana wengine wanaokimbilia maandamano na vurugu za wapinzani, warudi CCM.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.