ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Tuesday, March 25, 2014

AFRICAN BARRICK GOLD MINING WADHAMINI TIBA YA UPASUAJI BURE KWA KICHWA, MGONGO NA MISHIPA YA FAHAMU KATIKA HOSPITALI YA BUGANDO MWANZA.

Daktari Bingwa wa Ubongo, Mgongo na mishipa ya fahamu Dr. Othman W. Kiloloma kutoka hospitali ya Muhimbili amesema kuwa timu ya madaktari saba imewasili kutoka Muhimbili  ikiwa na daktari bingwa 1 wa usingizi wakiwa na vifaa vyote muhimu ili kuungana na madaktari Bingwa wa upasuaji Bugando kwaajili ya kuweka kambi ya tiba mkoani Mwanza.  
Dr. Othman W. Kiloloma ameongeza kuwa dhana ya kuweka kambi Mwanza imekuja ikiwa ni hatua ya kujaribu kupunguza vifo na usumbufu unaowakumba watu wenye maradhi hayo pindi wanapohitaji tiba ambapo wengi wameshindwa kupata huduma mapema kutokana na kushindwa kuzimudu gharama kwa magonjwa hayo ambayo kila kukicha idadi ya watu wenye matatizo ya Ubongo na Mishipa ya fahamu inaongezeka. Ameishukuru sana African Barrick Gold kwa kudhamini mpango huo. 
Kama upasuaji utahitaji kufanyika masaa 24 tuko tayari kwa hilo, nia ni kuwahudumia wale wote watakao jiandikisha kuwa wanamatatizo na wanahitaji tiba.
Mgeni rasmi wa Uzinduzi wa mpango huo wa tiba, Mstahiki Meya wa jiji la Mwanza ambaye pia ni diwani wa Kata ya Mkolani Mhe. Stanslaus Mabula amewataka wananchi wote wenye matatizo kujitokeza kwani ni nadra sana kupata tiba kama hiyo bure bila malipo, naye akisema kuwa ni mmoja katiya waathirika wa matatizo hayo ambapo ni hivi karibuni tu! naye ametoka kufanyiwa upasuaji wa matatizo ya mgongo katika Hospitali ya Rufaa ya Taifa ya Muhimbili. Pia amewashukuru sana Madaktari hao bingwa kwa kuliona tatizo na kulitafutia ufumbuzi sambamba na kuwashukuru Kampuni ya ABG waliodhamini mpango huo. 
Sehemu ya madaktari Bingwa watakao husika na zoezi hilo la tiba itakayo tolewa katika Hospitali ya Rufaa Bugando.
"Mpaka sasa tumeandaa wagonjwa 33, ambao wanahitaji oparesheni, leo kuna wagonjwa 12 ambao wamepangiwa oparesheni, watoto ni wa8 na watu wazima ni wa4". Miongoni mwao kuna wagonjwa wenye matatizo makubwa wawili, mmoja anausaa kwenye ubongo, mwingine damu imeingia kichwani" alisema Dr. Gerlard ambaye ni Bingwa wa upasuaji kutoka Hospitali ya Rufaa Bugando (BMC ambao ni wenyeji). 
Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Bugando (BMC) Prof. Charles Majinge, Meneja Mahusiano na jamii wa Kampuni ya ABG  Steve Kisake, mgeni rasmi Mstahiki Meya wa jiji la Mwanza Stanslaus Mabula na kulia ni mmoja kati ya madaktari bingwa wakisikiliza maelezo na ufafanuzi wa jinsi zoezi litakavyo fanyika.
Ni mmoja kati ya akinamama waliojitokeza kwa kuwaleta watoto wao kufanyiwa upasuaji wa mishipa na mgongo.
Ni uvimbe wa mmoja kati ya watoto wanao subiri tiba. Kila la kheri Mwenyezi Mungu awaongoze na mfanikishe kwa wale wote wanaopata tiba na wale wanao subiri tiba.
Ni mtoto ambaye anasubiri kupatiwa tiba kwa tatizo la kichwa kujaa maji kwa tiba ya bure itakayo tolewa na madaktari bingwa wa upasuaji toka MOI na BMC akiwa katika ward ya Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza. Kila la kheri Mwenyezi Mungu awaongoze na mfanikishe kwa wale wote wanaopata tiba na wale wanao subiri tiba.
Tatizo la kichwa.
Tatizo la uvimbe kwenye mgongo.
Baadhi ya akinamama wakiwa na watoto wao katika ward wakisubiri kupatiwa tiba kwa matatizo mbalimbali yanayo hitaji upasuaji unaofanywa na madaktari bingwa wa upasuaji toka MOI wakishirikiana na mabigwa wa upasuaji wa BMC, ni katika Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza.
Dr. Othman W. Kiloloma akitoa ufafanuzi katika kusanyiko la uzinduzi wa tiba ya bure kwa maradhi ya Kichwa, Mgongo na Mishipa uliofanyika ukumbi wa mikutano kitengo cha Satatani Bugando jijini Mwanza.

HALI IKIWA TETE KANDA YA ZIWA NAKO WODI ZA MOI ZIMEFURIKA.
MWANZA.
LICHA ya kuwa na Madaktari bingwa wa upasuaji wa kichwa wasiozidi watano tu nchini, wodi za kitengo cha upasuaji wa kichwa na mifupa cha Hospitali ya Rufaa ya Taifa Mhimbili (MOI) jijini Dar es Salaam, zimefurika wagonjwa.

Mratibu wa jopo la madakatari bingwa saba wa MOI walioweka kambi maalum ya matibabu ya mgongo na upasuaji kichwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC) jijini Mwanza, Dkt Othman Kiloloma, amesema hali hiyo ni moja ya changamoto kubwa inayokikabili kitengo hicho.

Amedai, kutokana na kusubiri matibabu hayo kwa muda mrefu, baadhi ya wagonjwa wa nje ya Dar es salaam huishiwa fedha za kujikimu na hata nauli, hivyo Madkatari hao kulazimika kuwasaidiwa nauli za kuwarudisha makwao.

Dkt Kiloloma alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi kabla ya uzinduzi wa Matibabu ya mgongo na upasuaji kichwa unaofanywa na wataalam hao hapa, kwa kushirikiana na madakatari bingwa wa BMC.  

Matibabu hayo yanayotolewa bure kwa ufadhili wa kampuni ya African Barrick Gold katika hospitali ya Bugando, yalianza juzi (Machi 24) na yataendelea hadi Machi 28 mwaka huu ambapo wagonjwa zaidi 33 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji mkubwa wa vichwa na kutibiwa migongo.

“Wodi zetu zimejaa wagonjwa wetu wanasubiri kwa muda mrefu, ukituletea mgonjwa atalala wapi wakati wamejaa hadi kwenye makorido lakini hatuwezi kuwafukuza.” Alieleza Dkt Kiloloma wakati akionyesha picha za wagonjwa waliolazwa MOI, walivyofurika.

Alisema kupeleka wagonjwa wa aina hiyo Dar ni gharama kubwa hivyo ndiyo maana jopo hilo kwa ufadhili wa kampuni hiyo ya uchimbaji madini nchini, limeweka kambi Bugando ili kuwasaidia wagonjwa waliopo kanda ya ziwa ambao ingebidi wapelekwe Mhimbili au nje ya nchi kwa matibabu hayo.

“Kati ya Madaktari saba tuliotoka MOI kuja Mwanza kuungana na wenetu wa Bugando kusaidia wangonjwa wa Kanda hii ya ziwa, mabingwa wa upasuaji wa kichwa tupo watatu. Tanzania nzima ina mabingwa wa Upasuaji kichwa wasiozidi watano, hivyo wawili ndio wamebaki Dar.” Alieleza bingwa huyo na kudai upungufu wa wataalamu hao ni changamoto kubwa inayolikabili taifa.

Alieleza kwamba kukamilika kwa jengo la ghorofa nane linalojengwa MOI kutasaidia kuondoa mlundikano wa wagonjwa ambao sasa wanakosa pa kulala licha ya wengine kuwa nje ya wodi wakisubiri matibabu.  

“Tunapasua wagonjwa 600 kwa mwezi lakini kutokana na kusubiri matibabu kwa muda mrefu kidogo, baadhi au wauguzi wao huishiwa fedha za kujikimu na kulazimika kuwasaidia nauli ya kurudi kwao, wengine (akina mama) hukuta waume zao walisha oa wanawake wengine.” Alidai.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.