Wahamiaji haramu zaidi ya Elfu kumi na mbili (12,000) wamekamatwa katika Oparesheni ya kuwaondoa wahamiaji haramu hapa nchini, katika awamu ya kwanza ya Oparesheni hiyo ambayo imefikia tamati wiki iliyopita, huku ikielezwa kwamba oparesheni hiyo imefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Hayo yalibainishwa jana Mkoani Mwanza na Kamanda msaidizi wa Oparesheni hiyo iliyofahamika kwa jina la Oparesheni Kimbuka, Naibu Kamishna wa jeshi la polisi nchini Simon Siro.
Kamanda Siro alisema kwamba Oparesheni hiyo imefanikiwa kwa mafanikio makubwa na kubainisha kwamba imetekelezwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo kwa kuzingatia haki za binadamu kulingana na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Jumla ya wahamiaji haramu waliokamatwa katika Oparesheni Kimbuka ni 12,704 ambapo kati ya hao Wanyarwanda ni 3,448 Waganda 2,496 Warundi 6,125 Wakongo 589 Wasomalia 44 Myemeni mmoja pamoja na Mhindi mmoja.
Alieza kwamba katika Oparesheni hiyo mbali ya kuwakamata wahamiaji haramu, pia wamekamata silaha mbalimbali zilizokuwa zikitumika katika uharifu hapa nchini, pamoja na waharifu 212 wanaosadikiwa kuwa majambazi sanjari na majangiri 23 waliokutwa na nyara mbalimbali za serikali pamoja na mifugo ipatayo elfu nane mia mbili ishirini na sita (8226).
Katika Oparesheni hiyo Silaha mbalimbali 61 zilikamatwa, risasi 665, mabomu ya kutupwa kwa mikopo 10, magogo 86, mbao 2,105 pamoja na vitu vingine mbalimbali ambavyo vilikuwa vikimilikiwa na wahamiaji hao haramau hapa nchini huku Kamanda Siro akiongeza kuwa Oparesheni kimbuka imevijumuisha vyombo vyote vya dola ikiwemo TAKUKURU na hivyo kukanusha suala la uwepo wa rushwa katika Oparesheni hiyo.
Alisema wahamiaji haramu waliokamatwa wamebainika kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Burundi, Rwanda, Uganda, Congo, Somalia, Yemen pamoja na India huku Oparesheni hiyo ikibaini Mikoa mitatu ambayo inaongoza kwa idadi kubwa ya wakimbizi haramu kuwa ni Geita ambo ni wa tatu, Mkoa wa Kigoma ambao ni wa pili pamoja na Mkoa wa Kagera ambao unaoongoza.
Aidha kamanda Siro alibainisha kwamba katika Oparesheni hiyo wamekutana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa vitambulisho vya uraia, wananchi kuwataja watu ambao si wahamiaji haramu kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo chuki miongoni mwa wanafamilia sanjari na baadhi ya viongozi wa serikali za vijiji na vitongoji kuwaficha wahamiaji haramu hali inayopelekea kuwa na idadi kubwa ya wahamiaji haramu hapa nchini.
Nae Mrakibu Mwandamizi wa uhamiaji Petro Malima alieza kwamba Oparesheni hiyo haikuwahusu wakimbizi walioko hapa nchini tofauti na taarifa zilizotolewa hapo awali, kwa kuwa wakimbizi wao wana vibali halali vya kuishi hapa nchini.`
Alifafanua kwamba Oparesheni hiyo imewagusa baadhi ya raia ambao hawakuwa raia wa Tanzania ambao walikuwa wakidhania kuwa wao ni raia halali wa Tanzania kwa kuwa walikuwa na hati mbalimbali za Tanzania zikiwemo kadi za kupigia kura, vyeti vya kuzaliwa pamoja na kadi za vyama vya siasa jambo ambalo afisa huyo wa uhamiaji alilitolea ufafanuzi kwamba raia halali wa Tanzania hapatikani kwa kuwa na vitu hivyo .
Aidha alieza kwamba raia halali wa Tanzania hupatikana kwa mjibu wa sheria ya uhamiaji huku akikanusha ya kwamba hakuna raia yeyote wa kigeni aliekuwa na hati halali za kuishi hapa nchini aliefukuzwa ama kurejeshwa kwao.
Baada ya awamu ya kwanza ya Oparesheni kimbunga kukamilika ijumaa iliyopita ya tarehe 20 mwezi huu, awamu ya pili ya Oparesheni hiyo ilianza jumapili ya tarehe 22 mwezi Septemba hadi tarehe 20 mwezi Octoba mwaka huu, huku kuendelea ama kufikia tamati kwa Oparesheni hiyo kukitegemea hali ya wakimbizi haramu hapa nchini itakavyokuwa, ambapo wananchi wametakiwa kutoa ushirikiano wao ili kuwezesha zoezi hilo kufanikiwa.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.