Wanokwenda Nigeria Airtel Rising Stars watajwa |
Dar es Salaam, Jumapili 8 Septemba 2013… Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) leo limetangaza kikosi cha wachezaji 32 wanaosafiri kwenda Lagos, Nigeria wiki ijayo kushiriki mashindano ya kimataifa kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars.
Afisa maendeleo wa TFF Salum Madadi amewataja wachezaji wanaounda timu ya wasichana kuwa ni walinda mlango Najihati Abbasi kutoka mkoa wa kisoka wa Kinondoni na Niwale Halfan (Temeke). Wengine ni Stumai Abdallah, Anastazia Anthony, Tatu Iddi (Kinondoni), Vumilia Maharifa, Donisia Daniel, Maimuna Hamisii na Amina Ally (Ilala).
Aliwataja wachezaji wengine kuwa ni Shelda Boniphace, Rehema Yahya na Anna Hebron (Kinondoni), Khadija Hiza (Tanga), Neema Paul, Amina Ramadhani na Latifa Ahmed (Temeke).
Wanaounda kikosi cha wavulana ni Arafat Mussa (Ilala) Aziz Hashim (Ilala), Rothan Mkanwa na Petro Mgaya (Morogoro), Bruno Shayo (Mwanza), Thomas Chideka (Temeke), George Chota (Morogoro), Luseke Kiggi (Mwanza) na Ramadhani Kondo (Morogoro).
Wengine ni Martin Luseke (Mwanza), Omary Hussein (Ilala), Joseph Mushi (Ilala), Miraj Kwangaya na Salum Issa (Temeke), Optanus Lupekenya (Morogoro) na Athanas Mdam (Mwanza).
Mashindano haya ya vijana ya kimataifa yanafanyika kwa mara ya pili mwaka baada ya yale ya uzinduzi kufanyika jijini Nairobi mwaka jana ambapo Tanzania iliwakilishwa na timu ya wavulana pekee ambayo hata hivyo ilitolewa katika hatua za awali huku timu ya Niger ikitawazwa kuwa mabingwa.
Airtel imeanzisha mashindano haya ya vijana barani Afrika kwa nia ya kusaidia upatikanaji wa vijana wenye vipaji vya soka kuanzia ngazi ya chini kabisa hadi ngazi ya Taifa. Airtel Rising Stars inatoa fursa kwa vijana kudhihirisha uwezo wao kwa makocha wa Taifa na kimataifa na kuweza kujiendeleza zaidi kisoka.
Hivi sasa Airtel Rising Stars ni moja ya matukio muhimu ya kisoka kwenye kalenda ya Shirikisho la Mpira wa miguu nchini (TFF). Huanzia katika hatua ya usajili ikifuatiwa na mechi za mtoano ili kupata wachezaji nyota wa kuunda timu za mikoa ambazo huchuana katika ngazi ya Taifa.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.