Akizungumza mjini hapa, Wenje alisema baada ya kumaliza mahojiano na polisi alizuiwa kusafiri kipindi hiki, huku akitakiwa kufika polisi jana saa 3:00 asubuhi.
Taarifa zinaeleza kuwa huenda akapandishwa kizimbani kwa makosa hayo.
“Nimezuiliwa kusafiri kwa sasa, wamenitaka kurudi polisi Alhamisi (leo), kwenye mahojiano yao walidai nilifanya maandamano bila kibali, ikiwamo kuwaita polisi mbwa,” alisema Wenje na kuongeza:
“Lakini ukweli niliwaeleza kuwa kauli yangu ilikuwa ikiwaasa wananchi kuhakikisha tunaandamana kwa amani, tusiruhusu maisha ya wanachama au mtu yeyote yapotee kwa kuumwa na mbwa wa polisi ambao walikuwa nao.”
Wenje alikamatwa juzi (jumatatu) saa 5:18 asubuhi na kuhojiwa hadi saa 10:15 alasiri, kwa kile kinachodaiwa kuongoza maandamano yasiyo na kibali.
Pia, anadaiwa kutoa lugha ya uchochezi hali ambayo ilisababisha vurugu na polisi kutumia mabomu ya machozi kusambaza wafuasi wa chama chake.
Kamanda wa Polisi Mkoa Mwanza, Ernest Mangu, licha ya kukiri kumhoji mbunge huyo, lakini hakutaka kuweka bayana zaidi suala la kumzuia kusafiri.
“Nipo kwenye kikao kwa hiyo siwezi kuzungumzia suala hilo kwa undani kuhusu kuzuiwa kusafiri kwa mbunge huyo,” alisema Mangu.
Licha ya Wenje, watu wengine wawili wanashikiliwa na polisi tangu juzi na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa makosa ya kuandamana bila kibali na kusababisha vurugu.
Juzi, polisi walitawanya maandamano ya wanachama wa Chadema kwa mabomu ya machozi.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.