ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, August 7, 2013

MBUNGE WA RORYA AWAPIGA TAFU VIJANA WA FURAHISHA KWA KUWABORESHEA KIWANJA CHAO

Uwanja wa Furahisha kama unavyoonekana mara baada ya Mbunge wa Jimbo la Rorya Lameck Airo (La-Kairo) kuusawazisha na kuukwangua kwa Greda ili utumike vyema na kwaurahisi kukuza vipaji vya watoto wilaya ya Ilemela Kirumba jijini Mwanza.

Timu A ya Vijana wa chini ya umri wa miaka 11 iliyoko Kirumba jijini Mwanza ikifanya mazoezi aubuhi ya leo ambapo vilevile vijana hawa walizungumza na blogu hii kuisifia hatua ya Mbunge wa Jimbo la Rorya Lameck Airo (La-Kairo) kuusawazisha na kuukwangua kwa Greda uwanja  maarufu wa michezo na mikutano ya hadhara wa Furahisha uliopo Kirumba Wilayani Ilemela.


Na Peter Fabian.
VIJANA na watoto walio chini ya umri miaka 17 wa Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela wamepongeza na kuushukuru uamuzi wa Mbunge wa Jimbo la Rorya Lameck Airo (La-Kairo) kwa kuusawazisha na kuukwangua kwa Greda uwanja  maarufu wa michezo na mikutano ya hadhara wa Furahisha uliopo Kirumba Wilayani Ilemela.

Wakionekana kujawa na furaha na kuzungumza kwa nyakati tofauti baada ya kumalizika kazi ya kuusawazisha uwanja huo iliyofanywa na Mbunge Airo kwenye uwanja huo wa Furahisha walisema kwamba kitendo hicho ni cha kiuungwana na kimewajali vijana na watoto kupata sehemu yenye ubora wa kuchezea na kuwapatia fursa ya kuonyesha vipaji vyao baada ya kutoka shuleni nyakati za jioni.

Mazoezi kwa timu B asubuhi ya leo.

“Huyu ni Mbunge wa Jimbo la Rorya lakini tulienda kumuomba kuusawazisha uwanja huo ili tupate pa kuchezea naye ameguswa na sisi kwa vile ni mtu wa watu na ameona ni vyema nasi tukapata kucheza kwenye mazingira yaliyo na ubora akizingatia mahusiano ya Jamii kutokana na kuwa mwakilishi wa wananchi wa Jimbo lake lakini pia anapofanyia biashara yake” alisema kijana Almasi Juma mkazi wa Kirumba.

Mbunge Airo ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya La-Kairo Investiment ya Jijini Mwanza inayojishughulisha na uuzaji na usambazaji wa bidhaa mbalimbali pamoja na kumiliki Hoteli amekuwa ni chachu ya kusaidia Kata ya Kirumba ambapo ndipo mahali alipowekeza biashara yake na kuonyesha ungwana kwa jamii inayomzunguka ikiwemo ya vijana na watoto hao.

Naye Jumanne maarufu kwa jina la J4 mkazi wa kirumba alisema kwamba Mbunge Airo ni mtu ambaye anapenda michezo si kwamba ni mwakirishi wa wananchi na wapiga kura wake tu wa Jimboni mwake bali ni kwa wananchi walio wengi na amekuwa akihamasika kushiriki katika mkakati wa kuibua vipaji ndani na nje ya nchi hususani nchi jirani ya Kenya kwa kuwaleta vijana wa shule kujifunza Mwanza.

“Huyu  ni Jembe na sasa amekuwa akitaka kuona vijana na watoto kupitia timu za mitaani na zile za Academy zikifanya vizuri kwa kuibua na kuviendeleza vipaji ikiwa ni moja ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM naye akiwa Mbunge anayetokana na Chama hicho tawala, kwa kweli yupo tayari kutusaidia kuhakikisha timu za Toto Afrika na Pamba za Mwanza zinafanya vizuri na kurudi kucheza Ligi Kuu ya Vodacom”alisema J4
Kwa upande wake Mbunge Airo alikiri kufuatwa na timu za vijana wa mitaa ya Vuka, Alfani na Penda wakimuomba kupeleka Greda lake kusawazisha uwanja huo, kweli niliwaeleza wawe na subira kidogo na wawasiliane pia na uongozi wa Manispaa ya Ilemela kwa kuwa ndiyo wamiliki wa eneo hilo ili kupata Baraka zake kabla ya kutekeleza ombi lao.

“Baada ya kupata ruksa ya Manispaa kutoka kwa Meya wa Manispaa Mh. Henry Matata nilianza kuusawazisha uwanja huo ili vijana na watoto wetu waendelee na michezo hasa mpira wa miguu na ukifika uwanjani hapo jioni utashuhudia vijana wengi wakichuana vikali na utaonao vipaji vya kweli”alisema Airo.

Mbunge huyo alitoa wito kwa viongozi wa serikali za mitaa na kata kuwahudumia wananchi na kuondoa kero zao zikiwemo za vijana na watoto huku wakihakikisha maeneo ya viwanja vya wazi yanatengwa na kuendelezwa badala ya kuwaachia watu wanaovamia na kufanya ujenzi wa majumba na kuwanyima vijana sehemu ya kuchezea na kuonyesha vipaji vyao  jambo ambalo hupelekea kulaumiwa serikali.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.