ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, August 19, 2013

MAANDAMO KUMNG'OA MEYA KUFANYIKA ASUBUHI HII MWANZA

Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Freeman Mbowe akinyanyua bango linalosomeka: 'Ona Chadema karibu mweshimiwa mkombozi wa haki zetu Mwanza', 'NO Matata' (akimaanisha kukataliwa kwa Meya Henry Matata wawilaya ya Ilemela). Ni picha ya mwishoni mwa wiki katika mkutano wa CHADEMA kujadili Rasimu ya Katiba uliofanyika uwanja wa Magomeni Kirumba wilaya ya Ilemela jijini Mwanza.
HABARI
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), manispaa ya Ilemela, mkoani Mwanza, kimeitisha maandamano makubwa ya amani leo kwa ajili ya kushinikiza kung’olewa kwa meya wa manispaa hiyo, Henry Matata, anayedaiwa kuchaguliwa kinyume cha sheria.

Akitangaza maandamano hayo mbele ya waandishi wa habari jijini hapa jana, Ofisa Operesheni wa CHADEMA Kanda ya Ziwa Magharibi, Tungaraza Njugu, alisema yataungwa mkono na maelfu ya wananchi wa Nyamagana.

Alisema maandamano hayo yataanzia Buzuruga saa 4:00 asubuhi kisha kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo, katika uwanja wa Furahisha, na kwamba unahitajika kufanyika upya uchaguzi wa meya na naibu wake.
Tungaraza aliyeongozana na ofisa wa chama kanda hiyo, Meshack Mikael, pamoja na katibu wa mbunge wa Ilemela, Laban Agrey, alisema maandamano hayo yanahusisha pia kupinga kufukuzwa kinyemela madiwani watatu wa chama hicho.

Madiwani waliofukuzwa na meya wa manispaa hiyo kinyume cha sheria ni Abubakar Kapera (Nyamanoro), Malietha Chenyenge (Ilemela) na Dany Kahungu wa kata ya Kirumba.

“CHADEMA tumeitisha maandamano makubwa hapo kwa lengo la kumkataa meya wa Ilemela na kushinikiza uchaguzi ufanyike upya.

“Matata amechaguliwa bila kukidhi akidi ya madiwani wa manispaa hiyo ambayo ni theluthi mbili ya madiwani wote 14, hivyo siyo meya.

“Lakini maandamano haya yatalenga pia kupinga Matata kuwafukuza madiwani wetu kinyemela. Sheria zinasema diwani atakosa sifa baada ya kutohudhuria mfululizo vikao vitatu vya Baraza la Madiwani, lakini Matata aliyechaguliwa kinyume cha sheria aliwafukuza ndani ya wiki moja baada ya kuchaguliwa,” alisema.

Alisema CHADEMA pamoja na wananchi wa Ilemela wanahitaji kufanyika upya kwa uchaguzi wa meya na naibu wake na kwamba kama kweli madiwani hao wamefukuzwa kihalali wapewe barua za kufukuzwa kwao na tume ya uchaguzi itangaze kata hizo kuwa wazi.

“Kuna taarifa zinaeleza kwamba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alishaandika barua ya kutengua uamuzi wa kufukuzwa madiwani hao na barua hiyo ‘imekaliwa’ na mkuu wa mkoa,”alisema.

Naye katibu wa Highness Kiwia, Laban Aggrey, kwa niaba ya mbunge huyo alisema kuwa maandamano hayo yataanzia Buzuruga kisha kupita barabara ya Nyerere, Mlango mmoja, Uhuru, Nkrumah, Balewa na kuishia uwanja wa Furahisha.
“Polisi wameshabariki kufanyika maandamano yetu, hivyo ofisi ya mbunge wa Ilemela inawasihi sana wananchi wajitokeze kwa wingi kuja kudai haki yao iliyoporwa kinyume cha sheria,” alisema.

Akizungumza na Tanzania Daima jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu, alisema maandamano hayo ya CHADEMA yameruhusiwa na jeshi lake.

“Haya maandamano tumeyaruhusu kabisa yafanyike, maana kama watu wanasema wanadai haki yao kwa nini tuwazuie? Tumewapangia maeneo ya kupita maandamano haya hadi huko Furahisha,” alisema Mangu.

Uchaguzi wa meya wa Ilemela uliofanyika Desemba mwaka jana, ulikiuka kanuni na sheria za halmashauri, ambapo akidi ya wajumbe iliyokuwa ikihitajika kwa ajili ya meya kupigiwa kura ni madiwani tisa, lakini ni madiwani sita tu ndiyo waliopiga kura.

Katika uchaguzi huo uliohudhuriwa na mkuu wa wilaya hiyo, Amina Masenza (DC), pamoja na mwanasheria wa jiji la Mwanza, Savela Manzi, aliyesimamia uchaguzi huo kwa upande wa mambo ya sheria, Matata alitangazwa kuwa meya baada ya kuchaguliwa na madiwani wasiokidhi theluthi mbili.

Madiwani waliopiga kura kumchagua Matata na naibu wake (Dede Swila wa CCM), walikuwa wanne wa CCM, mmoja wa CUF ambaye ni mbunge wa viti maalumu, Mkiwa Kimwanga, na Matata mwenyewe aliyefukuzwa uanachama wa CHADEMA.

Matata alichaguliwa wakati suala lake la kufukuzwa uanachama ndani ya CHADEMA likiwa bado linangojea uamuzi wa mahakama.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.