Na Peter Fabian
MWANZA.
HALMASHAURI ya Jiji la Mwanza imepiga marufuku na kuagiza
wamiliki wa maduka makubwa na madogo kuacha kupanga bidhaa zao nje ya maduka yao na kuwataka wamachinga
wote wanaofanya biashara kwenye njia za watembea kwa miguu kando ya barabara za
Kenyata na Nyerere kupisha maeneo hayo.
Agizo hilo limetolewa jana na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza
Halifa Hida kwa waandishi wa habari ofisini kwake, alisema kwamba hatua hiyo
inafuatia Jiji hilo kutoa muda wa miezi miwili ya kuwataka wafanyabiashara
wadogo (Machinga) kufanya biashara zao kwenye maeneo waliyotengewa badala ya
kuanza kuzagaa na kupanga bidhaa kiholela.
Mkurugenzi Hida alieleza kuwa kuanzia kesho wataanza
kutekeleza sheria ndogo namba 8 ya Mipango Miji ya mwaka 2007 na sheria ndogo
ya Usafi wa Mazingira ya mwaka 2010 pamoja na kuendelea kulinda na kulipatia
Jiji la Mwanza Hadhi ya Kimataifa itakayoleta
fursa mbalimbali za kiuchumi na kuendelea kuwanufaisha wananchi wake.
“Wananchi wetu kupitia sekta za Utalii,Biashara, Ujenzi wa
vitega Uchumi na Uwekezaji katika Jiji letu ili kutuingizia mapato na kuboreshwa
mazingira ya upatikanaji huduma kwa wananchi za kiwango cha kitaifa na
kimataifa likiwa na mwonekano wenye Hadhi kuendana na kasi ya ukuaji wake.
Hida alifafanua kuwa katika utekelezaji huo ambao
unaambatana na Mpango kazi unaozingatia suala la kuwapanga wamachinga ikiwa ni
mwendelezo ulioanza tangu mwaka 2007/2008 ili kufanikisha zoezi hili na
kuhakikisha Jiji linakuwa kwenye mpangilio mzuri na kila eneo la Mji linatumika
kama ilivyokusudiwa.
“Jiji tayari limeisha boresha maeneo ya yaliyotengwa kwa
ajili ya masoko ya wafanyabiashara wadogo (Machinga) kwa kuweka miundombinu
mwafaka ya vyoo, maji na vituo vya daladala lakini masoko hayo yamekuwa
hayatumiki na kutelekezwa jambo ambalo limewafanya vijana wengi kufanya
biashara kiholela katikati ya Mji”alisema.
Alieleza kuwa Jiji lake litaendelea
kubaini na kuyaendeleza maeneo yaliyoruhusiwa kwa wafanyabiashara wadogo,
kuainisha maeneo yasiyoruhusiwa kwa shughuli za biashara za machinga, kuondoa
kero nyingine na kuondosha huduma za chakula kwenye vichocholo vya wazi na
magenge sehemu mbalimbali zisizoruhusiwa kuwepo huduma hiyo.
“Wamiliki wa maduka tumeisha wapatia muda wa kutosha na
kuwatangazia kuwa wanatakiwa kupunguza kero za kutoweka bidhaa zao nje ya
maduka, kuweka mapipa ya plasitiki ya kuhifadhia taka pamoja na kuhakikisha
mitaro iliyo mbele ya maduka yao
haichafuliwi kwa taka ngumu au maji kutuama”alisisitiza
Aliyataja maeneo yasiyoruhusiwa kwa shughuli za
wafanyabiashra wadogo kuwa ni maeneo yote ya Mzunguko wa Mjini kati karibu na Benki Kuu ya Tanzania (BOT)
barabara ya Nyerere hadi Nyamhongolo, Pamba kuanzia mzunguko wa mnara wa
Nyerere, barabara kuelekea Kanisa Katoliki la Bugando hadi maungiyo ya barabara
ya Kenyata.
Barabara zingine alizitaja ni Rwagasore, Lumumba, Karuta,
Kenyata, Stesheni ya Reli, Soko kuu la Mjini kati, eneo la stendi ya zamani ya Tanganyika
pamoja na maeneo yote ya watembea kwa miguu kwa barabara za Nyerere,
Kenyata,Uwanja wa Ndege, Aghakan na kwenye nyumba za ibada za madhehebu
mbalimbali.
Mkurugenzi Hida alisema kuwa maeneo yaliyotengwa yataendelea
kutumiwa na wafanyabiashara wadogo kuwa ni maeneo ya Mirogo (Community Center),
Makoroboi, Uchochoro wa Tanganyika ,Stendi
ya zamani ya Mkuyuni, barabara ya vitunguu soko kuu, Asante moto, barabara ya Pamba
chini (Daraja-White Pub), Market
Street na Stendi ya Nyegezi.
“Biashara ya samaki haitaruhusiwa kwenye maeneo hayo na
watakao kwenda kinyume na maelekezo ya mpango huo wa kuwapanga wamachinga na wafanyabiashara wamiliki wa maduka makubwa na madogo Jiji litatumia sheria kuhakikisha
taratibu hizo zinafuatwa na halitakuwa tayari kukubaliana na wanasiasa kutumia
mwanya wa kuwarejesha kwa manufaa ya kujipatia umaarufu”alisisitiza.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.