Mbaspo watawazwa mabingwa ARS Mbeya
Kama ilivyotarajiwa, timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Mbaspo jana ilitawazwa kuwa mabingwa wa Airtel Rising Stars mkoa wa Mbeya baada ya kukusanya pointi nne sawa na mahasimu wao Mbosa lakini wakiwa na magoli mengi ya kufunga. Timu ya Mbeya Secondari haikupata hata pointi moja katika mtanange huo wa kusaka vipaji
Mbaspo walianza mbio zao za kutwaa ubingwa kwa kutoshana nguvu ya 3-3 dhidi ya Mbosa siku ya Jumatatu Juni 24 kabla ya kufanya mauaji makubwa ya 6-0 dhidi ya timu dhaifu ya Mbeya Sekondari siku ya Jumanne. Michezo yote imefanyika kwenye uwanja wa Magereza jijini Mbeya.
Mbosa walifikisha point nne juzi Jumatano walipoitandika Mbeya Sekondari 3-0 hivyo kumaliza wakiwa na point nne na magoli sita wakati wapinzani wao Mbaspo wakifikisha jumla ya magoli tisa ya kufunga. Katika mechi ya juzi, magoli ya Mbosa yalitiwa kwenye kamba na Michael Mwashilanga, Riziki Juma na Julius Landa.
Wakati huo huo, chama cha mpira wa miguu mkoa wa Mbeya kimetangaza kikosi cha wachezaji 18 kuuwakilisha mkoa huo kwenye michuano ya Taifa ya Airtel Rising Stars inayoanza kutimua vumbi kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 2.
Wachezaji hao ni Ismail Yesaya, Emmanuel Alex, Gift Sanga, Jackson Mwaibambe, Boaz Mwangole, Costa Sanga, Seif Zubery, Stanley Angelo, Enock Sikaonga, Kaunda Malata, Joel Kasimila, Hamprey Nyeo, Elia Salengo, Peter Noah, Emmaneul Mtimbi, Michael Bosco, Richard Kalinga na Zamoyoni Mwashambwa.
Katika mkoa wa Morogoro, mji kasoro bahari, timu ya Moro Kids imetoka sare ya bila kufungana na Techfort katika mchezo wa kushambuliana kwa zamu uliopigwa kwenye uwanja wa shule ya sekondari ya Morogoro juzi Jumatano na kushuhudiwa na mashabiki wengi wa mji huo.
Airtel Rising Stars vile vile imeanza kutimua vumbi katika jiji la Mwanza ambapo timu ya Marsh Athletical imedhihirisha umwambe wake katika soka baada ya kuifunga Nyamagana United 2-0 kwenye uwanja mkongwe wa Nyamagana.
Timu za mikoa zimepangwa kuanza kuwasili jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki tayari kwa ajili ya kindumbwe ndumbwe cha Airtel Rising Stars ngazi ya taifa katika uwanja wa Kumbukumbu ya Karume. Wachezaji 16 watachaguliwa wakati wa mashindano hayo ili kuunda timu itakayoiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa ya Airtel Rising Stars. Nchi mwenyeji wa michuano hiyo itatangazwa baadaye mwezi ujao.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.