Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Sekondari Holili, Benson Samizi akizungumza na mwandishi wa www.thehabari.com hivi karibuni wilayani Rombo. |
Geti la mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Holili, Wilaya ya Rombo. |
Shughuli za mpakani zaathiri elimu ya sekondari Rombo
Na Thehabari.com, Rombo
SHUGHULI za biashara zinazoendeshwa maeneo kadhaa ya mpakani mwa Tanzania na Kenya katika Wilaya ya Rombo zimeathiri maendeleo ya elimu hasa kwa shule za sekondari zilizopo pembezoni mwa maeneo hayo kwa kile wanafunzi kujiingiza katika biashara hizo.
Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni wilayani hapa na mwandishi wa habari hizi umebaini baadhi ya wanafunzi katika shule za sekondari kutumika katika biashara za mipakani jambo ambalo linachangia wilaya hiyo kufanya vibaya kielimu katika matokeo hasa ya kidato cha nne.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya walimu wakuu wa shule za Sekondari za Urauri, Holili, Tanya, Nduweni pamoja na baadhi ya wadau wa elimu maeneo hayo wamesema wapo baadhi ya wanafunzi wanajiingiza katika shughuli hizo ambazo huathiri maendeleo ya taaluma.
Akizungumzia shule yake, Mwalimu Mkuu wa Sekondari ya Urauli, iliyopo Tarakea wilayani Rombo, Sim Silayo alisema shughuli za biashara zinazofanyika mpakani mwa Tanzania na Kenya eneo hilo zinaathiri taaluma kwani wapo wanafunzi ambao hujiingiza katika shughuli hizo na kusahau masomo kwa vipindi tofauti.
Alisema baadhi ya wanafunzi wanafanya biashara ndogo ndogo na wengine kufanya vibarua mpakani jambo ambalo limekuwa likichangia taaluma kushuka katika shule hiyo, hasa nyakati za kilimo na mavuno maeneo ya vijiji vya mpakani Kenya na Tanzania.
"Kuna kipindi mahudhurio yanakuwa mabaya kabisa hasa kipindi cha mavuno, kilimo na palizi...wanafunzi wanakimbilia kufanya shughuli hizo kwa kulipwa, pia si wanafunzi tu wanaofanya kazi hizi hata baadhi ya wazazi nao hujumuika kufanya vibarua upande wa pili (Kenya) kwa madai kule malipo ni mazuri zaidi ya nchini kwetu," alisema Silayo.
Kwa mujibu wa matokeo ya kidato cha nne Shule ya Urauri mwaka jana, kati ya wanafunzi 92 waliofanya mtihani huo, ni wanafunzi sita tu ndiyo waliofanikiwa kufaulu huku wanafunzi 44 wakipata daraja la nne na wanafunzi 42 wakiambulia daraja sifuri.
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Sekondari Holili, Benson Samizi alisema pamoja na sababu nyingine shughuli za mpakani zimekuwa zikichangia shule hiyo kufanya vibaya kwa kile wazazi kushindwa kuwadhibiti wanafunzi wanaporudi nyumbani na kuwa huru kufanya shughuli nyingine zinazowaathiri kitaaluma.
Alisema matokeo ya kidato cha nne mwaka jana shule hiyo ilifanya vibaya kwani kati ya wanafunzi 94 waliofanya mtihani huo, hakukuwa na ufaulu wa daraja la kwanza, daraja la pili na la tatu lilikuwa na mwanafunzi mmoja mmoja huku 39 wakipata daraja la nne na wengine 50 kupata sifuri.
Akizungumzia hali hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Rombo, Judethadeus Mboya alikiri shule nyingi kufanya vibaya hasa matokeo ya mwaka jana na kuongeza uongozi wake umeanza kuchukua hatua kukabiliana na hali zote zinazoathiri maendeleo ya kitaaluma kwa shule zake.
Alisema kwa hatua ya kwanza halmashauri ilimgharamia mkaguzi wa shule ambaye alifanya ukaguzi katika shule mbalimbali zikiwemo zilizofanya vibaya na kutoa mapendekezo.
Aliongeza kuwa ili kukomesha utoro katika shule hizo viongozi wa serikali za vijiji waliagizwa kuwashughulikia wazazi wanaoshindwa kuwabana watoto wao katika kuhudhuria shuleni, ambapo baadhi walianza kutozwa faini mtoto anapokosa shule jambo ambalo alisema limeanza kuleta mabadiliko.
Tupe maoni yako
Great article, just what I needed.
ReplyDeleteAlso visit my page :: book of ra kostenlos spielen demo