ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Thursday, February 21, 2013

CHADEMA YATISHWA NA MACHAFUKO YA KIDINI

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimehofia machafuko na umwagaji damu unaoonekana kuendelea kwa sasa maeneo mbali mbali nchini, na kusema hali hiyo inatokana na nchi kukabiliwa na ombwe kubwa la uongozi.

 Kauli hiyo imetolewa jana na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe wakati alipokuwa akifungua kikao cha Baraza la Viongozi wa Chadema Kanda ya Ziwa Magharibi, kilichofanyika jijini Mwanza, kisha kuhudhuriwa na wajumbe kutoka kanda hiyo, inayoundwa na Mikoa ya Geita, Mwanza na Kagera.

Alisema, hali ya nchi kwa sasa siyo shwari ikilinganishwa na enzi za nyuma za utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julias Kambarage Nyerere, na kwamba kuna bomu linaloweza kulipuka muda wowote kutokana na baadhi ya mambo likiwemo suala la matokeo mabovu ya elimu pamoja na dhana potofu ya udini inayoonekana kuchafua hali ya hewa.

"Tanzania bado inakabiliwa na tatizo kubwa la ombwe la uongozi. Hali ya nchi kwa sasa siyo shwari...na Watanzania wote bila kujali itikadi zetu za kisiasa tunapaswa kuungana pamoja kuinusuru nchi na machafuko yoyote yanayoweza kutokea kwa kuiondoa CCM madarakani mwaka 2015", alisema Mbowe katika hotuba yake hiyo.

Aidha aliwahakikishia wananchi kwamba, Chadema ni chama makini chenye sera thabiti na zinazotekelezeka kwa wakati tofauti na CCM, hivyo chama chake kimejiandaa kuongoza haraiki ya Watanzania katika safari ya kuingia Ikulu kupitia Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015, kwani nguvu ya umma kamwe haishindwi.
Sera ya majimbo. 
Mwenyekiyio huyo wa Chadema taifa, ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Hai Mkoani Kilimanjaro alisema, sera ya majimbo iliyoanzishwa na chama chake imelenga kushusha madaraka ya kiuongozi ngazi ya chini, badala ya madaraka hayo kubaki juu kama ilivyo kwa CCM.

Alisema, mbali na sera hiyo kulenga kushusha madaraka ngazi ya chini, pia chama hicho kimeweka mikakati maalumu ya kuhakikisha kila kijiji na kaya 30 zinakuwa wa uwakilishi ndani ya chama, na kwamba Kanda zote 10 zikiwemo nane za Tanzania Bara na kanda mbili za Visiwani Zanzibar, ni kitanzi kikubwa kitakachoiangamiza CCM kwenye chaguzi zijazo.

"Mkakati na sera hii ya majimbo ni nzuri sana katika mapambano ya kusaka maendeleo na kushusha madaraka ya uongozi ngazi ya chini. Sera hii na nyingine kadhaa ni ya kutokea Chadema, na hata kama majeshi zaidi ya 1,000 yajipange vipi hayataweza kuzuia nguvu ya umma kuiingiza Chadema madarakani uchaguzi ujao.

"Tunaposema Chadema imejiandaa kukamata uongozi tupo kwenye mstari wa ukweli kabisa. Tumejiandaa vizuri na Tanzania kwa sasa inahitaji tiba maalumu ambayo ni kuing'oa CCM madarakani", alisema mwenyekiti huyo wa Chadema, Mbowe.

Alisema, chini ya sera hiyo, chama kitaunda kamati za utekelezaji ngazi hizo za chini, kuwa na waratibu wa kila kanda husika watakaowajibika kuratibu shughuli zote na ukusanyaji wa rasilimali watu, kuwa chombo cha maamuzi ngazi hizo na baadaye rufaa yake kuwasilishwa makao makuu pale inapobidi

Hata hivyo alionya kwa kusema kwamba, kamwe hawatakubali wendawazimu wowote ule kuona Chadema nadondoka katika jukwaa la kisiasa, kwani kwa sasa asilimia kubwa ya Watanzania wanaitegemea na kukiunga mkono chama chake hicho, na kikishuka itawagharimu wananchi kwa miaka 20 kutafuta chama kingine chenye nguvu kama Chadema.

           
 Vyombo vya habari.
Katika hotuba yake hiyo ya ufunguzi wa Baraza la Viongozi wa Kanda ya Ziwa Magharibi, Mbowe alivishukia baadhi vyombo vya habari na waandishi wake hapa nchini, ambapo alisema vipo baadhi yake vikiwemo vinavyomilikiwa na Serikali au CCM vimekuwa vikificha ukweli wa mambo hata pale jamii inapohitaji kupata uelewa wa jambo fulani.

Alisema, ukwepeshaji wa ukweli huo umma ni sawa na kuwadhulumu au kuwanyima haki wananchi kupata habari kwa mujibu wa katiba ya nchi, na alivyitaka vyombo hivyo kuhakikisha vinawatendea haki wananchi kwa kueleza ukweli wa jambo, ikiwa ni pamoja na kuwakosoa watawala pale wanapokwenda kinyume na matakwa halisi ya wananchi.

"Waandishi wa habari ni watu muhimu sana katika maendeleo ya nchi. Lakini, kuna baadhi ya waandishi wa habari na vyombo vyao wamekuwa wakipindisha ukweli kwa kusema uongo!. Na hata kwenye uongo waandishi na vyombo hivi wanadiriki kuwaaminisha wananchi kwamba ni jambo la kweli.

"Suala hili siyo zuri hata kidogo. Najua vipo baadhi ya vyombo vinavyomilikiwa na wanasiasa au na serikali vinaegemea upande wa watawala kisha kushindwa kufanyakazi zake nzuri za kuuhabarisha umma habari njema na zenye ukweli mtupu. Vyombo hivi tunavitaka navyo vibadilike, muda ndiyo huu Chadema inaelekea Ikulu", alisema Mbowe.

Hata hivyo, Mbowe alitoa wito kwa wanachama, viongozi wa Chama pamoja na wananchi wote kwa ujumla, kuunganisha nguvu pamoja katika kusaka mabadiliko ya kisiasa yatakayowakomboa Watanzania kutoka katika umasikini unaoonekana kushindwa kuondolewa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM).




Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.