ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, July 18, 2012

TANZANIA TWAWEZA KUUONDOA UMASIKINI





Tanzania chini ya uongozi wa Rais Kikwete imekuwa mfano wa kuingwa katika jitihada za kuendeleza kilimo. Alipoingia madarakani tu, Rais Kikwete alibuni na kuanzisha Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo – Agricultural Sector Development Programme (ASDP).

Mpango huu wa miaka 14 unalenga kukabiliana na changamoto kuu ambazo zimekuwa zinazuia maendeleo ya kilimo nchini ikiwa ni pamoja na kuongeza matumizi ya maji na umwagiliaji, kuondokana na matumizi ya jembe la mkono na kuingiza teknolojia ya kisasa, matumizi ya mbegu bora, matumizi ya mbolea zaidi, uendelezaji wa masoko, uendelezaji wa miundombinu ya barabara za vijijini.

Mengi yamefanyika chini ya mpango huu. Wakulima, kwa mfano, wamekuwa wanapata ruzuku ya mbolea na mahitaji mengine ya kilimo. Bajeti ya ruzuku hiyo imepanda kutoka sh bilioni saba mwaka 2005 wakati Rais anaingia madarakani na kufikia sh bilioni 121 kwa sasa.

Ili kuunga mkono malengo makuu ya ASDP, zimeanzishwa programu nyingine kama vile Kilimo Kwanza ambayo inalenga kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa ASDP kwa kushirikisha sekta binafsi katika shughuli za kilimo badala ya kilimo hicho kuachwa mikononi mwa wakulima wadogo, wa kujikimu na wasiokuwa na vyanzo vya mitaji ya kutosha kwa ajili ya shughuli za kilimo.

Katika kutafuta majawabu ya baadhi ya matatizo yanayokikabili kilimo katika Tanzania, Serikali tayari imeanza mchakato wa kuanzisha Benki ya Kilimo kwa kufungua dirisha dogo la mikopo katika Benki ya Raslimali Tanzania (TIB), na iko kwenye maandalizi ya mwisho kuanzisha Soko la Mitaji na Mazao nchini kwa nia ya kuinua kwa kiwango kikubwa kipato cha wakulima na wawekezaji katika sekta ya kilimo nchini.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.