Kamanda Barrow akiwasilisha taarifa. |
Polisi jijini Mwanza kwa kushirikiana na Mamlaka ya Chakula na Madawa nchini (TFDA) kupitia ofisi zake mkoani Mwanza limefanikiwa kuwatia mbaroni watu 13 wanaojihusisha na uuzaji, usambazwaji na utengenezwaji wa madawa bandia kwa mikoa ya kanda ya ziwa.
Kati ya tarehe 28 Mei na 12 Juni 2012, TFDA ilifanya Operesheni Maalum katika maeneo mbalimbali Kanda ya Ziwa ikiwa ni mwendelezo wa Operesheni za kubaini bidhaa duni na bandia kwenye soko kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi nchini pamoja na Ofisi za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) za mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera.
Ukaguzi na upekuzi ulifanyika kwenye maduka ya dawa, kituo cha mabasi ya kwenda mikoani, nyumba za makazi ya watu, nyumba za kulala wageni na ofisi zinazojishughulisha na kuuza shajala (stationeries).
Mkurugenzi wa TFDA bw. Hiiti B. Sillo akionyesha moja kati ya kemikali maalum za kufutia lebo kwa ajili ya kugushi tarehe za utengenezwaji na mwisho wa ukomo wa bidhaa.
*Kufuatia Operesheni hii, dawa mbalimbali bandia zilikamatwa kama ifuatavyo;
1. Dawa moja yenye majina mawili tofauti kwenye lebo yaani PRAZIQUANTEL 600mg na AMODIAQUINE HYDROCHLORIDE 200mg. Dawa hii ipo kwenye makopo ya ujazo wa vidonge 100 na imeghushiwa mtengenezaji kuwa ni Tanzania Pharmaceutical Industries (TPI) Limited –Arusha.
Lebo za dawa hii zinaonesha imetengenezwa Oktoba 2011 na inaisha muda wa matumizi Septemba 2014. Namba ya toleo (batch number) haisomeki vizuri. Kuna nembo ya MSD pia kwenye lebo za dawa hii. Jumla ya makopo 117 ya dawa hii yamekamatwa kwenye nyumba ya kulala wageni iliyopo Igoma na duka linalouza vocha za simu lililoko katikati ya jiji la Mwanza.
2. Dawa yenye jina la kibiashara SULXINE & PRIMINE na jina halisi SULPHADOXINE & PYRIMETHAMINE (SP). Dawa hii ipo kwenye makopo ya ujazo wa vidonge 1000 na imeghushiwa mtengenezaji kuwa ni Micro Labs Limited – India. Lebo za dawa hii zinaonesha imetengenezwa Machi 2009 na inaisha muda wa matumizi Aprili 2013. Namba ya toleo (batch number) ni MRAG024. Namba ya usajili iliyoghushiwa na kuwekwa kwenye lebo ni TAN 07, 512 JO1E MIC. Makopo mawili ya dawa hii yamekamatwa katika maduka ya dawa baridi yaliyopo Mkuyuni (Nyamagana) na Nyanguge (Magu) mkoani Mwanza.
Wanahabari waliohudhuria usomwaji wa taarifa hiyo toka TFDA.
Kwa upande wa wataalamu wa sheria wamechangi kuwa ipo haja ya serikali kurekebisha adhabu kwa wanao thibitika kujihusisha nautengenezaji, uuzaji na usambazaji wa dawa bandia
3. Dawa yenye jina la kibiashara DIOSULPH na jina halisi SULPHADOXINE & PYRIMETHAMINE (SP). Dawa hii ipo kwenye makopo ya ujazo wa vidonge 1000 na imeghushiwa mtengenezaji kuwa ni Keko Pharmaceutical Industries (1997) Ltd - Dar Es Salaam. Lebo za dawa hii zinaonesha imetengenezwa Novemba 2011 na inaisha muda wa matumizi Oktoba 2014. Namba ya toleo (batch number) ni 051110. Kuna nembo ya MSD pia kwenye lebo za dawa hii. Makopo mawili ya dawa hii yamekamatwa mikononi mwa mtuhumiwa aliyekuwa anaisambaza.
4. Aidha, upekuzi uliofanyika kwenye makazi ya mtuhumiwa mmoja eneo la Sinai (Mabatini) Mwanza umewezesha kukamatwa kwa lebo kadhaa za dawa bandia aina ya Ephedrin, Dioerythro na Erythromycin ambapo baadhi yake ziliwahi kukamatwa na TFDA mwaka 2011 na taarifa kutolewa kwa umma.
5. Vile vile, pamoja na dawa bandia zilizokamatwa, TFDA ikishirikiana na Jeshi la Polisi na TAMISEMI pia imekamata dawa moto ambazo haziruhusiwi kuuzwa kwenye maduka ya dawa baridi, dawa ambazo hazijasajiliwa kutumika nchini, dawa za Serikali na dawa zinazotumika kutibu ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma ambazo haziruhusiwi kuuzwa kwenye maduka ya dawa binafsi.
6. Makopo tupu 62 yasiyokuwa na lebo yoyote, makopo tupu 54 yenye lebo tofauti za dawa, mifuko ya kufungia dawa katika makopo, chupa moja yenye kemikali ya kufutia maandishi na nyaraka mbalimbali pia zimekamatwa kwenye nyumba ya kulala wageni iliyoko Igoma - Mwanza. Makopo yaliyokamatwa hutumika kufungashia dawa bandia na kemikali hutumika kufutia tarehe za kutengenezwa na kuisha kwa muda wa matumizi wa dawa.
Lengo la Operesheni hii lilikuwa ni kuwabaini na kuwakamata wale wote wanaojihusisha na biashara ya dawa duni na bandia kinyume cha Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya mwaka 2003 ili hatimaye waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.