ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Sunday, June 17, 2012

MGOMO WA WAFANYABIASHARA WA SAMAKI KWA WENYE VIWANDA MWANZA WAFIKIA PABAYA

Mgomo baridi wa wafanyabiashara wa samaki wa kusitisha uuzaji kwenye viwanda vya kuchakata, kusindika na uuzaji nje vilivyopo mikoa ya Kanda ya Ziwa unaendelea kwa takribani wiki sasa mara baada ya kutolewa maazimio na msimamo mkali na umoja wa wafanyabiashara hao Jijini Mwanza.




Wavuvi na mitumbwi yao pembezoni mwa kiwanda cha TFP
Wavuvi na wafanyabiashara wa uuzaji wa samaki kwenye viwanda wamefikia hatua hiyo kutokana na kushindwa kukubaliana na wamiliki wa viwanda hivyo kutokana na kushuka kwa bei ya ununuzi wanayopewa na wenye viwanda kwa madai kuwa soko la samaki nje limekumbwa na mtikisiko wa uchumi kwa baadhi ya nchi zilizokuwa zikinunua samaki kutoka kwenye viwanda hivyo.

Wakizungumza baada ya kukutana takilibani siku tatu wakati wakihamasishana na kuweka azimio la kugoma kuuza samaki katika viwanda hivyo   baadhi ya wafanyabiashara hao wamesema kwamba wamiliki hao wameshusha bei ya ununuzi wa samaki kutoka shilingi 6000 hadi kati ya shi 3000 na 2700 kwa kila kilo moja.

Bakari Ramadhani mmoja wa wafanyabiashara hao amesema kwamba wamiliki wa viwanda hivyo kwa pamoja walibandika na kuwapatia matangazo ya kushusha bei ya kununulia samaki kwenye viwanda vyao kwa madai kuwa wanunuzi wa soko la nje wamepunguza bei kwa baadhi ya wateja wao wa mataifa ya jumuiya ya Ulaya kukumbwa na mtikisiko wa uchumi.

"Tumekutana na kuazimia kugoma ili kujadiliana kutokana na wamiliki hao kushindwa kununua samaki zetu kwa madai kuwa baadhi ya wateja wao wa mataifa ya nchi za jumuiya ya Ulaya kushusha bei ya samaki kwa kile kinachoelezwa baadhi ya mataifa hayo kukumbwa na mtikisiko wa uchumi hali ambayo wamelazimika kushindwa kuagiza bidaha hiyo kwa bei iliyokuwepo"alisema Mwakabenga.

Naye Petro Angelo ameeleza kuwa kutokana na bei ya kati ya shilingi 6000/= na sh.5500 /kwa kila kilo moja iliyokuwepo sokoni kwenye viwanda hivyo kushushwa hadi kati ya sh.3000 na sh.2700/= ikiwa ni asilimia hamsini imewapa wakati mugumu wafanyabiashara hao kwa ujumla na wavuvi wanaofanya shughuli hizo kwenye mazingira magumu ikizingatiwa ni wajasiliamali wasio na mitaji.

"Wengi wa fanyabiashara na wavuvi wamekopa fedha kwenye Taasisi za fedha,SACOS,watu binafisi na baadhi kupewa mkopo na wamiliki wa viwanda hivyo na wamekuwa wakiwakata fedha wakati wa malipo kulipia madeni hayo hivyo kushusha bei ghafla ni kuwapa hasara ikizingatiwa wao pia wamenunulia bei kubwa na kutumia garama kubwa kwa wenye makambi ya uvuvi"Alisema Angelo.

Kwa upande wao baadhi wa wamiliki wa viwanda vya samaki Jijini mwanza Bw.Vedagri Mkurugenzi wa kiwanda cha Tanzania Fishing Processing (TFP) amesema kwamba hali ya soko la nchi ambazo zimekuwa zikinunua samaki hasa mataifa ya nchi za ulaya yameshusha bei kutokana na baadhi ya nchi hizo kukumbwa na mtikisiko wa uchumi unaotishia baadhi ya nchi nyingi barani ulaya.

Ameongeza kuwa kilochotokea ni hali halisi ya mataifa hayo kuchukua bidhaa kwa kuweka mashariti ya kushusha bei hivyo nawao kama wauzaji wa nje wametoa bei ili kukabiliana na bei iliyopo sokoni kwa wakati huu ili kuwawawezesha kuendelea kuuza na kuendesha biashara hiyo kwa tija ikizingatiwa kuwa Serikali inaendelea kutoza viwango vile  vile vya kodi, gharama za umeme, mafuta na kulipa mishahara ya wafanyakazi vyote viko pale pale.

Pia amesema kuwa tatizo hilo la bei kushushwa na mataifa ya nchi za Jumuiya ya Ulaya na baadhi ya nchi za ASIA na Amerika ni la kidunia na linatokana na msukosuko wa kuyumba kwa baadhi ya nchi hizo kiuchumi hivyo lazima ieleweke na wavuvi na wafanyabiashara hao watambue hilo pia wasikimbilie kulaumu hata wamiliki wanatumia garama kubwa kuendesha viwanda hivyo.
Wafanyabiashara wakitoka kwenye mkutano na TFP ambapo hawakufikia muafaka. 
Kwa hivi sasa biashara ya zao hilo imeshuka kiasi cha kutishia mapato ya serikali na halmashauri ya jiji la Mwanza kupitia kodi na hata isijulikane nini hatma yake.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Evarist Ndikilo alipofuatwa na waandishi wa habari ili kulitolea ufafanuzi sakata hilo alisema wamelisikia na kulipokea na hivyo wanalishughulikia lakini akieleza kuwa ni suala ambalo majibu yake siyo ya haraka mpaka pale watakapoka na wamiliki hao na wafanyabiashara ili kuona jinsi ya kulimaliza mgogoro huo kwa kuhusisha pia Idara na Wizara husika .

Wavuvi na wafanyabiashara hao wanatarajia kukutana na wenye viwanda leo jioni katika ukumbi wa Hotel Monarch kujadili anguko hilo la bei ya samaki.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.