ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Monday, July 11, 2011

MABINTI WA FAMILIA MOJA WABAKWA, MMOJA AUAWA.

NA: Dinna Maningo, Tarime
WASICHANA wawili wa familia moja, wakazi wa Kitongoji cha Nyabirongo, Kijiji cha Gibaso, Kata ya Nyarukoba, wilayani Tarime, wamebakwa na watu wanaosakiwa kuwa majambazi, kisha kuwashambulia kwa kuwakatakata mapanga na kusababisha kifo cha binti mmoja.

Majambazi hao waliwavamia mabinti hao kwenye nyumba walikokuwa wamelala, waliwabaka kasha kuwakatakata mapanga na kupora Sh58,000.

Kutokana na majeraha ya mapanga waliyopata, wasichana hao walikimbizwa Hospitali ya Masanga na mmoja alifariki akipatiwa matibabu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tarime/Rorya, Deus Kato, alisema tukio hilo lilitokea Julai 7, mwaka huu saa 5:00 usiku.

Wakizungumza nyumbani kwa Mwera Wantae jana, mmoja wa mashuhuda Daniel Nyandege, alisema walisikia sauti ya yowe nyumbani hapo hatua iliyowalazimu kukimbilia eneo hilo.

“Ilikuwa muda wa saa 5:00 usiku nikasikia sauti ya yowe, ilinibidi nikimbie hadi eneo la tukio nilipofika ndani nilimkuta mama wa familia akiwa analia, huku akiwa amefungwa mikono yote miwili, nilipomuuliza aliniambia niingie ndani walikolala mabinti wake, nilipoingia nilikuta wakiwa wamejeruhiwa kwa kukatwakatwa mapanga huku nguo zao za ndani zikiwa zimetupwa chini na magauni yakiwa yamesogezwa hadi juu ya kifua, sehemu za siri zikiwa wazi,” alisema Nyandege.

Shuhuda mwingine, Mjumbe wa kitongoji hicho, Simion Chacha, alisema alipofika alishangaa kuona damu ikimiminika na kwamba, alimuona mmoja wa mabinti hao akiwa na majeraha matatu ya kukatwakatwa panga.

Hata hivyo, mabinti hao wakiwa Hospitali ya Masanga wakipatiwa matibabu, mdogo alipoteza maisha na mwingine anaendelea na matibabu.

Kamanda Kato alisema hadi sasa hakuna anayeshikiliwa kuhusiana na mauaji hayo na kwamba, polisi kwa kushirikiana na wananchi wanaendelea kuwasaka wahusika.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.