ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

ZIMA KILA KITU ILA WASHA JEMBE FM 93.7 MWANZA

Wednesday, September 8, 2010

Mamia ya wafungwa wametoroka jela NIGERIA.

Mamia ya wafungwa wametoroka jela moja iliyo eneo la kati la Nigeria baada ya genge lenye silaha kuvamia gereza.

Wakuu wa Nigeria wanadai kuwa kundi lenye msimamo mkali wa Kiislamu, Boko Haram ndilo lililohusika na shambulio hilo.

Imethibitishwa kuwa watu wanne waliuawa na wengine sita kujeruhiwa.

Polisi sasa wanasaka baina ya watu mia saba na mia nane katika Jimbo la Bauchi.

Wahalifu hao wenye silaha walivamia jela na kuingia kila chumba wakiwaachilia huru wafungwa kabla ya kulichoma moto jengo zima la gereza.

Wakuu hao wanasema taarifa za kijasusi zinaonyesha kuwa kundi la Boko Haram lenye msimamo mkali unaopinga elimu ya magharibi na sayansi ndilo lililohusika.

Takriban wafuasi 100 wa kundi hilo walikuwa ndani ya jela hiyo wakisubiri hukumu kutokana na ghasia za mwaka jana dhidi ya polisi na serikali ya Nigeria.

Wakati huo zaidi ya watu 800 waliuawa na kiongozi wa kundi hilo Mohammed Yousef akauawa kwa risasi baada ya kuizingira nyumba yake.

Lakini katika siku za hivi karibuni kundi hilo limejigamba kuwa na kiongozi mpya na kwamba lina mipango ya kujiimarisha kwa silaha.

Kuna khofu kwamba kundi hilo linatumia mbinu mpya na ujanja na huenda limehusika katika 'mawaji baridi' ambamo maofisa kadhaa wameuawa kwa kupigwa risasi na watu wenye silaha wakitoroka kwa kutumia kasi ya pikipiki.


KWA HISANI YA BBC SWAHILI.

Tupe maoni yako

0 comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.