PICHANI Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Meja mstaafu Bahati Matala, wa pili kutoka kulia mstari wa mbele akipeana mkono na Meneja Mahusiano na Serikali wa African Barrick Gold, Philbert Rweyemamu.
HABARI KAMILI:-Mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu umetoa msaada wa shilingi milioni 50 kwa waathirika wa mafuriko wilayani Bukombe na pia kusaidia wilaya hiyo katika kuanzisha Mfuko wa Maafa.
Akikabidhi hudi ya fedha hizo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Meja mstaafu Bahati Matala, Meneja Mahusiano na Serikali wa African Barrick Gold, Philbert Rweyemamu, amesema kampuni imeguswa na maafa hayo ya mafuriko katika wilaya ya Bukombe.
“African Barrick Gold haiko nchini kwa ajili ya kuchimba madini pekee, bali pia kuisaidia jamii katika shughuli za maendeleo na kubwa zaidi wakati wa matatizo pia,” alisema Rweyemamu.
Rweyemamu alisema ABG kama mwekezaji katika sekta ya madini nchini Tanzania, itaendelea kufanya kazi na serikali katika kuhakikisha kuna maendeleo endelevu katika jamii inayozunguka migodi yake na kutoa msaada wa aina yoyote kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya aliipongeza BGML kwa kuitikia haraka wito wa kutoa msaada na kuongeza kuwa fedha hizo zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Alifafanua kwamba, msaada huo utazilenga kaya 421 katika vijiji vya Lelembela na Kabanga kata ya Ikunguigazi ambazo nyumba zao zilibomolewa na mafuriko kutokana na mvua kubwa zilizonyesha Aprili 2 2010.
Kadhalika mvua hizo pia zilisababisha vifo vya watu watatu na daraja lililopo kati ya Runzewe na Ushirombo katika barabara kuu iendayo Rwanda na Burundi kusombwa na maji, hali iliyosababisha barabara hiyo kufungwa kwa siku mbili.
Jumla ya hekari 4,700 za mazao pia ziliharibiwa na mvua hizo.
Msaada huo wa fedha utatumika kununulia mahitaji muhimu kwa wananchi ikiwa ni pamoja na madawa, chakula, mahema na vitanda.
Tupe maoni yako
barrick ni kampuni ya kinyonyaji inayoangalia maslahi yao, mfano wanaangalia kitu wanaita safety na siyo health hivyo vituo vya matibabu wameweka siri kubwa ukifika una matatizo ya kifua,mapafu au madhara ya sumu wakwambie huna tatizo hadi utakapokufa mwenyewe, sasa hii ni hatari serikali kama inatupenda itusaidie.
ReplyDelete