
Watoto wawili wamepoteza maisha baada ya moto kuteketeza nyumba waliyokuwa wakiishi katika Mtaa wa Katanini, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomaji, amesema watoto hao ni wana wa wakili wa kujitegemea, Caessar Shayo.
Kaimu Kamanda Zimamoto amewataja watoto waliopoteza maisha kuwa ni Jerial Shayo (4) na Leoni Shayo (2), pia kulikuwa na majeruhi baba na mama wa watoto hao na kwa sasa wanapatiwa matibabu rufaa ya Kanda ya kaskazini,
Kamanda Jeremiah amesema tukio hilo lilitokea majira ya saa nne asubuhi, ambapo kwa mujibu wa mashuhuda, watoto hao walifariki dunia muda mfupi baada ya kupewa uji na dada wa kazi.
Naye, Mwenyekiti wa Mtaa wa Katanini, Ester Mekiesia, amesema alipokea taarifa za moto huo kutoka kwa wananchi na mara moja alichukua jukumu la kutoa taarifa kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kuokoa hali hiyo.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Erick Pessa, amesema walifika eneo la tukio baada ya kusikia kelele za kuomba msaada.
Amesema walipofika waliwakuta wanawake wawili waliowaeleza kuwa watoto walikuwa bado ndani ya nyumba iliyokuwa ikiteketea kwa moto.
"Kulikuwa na mkanganyiko mkubwa juu ya watoto walipokuwapo, hivyo waliingia ndani ya nyumba kuanza kuwasaka. Walianza jikoni bila mafanikio, wakaelekea sebule ya kwanza na chumba cha kulala lakini hawakuwapata kutokana na moshi mzito uliokuwa umetanda.
…Baadaye walilazimika kutoka nje na kuvunja dirisha kubwa ili kuingia tena ndani, ambapo waliwakuta watoto hao wakiwa wamekumbatiana pembeni ya chumba, tayari wakiwa wamefariki dunia,"amesema Michael
Aliongeza kuwa mama wa watoto alikuwa nyumbani wakati tukio linatokea, lakini moto ulikuwa mkubwa na maji hayakutosha, hali iliyosababisha kuchelewa kuwaokoa watoto hao.
Aidha, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amemjulisha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kuhusu tukio hilo katika kikao cha ushauri cha mkoa, akibainisha kuwa watoto wawili wamepoteza maisha kufuatia moto ulioteketeza nyumba hiyo.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, limewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya majanga ya moto na kutoa taarifa mapema pindi moto unapotokea ili kusaidia juhudi za uokoaji na kupunguza madhara.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment