
TIMU ya taifa ya wanawake ya Tanzania ‘Twiga Stars’ imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ‘Léopards Dames’ katika mchezo wa kirafiki leo Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam.
Mabao ya Twiga Stars leo yamefungwa na wacheza wa FC Juárez ya Mexico, mshambuliaji Opah Clement Tukumbuke dakika ya 26, beki Julitha Aminiel Tamuwai Singano dakika ya 43 na kiungo mshambuliaji wa Al Nassr ya Saudi Arabia, , Clara Cleitus Luvanga dakika ya 47, wakati bao pekee la Chui Jike limefungwa na mshambuliaji wa TP Mazembe ya kwao, Lubumbashi Esther Dikisha Bushiri dakika ya 90.
Ulikuwa mchezo wa pili kuzikutanisha timu hizo ndani ya tano, baada ya Ijumaa pia Twiga Stars kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 hapo hapo Azam Complex, mabao ya Twiga Stars yote yakifungwa na Clara Luvanga dakika ya 28 na 88, wakati bao pekee la Léopards Dames lilifungwa na Esther Dikisha dakika ya 72.
Michezo hiyo ni maandalizi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) kwa timu zote ambazo zinatarajiwa kufanyika nchini Morocco kuanza Julai 5 hadi 26, mwaka huu.
Tanzania imepangwa Kundi C pamoja na Afrika Kusini, Ghana na Mali, wakati DRC ipo Kundi A pamoja na wenyeji, Morocco, Zambia na Senegal na Kundi B kuna Nigeria, Tunisia, Algeria na Botswana.
Tupe maoni yako
0 comments:
Post a Comment